December 30, 2017

PUGU HADI PERAMIHO; Kijiji cha Dar, Utemi wa Wangoni na kumbukizi maridhawa.

Katika kitabu cha "PUGU HADI PERAMIHO" kuna masimulizi ya kutoka mwaka 1888-1988 na ujio wa Wamisionari wa kijerumani kupitia Shirika lao la Benedictine Fathers lenye makao yale mjini Peramiho kwa sasa.  
Kitabu hiki ni mkusanyiko wa barua na kumbukizi binafsi (Diaries) zilizoandikwa na Mapadre, Mabruda, Masista wakielezea masuala ya ukoloni wa Kijerumani, Injili, Umisionari, Wapagazi, Wangoni na kupenda vita na starehe pamoja na mahusiano ya kibadamu kati ya wazungu na waafrika.

PADRE ANDREAS AMRHREIN
Kitabu hiki kinaanza kwa maandiko ya Abate Lambert Doerr, OSB. Kwanza "Abate" ni wadhifa waliopewa wakuu wa mashirika ya Benedictine Fathers. Lambert anafungua pazia la masimulizi ya Wamisionari Wabenediktine kusini mwa Tanzania. 


Lambert anasimulia kwa ufupi historia ya Padre Andreas Amrhein, mzaliwa wa Uswisi na Monaki wa Monesteri ya Beuron kusini mwa Ujerumani alivyoanza kusuka mapokeo ya Wabenediktine kupitia St. Ottilien na safari zao barani Afrika hususani Dar es salaam hadi Ziwa Nyasa. Anaelezea juu ya Askofu Kasian Spiss alivyoongoza taasisi katikati ya vita vya majiamji. 


Naweka dondoo;
MPUTA GAMA; Alizaliwa na kukulia Malawi sio kama inavyodhaniwa alizaliwa Afrika kusini hususani Jimbo la Limpopo. Baba yake alikuwa Gwazerapasi aliishi uhamishoni katika Falme za Wangoni wa Mbelwa (Mombera).

Kwa mujibu wa kitabu hiki kumbukumbu za Nduna Adam Mtazama Gama b.Mkulayedwa ndizo zinaonyesha alitokea Malawi.
DOAG; Lilikuwa shirika la kibiashara la kundi Fulani la Wajerumani wakiwa chini ya Mwenyekiti Dk. Peters na Karl von Gravenreuth.
LANGERNBURG; ni jina la zamani la mji wa Kyela (Mbeya). Jina hilo pia lilitumika kwa mji wa Tukuyu kwakuwa ulipewa jina moja(Jimbo).
KIJIJI CHA DAR ES SALAAM; Dar es salaam hadi mwaka 1888 kilikuwa kijiji chenye wakazi 2000 tu. Kati yao Wahindi (200), Waarabu (150) na Watumwa (500). Hapakuwa na hotel, hivyo Wamisionari walitegemea nyumba ya kampuni ya kijerumani ya DOAG ya Dk. Karl Peter.

MIKAEL HOFER OSB
Ndani ya kitabu hiki nimevutiwa na Bruda Mikael Hofer OSB ambaye aliwasili Julai 4, mwaka 1890. Huyu ana maandiko mengi humu. Kumbukumbu zake nyingi zimetengeneza kitabu hiki kwa asilimia 70. Anasimulia matumizi ya Wapagazi ambao hata wamisionari walilazimika kuwatumia. 

Anaelezea namna magonjwa ya manjano,kuharisha na malaria yalivyosababisha Vifo. Anasimulia juu ya urafiki wake na Sultani Motto aliyekuwa kiongozi wa kijiji cha Moto kilichokuwa katika msitu wa mto Ruvu.
Anasema katika kipindi hicho watoto walichukuliwa utumwani. Walikuwa wadogo sana, baadhi walikuwa na miaka minne lakini waliuzwa utumwani. Hapakuwa na matibabu kwa wapagazi waliougua njiani. Bruda Hofer OSB ndiye alianzisha Misioni ya Lukuledi pamoja na Tosamaganga ambako walikumbana na ugonjwa wa Tauni. Ni hayo tu kwa ufupi.

FUNZO; Kitabu hiki kimetokana na "Diary" na barua walizokuwa wakiandikiana wahusika. Namna walivyokuwa wakiweka kumbukumbu katika "diary" zao kwa kuelezea shughuli pamoja na mikakati. Na sasa simulizi zao zinaleta Elimu ya historia, Mazingira, Afya na kadhalika.
CHANGAMOTO: Yapo machache yameninyima taarifa za kutosha katika masimulizi yao. 

© "Bruda" Markus Mpangala OSB
Lundu, Nyasa
Disemba 21, 2017.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako