February 03, 2018

GEORGE CRUM: MPISHI MASHUHURI ALIYEVUMBUA CHIPSI YA VIAZI

NA KIZITO MPANGALA

Alizaliwa mwaka 1824 katika mji wa Saratoga, sasa ndilo jiji la New York nchini Marekani. Alijishughulisha na uwindaji na upishi katika migahawa ilikuwa katika milima ya Adirondack. Alifanya shughuli hizo kwa bidii lakini baadae alielekeza nguvu zake zaidi katika upishi. Jina lake lilikuwa ni George Speck. Kutokana na jina la uchepe kushamiri zaidi ambalo ni Crum, aliamua kujiita George Crum.

Baba yake aliitwa Abe Speck ambaye alikuwa mhamiaji kutoka Kentucky kwenda Saratoga. Akiwa Saratoga alimuoa mwanamke mwenye asili ya India ambapo baadae George alizaliwa. 

Bidii yake ilipoonekana zaidi, alichukuliwa na tajiri mmoja katika mgahawa ulioitwa Moon’s Lake House, karibu na maporomoko ya maji ya Saratoga. Mgahawa huo uliaminika kuwa ndio wenye gharama za juu za chalula. Hapo ndipo ujuzi wake wa upishi ulipofahamika na watu wengi zaidi. Licha ya kuwa na gharama za juu katika mgahawa huo watu walipenda kufika kwa wingi kutokana na umahiri wa George Crum katika upishi wake.

Bada ya kufanya kazi kwa muda mrefu katika mgahawa huo, George aliamua kumchukua dada yake ili wafanye kazi pamoja kutokana na ukata ulioikumba familia yao. Walikuwa ni wenye rangi mchanganyiko.

George na dada yake walifanya kazi pia katika mgahawa wa Sans Souci ambapo walijikita zaidi na upishi tu. Mteja mmojawapo katika mgahawa huo alikuwa ni bwana Commodore Cornellius Vanderbilt ambaye ahkulijua jina la George wala dada yake, lakini kilichomfanya afike mgahawani hapo mara nyingi ni kutokana na utamu wa chakula kilichokuwa kikipikwa na George Crum.


Mwaka 1860, George Crum aliamua kufungua mgahawa wake mwenyewe ambao aliuita Crum katika maeneo ya miinuko ya Storey karibu na Malta jijini New York nchini Marekani. Umahiri wake katika mapishi ulihitajika sana katika migahawa iliyokuwa maeneo ya maporomoko ya maji ya Saratoga ambapo kulikuwa na watalii wengi waliohitaji chakula kilichopikwa na yeye.

Tahamani yake ilipaa zaidi katika upishi hasa katika migahawa ya kisasa wakati ule iliyokuwepo katika jiji la New York. Lakini aliamua kuendelea na mgahawa wake ambapo chakula alichokuwa akipika mgahawani hapo kiliwezekana kwa urahisi kwa kuwa alikuwa akipata mazao kutoka katika shamba lake.  Hivyo, George Crum alikuwa mwangalifu zaidi katika matumizi ya mazao yake shambani ambayo alikuwa akiyachakata na kupika chakula mgahawani kwake. Katika kila meza mgahawani hapo alikuwa akiweka bakuli la chipsi chakula ambacho kiliwavutia wengi.

Gerge Crum hakuwa mtu wa kuulizwa maswali mara kwa mara katika mgahawa wake kwa kuwa alipanga kanuni imara ambazo zilimsaidia kutotumia muda mwingi kuongea na wateja. Vile vile hakujali sana masuala ya ubaguzi wa rangi. 

Katika mgahawa wake huo, George Crum hakupenda kufanya upendeleo usio na manufaa. Hivyo yeyote aliyeingia na kuhutaji huduma alipaswa kufuata utaratibu uliopangwa katika mgahawa huo. Mamilionea wengi walipenda kufika mgahawani hapo na walilazimika kufuata utaratibu uliowekwa. Bwana Commodore Cornellius kutokana na mapenzi yake katika mgahawa huo alikubali kusubiri chakula hata kwa saa nzima.

George Crum alikuwa mashuhuri sana kutokana na kupenda kukaanga viazi ambavyo alikuwa akivikata kwa umbo la mduara na vyembamba ambavyo ndivyo chipsi. Hapo ndipo palipowavutia wateja wengi kutokana na aina mpya ya chakula hicho. Mbinu hii ya ukataji viazi ilichapishwa kwenye vitabu mbalimbali ambavyo vilimpaisha George Crum katika uga wa upishi. Katika kitabu cha The Cook’s Oracle kilichoandikwa na William Kitchiner, kimeeleza mbinu hiyo ya kukaanga viazi.

George Crum alianza kukaanga viazi katika mtindo wa chipsi tangu alipokuwa akifanya kazi kwenye migahawa ya Saratoga lakini wengi hawakutilia maanani sana lakini iliitwa Chipsi ya Saratoga (Saratoga Chips) ambayo ilifahamika baadae mwanzilishi wa chakula hicho ni George Crum. Hii ni kutokana na kuona chakula cha aina ile katika mgahawa wake, hivyo kumbukumbu ziliwarejea weteja wengi kwamba waliwahi kuona chakula kama kile mjini Saratoga. 

George Crum alifariki mwaka 1914. Dada yake alifariki mwaka 1924 akiwa na umri wa miaka 102. Machapisho ya majarida mengi yaliandikwa yakimtaja dada yake George Crum ndiye mwanzilishi wa chakula aina ya chipsi lakini mwanzilishi mkuu ni George Crum katika mgahawa wa Saratoga alikokuwa na dada yake. 

Dada yake George Crum alipohojiwa kuhusu chipsi alieleza jinsi kaka yake alivyoivumbua bila kutarajia chakula kizuri namna ile. George Crum alipokuwa akikaanga viazi, kipande kimoja kwa bahati mbaya kiruka na kutua chini lakini kilikuwa kimeshaiva ndipo alipokiokota na kuweka kwenye sahani kisha akakionja. Baadae akamwambia dada yake kwamba ni chakula kizuri hivyo analazimika kukaanga vingi zaidi.

George Crum alisaidia kuifanya chpsi ijulikane na watu wengi alipokuwa Sartoga na baadae alipofungua mgahawa wake mwenyewe. Baadae alidai haki miliki ya uvumbuzi wa chipsi ambapo alianza kuiuza kwa kuweka kwenye pakiti maalumu zilizokuwa na muundo wa umbo la pia. Baada ya wateja kuongezeka, alitengeneza maboksi madogo madogo kwa ajili ya kuwekea chipsi hizo. 

Mwaka 1973 kampuni ya kutengeneza pakiti za kuwekea chipsi ilitoa simulizi kuhusu mvumbuzi wa chipsi, na ilichapishwa katika majarida ya taifa, Fortune na Time. Na katika jarida la Western Folklore, ilichapishwa simulizi hiyo ambapo ilisema chimbuko la chipsi ni huko Saratoga, New York. Kutoka hapo chipsi ikawa maarufu sana, pia, mteja maarufu wa chipsi katika mgahawa wa Saratoga bwana Commodore Vanderbilt alihamia Malta ambako George Crum alifungua mgahawa wake. Sababu ya kuhamia Malta ilikuwa ni kufuata chipsi za Ceorge Crum.

© Kizito Mpangala (0692 555 874)

No comments:

Post a Comment

Maoni yako