October 21, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU CHA UHAMASISHAJI

KITABU: ISHINDE TABIA YA KUGHAIRISHA MAMBO
MWANDISHI: JOEL NANAUKA
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA


JOEL NANAUKA ni miongoni mwa waandishi wazuri katika vitabu vya uhamasishaji na utambuzi. Kitabu chake cha “Ishinde Tabia ya Kughairisha Mambo” kimechapishwa na kampuni ya Benison Communication &Printing iliyopo Dar es salaam na kupewa nambari za usajili ISBN 978-9987-761-99-9.


Msingi wa kitabu hiki unaanza kupatikana katika utangulizi wake ambapo mwandishi anaandika, “Unakumbuka wakati watu wametangaziwa kujisajili kwaajili ya kupiga kura? Unakumbuka watu walivyotangaziwa kuhusu usajili wa vitambulisho vya utaifa? Ni siku gani watu walijaa zaidi? Bila shaka, utakumbuka ni siku ya mwisho hata kama waliliona tangazo. Kuna watu kila siku wanatuma maombi ya kazi siku ya mwisho hata kama waliliona tangazo hilo miezi miwili kabla. Kuna watu kila wakati watatuma ripoti yao siku ya mwisho, kuna watu kila wakati kazi waliyopewa kufanya wataiwasilisha dakika za mwisho” (uk.2).

Sura ya kwanza ya kitabu hiki inaeleza tabia za baadhi ya watu kupanga mipango fulani na kushindwa kutekeleza. Mathalani mtu anapanga kutekeleza jambo fulani lakini kabla hajaanza au akifika nusu ya jambo lenyewe anaahirisha. Mwandishi anatumia utafiti wa Profesa Joseph Ferrari ambaye aligundua kuwa takribani asilimia 20 ya watu duniani ni waahirishaji wakubwa wa mambo yao. 

Kwa mfano, mtu anataka kununua saruji kwaajili ya kujiandaa kwa ujenzi wa nyumba, pengine inahitajika mifuko 150, lakini yeye ananunua 50, na kuahirisha ujenzi kisha anasema ataanza mwaka mwingine. 

Mwandishi amebainisha taswira halisi katika maeneo ya kazi. Anasema wapo wafanyakazi ambao hawapendi kutekeleza kazi zao kwa wakati badala yake wanasubiri hadi dakika za mwisho ndipo waanze kuhaha huko na huko. Kimsingi tabia hizi zinazozungumzwa zinawagusa watu kila kaliba. Haijalishi umri wala nasaba au jinsia.

“Unaweza ukachukua daftari lako kuandika, ama ripoti yako ama hata kusoma kitabu, ukaamua kuwa unafanya unachotaka kwa nusu saa bila kuyumbishwa na kitu chochote, ghafla baada ya dakika 10 unajikuta nunashika simu na unasema ngoja niangalie meseji, kuja kushtuka unajikuta umeshatumia takribani nusu saa kuperuzi mitandao na hamu ya kuendelea na kazi uliyokuwa unaifanya inapotea kabisa. Ama wakati mwingine unasema ngoja niangalie TV kidogo kisha nitalala ama nitasoma kidogo, kuja kugundua unakuwa umeshafika saa 7 usiku na umeshindwa kuondoka kwneye TV yako. Ni kitu gani kinasababisha uamue jambo moja na kisha ujikute umefanya kitu tofauti,”(uk.9).

Katika muktadha huo mwandishi anakumbusha kuwa wapo watu wanaoishi kwa kuahirisha. Wengine ambao hadi wakumbushwe ndipo hutekeleza jambo fulani. Wapo watu ambao hawezi kujikita kwenye eneo husika. 

Tunaweza kutumia dhana ya “kutanga tanga kimawazo”. Kwamba anayetanga tanga kimawazo anakuwa na vitu vinavyovuruga zaidi utaratibu wa utendaji wa kazi. Hali ya kutanga tanga kimawazo huchochea uvivu na uzembe. 

Mathalani unaweza kuona mtu anajishughulisha kupika jikoni, kwakuwa anajua itachukua dakika takribani 5 au zaidi, anakwenda sebuleni kutazama TV au kukaa mbali na jikoni ili afanye kitu kingine kisichohusika na mapishi. Katika hali kama hiyo unaweza kushuhudia mtu huyo akikurupuka alikokaa na kukimbilia jikoni kutazama anachokipika baada ya kugundua kuwa ameunguza. Mara nyingi vitu vinavyosababisha hayo ni vile tunavyodhani ni vinatupatia raha na kadhalika.

Ili kubaini hilo mwandishi ameeleza tabia za watu mbalimbali na namna wanavyoweza kuahirisha mambo. Wengi wao hukosa nidhamu ya muda, wana mambo mengi yasiyokwisha (sababu ya kutotekeleza kwa wakati na kulimbikiza majukumu), wanatatizo la kulipua mambo, na wanakosa vipaumbele.

Sura ya pili anazungumzia tabia zingine zinazochochea kuahirisha mambo ni kutenda jambo katika dakika za mwisho ambayo huchochea presha kubwa. Pia watu wenye tabia hizo hawafanikiwi kwasababu wanaendeshwa na maoni ya watu. 

Anasema wapo watu ambao wanaogopa kulipia gharama za uamuzi wao hivyo wana tabia ya kuahirisha mambo. Ili kufahamu zaidi yaliyomo katika sura za tatu, nne na tano ni vema msomaji akitafuta kitabu hiki na kujipatia elimu.

Nihitimishe kwa kumkumbusha mwandishi juu ya matumizi sahihi ya maneno ya Kiswahili. Usahihi ni “Kuahirisha” si “kughairisha. Mwandishi wa habari na nguli wa Kiswahili, Amabilis Batamula, anasema “Naomba nisahihishwe kipengele cha lugha kama nakosea, maana na mimi kwa kupenda kuhariri nimeshajishtukia. Hilo neno kughairisha linatumikaje hapo? Ninavyofahamu mimi kuahirisha ndio ‘Procrastination’, kusogeza sogeza, na kughairi ni kubadili mawazo na kuacha kufanya ulichokwisha amua kufanya. Nisahihishwe tafadhali.”.

1 comment:

  1. Nafasi kati ya neno na neno ni kubwa mno.

    ReplyDelete

Maoni yako