February 03, 2018

GARETT AGUSTUS MORGAN: MJASIRIAMALI ALIYEVUMBUA TAA ZA KUONGOZEA MAGARI BARABARANI.

Na Kizito Mpangala

Garett Morgan alizaliwa mwaka 1877 katika kitongoji cha Claysville mjini Kentucky nchini Marekani akiwa na asili ya Afrika yaani. Baba yake alikuwa mtumwa aliezaliwa katika kitongoji cha Huntsville mjini Alabama. Baba yake alikuwa mtumwa kwa kurithishwa na wazazi wake waliokuwa watumwa. Miaka kadhaa baadae baba yake, John Morgan akawa Luteni Kanali wa jeshi la Marekani, Brigedia Jenerali katika jeshi la Kentucky kwa lazima. Mama yake Garett Morgan pia alikuwa mtumwa kama mume wake.

Garett Morgan alipofikia darasa la sita katika shule ya Brach Elementary mjini Claysville akiwa na umri wa miaka 16 alikwenda katika kitongoji cha Cincinnati mjini Ohio kutafuta kazi itakayompa ujira ili kupata mahitaji yake. Aliajiriwa mashambani.

Kama ilivyokuwa kawaida ya watoto wengi nchini Marekani wakati huo, Garett Morgan alilazimika kuacha shule akiwa darasa la sita na kuamua kufanya kazi katika mashamba kutwa nzima. Kutokana na bidii yake katika kazi, aliletewa mwalimu awe anamfundisha hapohapo shambani ambako ndiko yalikokuwa makazi huku akiendelea na kazi za shambani huko. 

Alifundishwa ufundi na baadae akawa fundi mahiri wa kutengeneza mashine za kushonea nguo yaani cherehani. Uzefu huo wa kutengeneza cherehani aliuheshimu na kujifunza zaidi jinsi mashine zinavyofanya kazi. Kazi yake ya kwanza kuvumbua ilikuwa ni cherehani inayotumia mkanda kama cherehani za sasa. Alivumbua cherehani hiyo tofauti na za mwanzo zilizokuwa zikizungushwa kwa mikono.
Mwaka 1907 Garett Morgan alifungua kiwanda chake kidogo ambapo alikuwa akitengeneza viatu, hasa kushona viatu vilivyochanika na kushona nguo kwa mashine alizoziunda yeye mwenyewe. Mwaka 1909 alimuoa Mary Anne ambaye kwa pamoja waliamua kuipanua biashara yao ya ushonaji nguo na viatu na walifungua duka lililoitwa Morgan’s Cut Rate Ladies Clothing Store. Aliwaajiri wafanyakazi 32 katika duka hilo, walishona makoti, suti, magauni,  na nguo nyinginezo.


Mwaka 1910 hobi yake ya ufundi iliwaka zaidi nafsini mwake na alipenda kujifunza kutokana na kazi za wavumbuzi waliomtangulia. Ndipo alipovumbua koti la usalama livaliwalo na askari wa zimamoto ili kujikinga na moshi. Koti hilo lina mpira maalumu wa kupitishia hewa. Hapo alianzisha kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya usalama, iliitwa National Safety Device Company mwaka 1914. Alipata tuzo ya uvumbuzi wa koti hilo kutoka katika taasisi ya kimataifa ya wahandisi wa zimamoto (International Association Of Fire Engineers).  

Mwaka 1913 kabla ya kuanzisha kampuni ya vifaa vya usalama, Garett Morgan alifungua duka lililokuwa na bidhaa za nywela kama vile mafuta, mashine za kuakushia nywele, chanuo na kadhalika. Vingi kati ya hivyo viliundwa na yeye mwenyewe. Duka hilo hilo likawa kubwa na ikawa kama kampunia ambapo aliiita G. A. Morgan Hair Refing Company.


Mwaka 1913 pia, Garett Morgan alikerwa na ajali mbalimbali alizokuwa akizishuhudia barabarani. Nia ajali za magari, pikipiki na baiskeli pia. Ndipo alipotafakari ili kupata ‘dawa’ ya kumaliza au kupunguza ajali hizo. Magari, baiskeli, mikokoteni, maguta, na waenda kwa miguu walilazimika kushiriki barabara kwa pamoja kutokana na kutokuwepo njia za pembeni kama ilivyo katika barabara za sasa.


Mwaka 1922, Garett Morgan alishihudia ajali mbaya katika makutanao ya barabara, na akamua kuanza zoezi la kuunda taa za kuongozea watumiaji wote wa barabara, yaani magari, baiskeli, maguta, mikokoteni, bajaji na waenda kwa miguu. Aliunda kifaa hicho chenye taa tatu zenye rangi tofauti. Alipata haki miliki mwaka 1923 ingawa aliambiwa wapo waliotangulia kuvumbua taa kama hizo lakini hazikuwa bora kama hizi za kwake. Baada ya uvumbuzi wa Garett Morgan kukubaliwa mwaka 1923, aliuza uvumbuzi huo katika kampuni ya umeme ya General Electric Company iliyoanzishwa na mwanasayansi Tomas Edison na wenzake kwa kiasi cha dola 40,000 sawa na shilingi milioni themanini (80,000,000/=) za sasa za Tanzania. Aliamua kuiuzia kampuni hiyo kwa sababu yeye alikuwa ametoa mchoro tu na kuwapa maelekezo ya kina kuhusu utendaji alioufikiria wa taa hizo ambazo tunaziona leo barabarani. 
Mchoro wa taa za kuongozea watumiaji wa barabara. 



Mwaka 1908, aliamua kuwasaidia wenzake ambapo alianzisha Taasisi ya Watu Wenye Rangi mjini Cleverland (Cleverland Association of Coloured Men). Sababu ya kuanzisha taasisi hiyo alifikiria kuwakwamua kiuchumi na kijamii wale wote waliokuwa na asili ya Afrika katika eneo alilokuwepo. Alikuwa akitunza faedha katika taasisi hiyo ambapo baadae iliitwa NAACP (National Association for the Advancement of Coloured People) ambayo iliweka makzi yake katika kitongoji cha Baltimore mjini Maryland na kuwa na wanachama 300,000. Garett Morgan alikifadhili chuo cha Negro ambacho kilianzishwa kwa ajili ya watu weusi kutosajiliwa katika vyuo vya umma.

Mwaka 1916 alisaidia kuanzishwa kwa gazeti la Cleverland Call na mwaka 1920 alianzisha klabu maalumu kwa ajili ya watu weusi tu. Klabu hiyo iliitwa Wakeman Country Club. Mwaka 2002 Garett Morgan alijumuishwa katika kitabu cha “100 Greatest African Americansí” kilichoandikwa na Molefi Kete Asante profesa wa Africolojia (Africology) katika chuo kikuu cha Temple.

Mwaka 1931 aligombea uongozi katika halmashauri ya jiji la Cleverland kama mgombea binafsi akiwa na lengo la kuwakilisha watu weusi katika halmashauri hiyo na alikuwa mtu wa kwanza mweusi kumiliki gari mjini Cleverland. Alifariki mwak 1963 akiwa na umri wa miaka 86.

© Kizito Mpangala (0692 555 874)


No comments:

Post a Comment

Maoni yako