NA MARKUS MPANGALA
NIMEANDIKA safu hii leo baada ya kusoma Hotuba
ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyosomwa na waziri
Profesa Makame Mbarawa mjini Dodoma. Kwa mujibu Tovuti ya Mkoa wa Ruvuma inaeleza
kuwa Wilaya ya Nyasa iliyopo mkoni humo, ilianzishwa rasmi mnamo Machi 2012 baada ya kumegwa kutoka wilaya ya Mbinga.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mheshimiwa Stella Manyanya |
Aidha, eneo la wilaya hii liko kando ya Ziwa
Nyasa. Makao makuu ya wilaya yako mjini Mbamba Bay. Wakati wa sensa ya mwaka
2012, wilaya ya Nyasa ilikuwa na wakazi 146,16. Vilevile wilaya hiyo ina jumla ya Kata 16 ambazo
ni Chiwanda, Kihagara, Kilosa, Kingerikiti, Liparamba, Lipingo, Lituhi, Liuli, Liwundi,
Luhangarasi, Mbaha, Mbamba Bay,Mtipwili,
Ngumbo, Nindai,na Tingi.
Kwanini ninamkumbusha Mbunge wa Jimbo la Nyasa,
Mama Stella Manyanya? Nitaeleza sababu za msingi kwa madhumuni ya kumsaidia
vipaumbele katika jimbo lake.
Sekta ya kwanza; Babaraba;
Tunakubaliana kuwa wilaya hii inazo barabara kuu
tatu; ambazo ni chanzo cha mawasiliano pamoja na ukuaji wa uchumi unaounganisha
na wilaya nyingine.
Barabara ya kwanza ni Mbinga-Mbamba Bay, ya pili
ni Mbinga-Lituhi (ambayo inaanzia njia panda inayounganisha wilaya tatu; Songea,
Mbinga na Nyasa yenyewe) na ya tatu ni Lituhi-Mbamba Bay. Mipango ya kuinua
maisha ya wakazi wa wilaya hii inatakiwa kujikita kwenye ujenzi wa barabara
hizo kwa awamu ya kwanza.
Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya wizara ya ujenzi,
uchukuzi na mawasiliano kipengere cha “Sekta ya Ujenzi” kifungu cha 37 kutoka
“Miradi ya Barabara na Madaraja”, serikali imesema kuwa mradi wa Barabara ya
Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa Kilometa 66 utaanza kujengwa.
Taarifa nilizonazo ni kwamba ujenzi huo utaanza
mwezi Juni mwaka huu. Kwangu ninaamini hii taarifa iliyochelewa na isiyo na
lolote jipya, pengine inakera zaidi kuisikia kuliko kawaida. Nakumbuka wakati wa uzinduzi wa Stendi Kuu ya
Mbinga na Barabara ya Peramiho-Mbinga yenye urefu wa Kilometa 78, Julai 19, mwaka
2014 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete
alibainisha suala la ujenzi wa barabara hiyo.
Ilielezwa kuwa ujenzi huo utafanyika kwa
kutokana na ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB). Benki hiyo inagharimia
ujenzi wa barabara hiyo ya kiwango cha lami kati ya Mbinga na Mbamba Bay. Lengo ni kukamilisha ujenzi wa kiwango cha lami
wa barabara ya ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor) kati ya Mtwara na Mbamba Bay
yenye kiasi cha kilomita 823.
Mradi wa Mtwara Corridor ulipangwa mwanzoni mwa
mwaka 2000. Kutokana na kusuasua kwa mradi huo umesababisha hata jirani zetu
Malawi watukimbie katika ushirikiano wa kibiashara na uchumi kupitia bandari ya
Mbamba Bay. Mwanzoni mwa miaka hiyo Meli za abiria na mizigo
za Malawi mfano Mv. Ilala ilikuwa inatia nanga bandarini Mbamba Bay, lakini kwa
sasa hali ni tofauti. Bandari hiyo ingeliweza kuingiza bidhaa kutoka Msumbiji
kuja Tanzania na kinyume chake. Bahati mbaya kukosekana kwa barabara rafiki
kumesababisha tukimbiwe.
Ukizitazama bajeti za toka mwaka 2012 pale
wilaya (au jimbo) ilipoanza unabaki kushangaa, vipaumbele vyetu katika wilaya
hii vilikuwa nini? Mathalani, kutoka mwaka 2014 kumekuwa kumekuwa na bajeti
tofauti.
Utawala wa awamu ya tano uliwasilisha bajeti ya kwanza
ya mwaka wa fedha 2016/2017 lakini barabara hii haijakamilika. Serikali ya
awamu ya tano imewasilisha bajeti ya pili ya mwaka wa fedha 2017/2018 na
kubanisha kuwa ujenzi unatarajiwa kujengwa.
Ukijumlisha utaona tangu mwaka 2000 kumekuwa
“barabara itajengwa’. Kila awamu tunajibebesha ‘excuse’ ambazo zinadhoofisha
mapato ya wilaya ya Nyasa. Inadhoofisha uchumi wa wananchi wa jimbo husika. Sitegemei kuona Mbunge wa Jimbo hilo akija na
‘excuse’ ifikapo mwaka 2020 kwasababu kumekuwa na uahirishwaji usiokuwa na
maelezo yanayojitosheleza. Aidha, sasa tunafahamu mfadhili husika wa mradi huu,
ukicheleweshwa lawama kwa Mbunge na chama chake.
Wataalamu wa masuala ya habari tunasema ‘habari
ni biashara na uchumi’. Wimbi la habari za wilaya ya Nyasa limezidi kuchanua
kuliko miaka ya nyuma. Kwa sasa wananchi wa jimbo la Nyasa wanafahamu kuwa kipande
cha eneo la Ndengu kwenda Nyasa hapatiki, isipokuwa wanasafiri kwasababu ya dhiki
na shida walizonazo hata kuhatarisha usalama wao.
Maisha ya wananchi wa mji wa Buruma hususani kitongoji
cha Sisi kwa sisi mambo yamezidi kuwa magumu na haitashangaza siku moja kuona
hawana mawasiliano na makao makuu ya wilaya au kufanya shughuli za uchumi
kutoka Mbinga kwenda Mbamba bay.
Mawaziri wa awamu ya tano wamefanya ziara maeneo
yanayogusa wilaya ya Nyasa. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo
alitembelea machimbo ya Makaa ya Mawe yanayofanywa na TANCOAL huko Amanimakoro,
Mbinga.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na miundombinu,
Edwin Ngonyani alimhakikishia mbunge wa Nyasa kuwa ujenzi wa barabara utaanza
mara moja kama ambavyo Ilani ya CCM 2015-2020 inavyoelekeza.
Naibu waziri wa Nishati na Madini, Medard
Kalemani, alitembelea mji wa Liuli mnamo Februari 15 mwaka huu aliahidi kuwa nguzo
za Umeme zitaanza kuwekwa mjini humo na vitongoji vyake lakini hadi hii leo
hakuna chochote. Kwahiyo namkumbusha Mbunge wa Jimbo la Nyasa
hayo mambo kwa moyo mkujufu kwamba yasiwe sababu ya kuanza kunyosheana vidole.
Sisi wengine kazi zetu ni kuandika. Tutaandika
barabara ya Mbinga-Lituhi ni mbovu, huku Makaa ya Mawe yakiwa bidhaa muhimu
inayohitajika kuinua uchumi wa wilaya ya Nyasa. Tutaandika kuwa gati lililojengwa bandari ya
Ndumbi kando ya barabara ya Lituhi-Mbamba Bay wilayani Nyasa halitakuwa na
maana kama barabara hiyo inayotarajiwa kutumika itaendelea kuwa mbovu.
Aidha, ninamkumbusha Mbunge kuwa kutoka mwaka
2000 hadi leo kumekuwa mipango na Ilani vilevile lakini hakuna
lililokamilishwa. Ninamkumbusha kuwa Daraja la Yungu linaounganisha miji ya Puulu
na Liuli katika Barabara ya Mbamba bay-Lituhi limeharibika.
Itaendelea …
No comments:
Post a Comment
Maoni yako