December 30, 2017

TUWENI KAMA NYOKA.

NA SAMWEL CHITANYA, SONGEA.
Pamoja na kwamba wafamasia na wanasayansi wakuu hawajavutiwa sana na utafiti Wa chanjo na matibabu ya nyoka ili waweze kuendeleza kizazi chao hapa nchini, lakini kwa upande wao wenyewe nyoka wamezidi kujitahidi kufanya kazi ya kuhakikisha kizazi chao hakipotei. Hizi ni juhudi na maarifa binafsi ya nyoka. Nyoka wamethubutu.
Sasa kinachotakiwa mtu binafsi si kama unawapenda nyoka au la, bali ni jinsi gani unaweza kuishi nao. Lazima uhakikishe hupotezi mwelekeo dhidi ya sheria za mchezo. Kuna falsafa ya muumini anayekwenda kuungama kanisani kuwa ameiba mbuzi, lakini huku muumini huyo akiendelea kufaidi minofu na supu ya mbuzi aliyemuiba. Huu ni mzaha na utani katika mambo ya msingi.


Niwaombe radhi Watanzania wenzangu kwa kuwasihi kuwa muwe nyoka kama mnadhani ni tusi, lakini hilo siyo tusi. Nyoka ni mnyama anayesadikiwa kuwa mwerevu sana. Wagiriki au Wayunani na Wayahudi walimpenda sana nyoka kwa kuwa kati ya wanyama wote walioumbwa na mungu yeye anasadikiwa kuwa mwerevu kuliko wote. Nyoka yeyote yule hata asiye na sumu lazima anajua jinsi gani ya kujilinda dhidi ya adui. Nyoka anaweza kukuachia mwili wake wote ukaupondaponda kadri utakavyoona inafaa, lakini atajitahidi sana kukwepesha chake kisijeruhiwe hata kidogo. 

Nyoka pia wana mitego mingi ya kukamata vitoweo vyao. Nyoka wengi wanakawaida ya kujivua magamba kama mbinu na asili yao ya kuruhusu ukuaji zaidi. Ni Mara chache sana kumkuta nyoka Wa aina fulani amemuua nyoka wa aina Nyingine wakiwa katika mawindo yao ya kutafuta vitoweo. Wanaweza kugombana sana lakini si kuuana. Hili ni tofauti na sisi binadamu( Watanzania) ambao tunauana Mara kwa Mara, kumbe tulitakiwa tugombane pasipo kuuana maana migongano na mifarakano ni sehemu ya maisha ya kiumbe chochote kile.
Kila mmoja wetu inampasa kuwa ajigeuze kuwa nyoka ili aweze kuishi na nyoka wenzake kwa sababu baadhi ya Watu wanakiri wamekuwa nyoka. Jambo hilo liendane sambamba na kuvaa sifa alizonazo nyoka na mambo afanyayo.
Wagiriki pia waliamini kuwa njiwa na kondoo ni wanyama wapole sana kuliko wanyama wengine wote. Walisisitiza pia watu wawe wapole kama njiwa au kondoo, lakini wasiache kuwa waerevu kama nyoka. 


Nyoka wanatupatia njia Nyingine ya kukabiliana na haya tuliyo nayo. Nyoka hawana kawaida ya kupiga kelele kama ndege. Nyoka wengi hutenda mambo yao kimya kimya, lakini utasikia mtu analalamika eti ameumwa na nyoka. Kinywa ni silaha na dawa ya nyoka. Nyoka humwangamiza binadamu kwa sababu ya kelelel zake. Binadamu akiona nyoka huanza kupiga kelele nyingi akisema: yule pale nyoka, yule pale fisadi, piga nyoka huyo piga nyoka huyo, piga huyo mla rushwa, piga!! piga!! pigaaa!! Ponda kichwa kabisa!!! 


Binadamu( Watanzania) tusivyokuwa werevu, Anaweza kupiga kelele zote hizo wakati hana Hata silaha yoyote mkononi ya kifikra au kimaada ya kumuulia nyoka huyo.

Nyoka asikiapo kelele za namna hii hujua kabisa hawa ni binadamu ambao wana kelele nyingi kama hizi pasipo na vitendo, basi huweza kuamua kumng'ata mtu mmojawapo au kukimbia. Hapo utasikia tena binadamu akipiga kelele zake kama kawaida, nyoka amekimbia!! Huyo anaenda!!! 

Kimya kikuu ni dawa ya nyoka. Kumbe ilitakiwa binadamu amuonapo nyoka ajaribu kuwa mtulivu kama yeye alivyo, kisha atafute silaha pasipo hata kupiga kelele kabisa, kisha ampige vizuri kichwani hadi afe kabisa; biashara asubuhi mhasebau mwachie mungu jioni.

Nyoka humuuma mtu kwa nia ya kumuua baada ya kuwa amepigiwa kelele na kuchokozwa. Nyoka huwauma watu pasipo kutoa sumu yake kwa wale ambao huwa hawajapiga kelele na kumchokoza, na jeraha litokanalo na na nyoka Wa aina hiyo huwa halina madhara yoyote. 

Kuna nyoka baadhi hutoa mluzi au sauti Fulani kama kipyenga, hawa huwa ni wale walioshiba kwa kitoweo walichokipata( Wao ). Usikiapo sauti ya ajabu ajabu kama kipyenga isikilize kwa makini na uangalifu mkubwa usije kimbilia huko(kujiingiza kwenye mambo tusiyoyajua kichwakichwa) ukadhani kuna kandanda linachezwa huko maana utaumwa na kufa hapo hapo. 

Nyoka Wa aina hiyo waogope sana. Yaani unafyata mkia wako na usizungumze chochote kama kweli unataka kuishi. Lakini kama unataka kuwa shujaa katika kijiji chako,jitoe mhanga kama UPATU kumuua nyoka Wa namna hii. Kila mmoha atakushukuru sana na kukuita shujaa. ( unaweza kuchagua kuwa shujaa au kuishi maisha yako ).

Kuna nyoka wengine wakiwa wanajivua magamba huwa wanatoa harufu kama ya ubwabwa au wali uliopikwa vizuri. Ndugu yangu uhusipo harufu ya ubwabwa au pilau kutoka vichakani au kwenye nyasi ndefu,usifurahie na mate yasianze kukutoka na kuanza kupekuapekua huku na huko kutafuta sufuria hilo la ubwabwa ukidhani kuna mtu alilificha huko. Acha tamaa za ubwabwa zipite maana yatakukuta makubwa. 

Heri ujisemee moyoni mwako kuwa sidanganyiki kwa harufu ya ubwabwa( Wakati mwingine ni bora kujifanya Mjinga kuliko kuhatarisha maisha yako).
Kila mtu anaalikwa sasa kuwa nyoka( siyo lazima ) ili aishi vema na wenzake. Ili mwenzako akisema nimejivua gamba moja Leo, na wewe unamjibu mami nilijivua magamba kumi jana.!!!!. Akikudanganya kwa harufu ya ubwabwa, mwambie sidanganyiki kwa harufu, ninajua ubwabwa Wa joka una sumu ndani yake!!!!! Wasubiri muda wao unakaribia watakuja. Jiandae!!! Wahenga walisema "Alimaye bondeni hujulikana kwa Moshi". #1820.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako