NA
MWANDISHI WETU
“ULIKUWA
unafanya nini ulipokuwa na umri wa miaka 31? Hiyo ni sentensi ya kwanza iliyoandikwa
na Mwanahabari wa Televisheni ya CNN, James Masters, kwenye tovuti ya CNN.
Sentensi hiyo ilinivutia zaidi, ingawa aliendelea na mengine, lakini staili
pekee haikuwa kivutio, bali mtu aliyekuwa akizungumzwa alivutia zaidi.
Mwandishi
James Masters alikuwa anamzungumzia kijana mmoja aitwaye Sebastian Kurz kutoka
Austria. Ni kijana ambaye anazidi kuvutia duniani kutokana na siasa zake ambazo
kwa namna moja au nyingine ziliibua nchi hiyo kwenye ramani ya kidiplomasia.
Baada
ya hapo nililazimika kufuatilia habari zaidi za Sebastian Kurz. Niliyokutana
nayo ni somo, ingawa kwa Tanzania lilianza muda mrefu.
Nimekuandalia
makala haya msomaji ili kujifunza jambo katika malezi ya familia na taifa kwa
ujumla. Austria ipo tayari kwa kiongozi kijana? Fuatilia.
Kijana
huyu alizaliwaAgosti 27, mwaka 1986. Kwa sasa ana umri wa miaka 31 tu. Yeye ni
mwenyekiti wa chama cha Austrian People’s Party (OVP) tangu Mei, mwaka huu.
Baba yake ni Josef Kurz, ambaye alikuwa injinia. Mama yake ni Elizabeth Kurz,
ambaye kitaaluma alikuwa mwalimu. Amekulia katika jiji la Vienna, ambalo ndilo
makao makuu ya serikali na mji wa kibiashara nchini humo. Sebastian ni muumini
wa Kanisa Katoliki. Anatajwa kuwa ni Mkatoliki mhafidhina.
Miaka ‘mitatu mitatu’ ya
dhahabu
Baaadhi
ya wazungu wanahusudu sana mchezo wa namba. Katika mchezo wa soka namba 13
inatajwa kuwa yenye mkosi. Mifano mbalimbali inatolewa, lakini hali hiyo ni
tofauti kwa miaka mitatu mitatu ya dhahabu kwa Sebastian. Iko hivi, mwaka 2009,
akiwa na miaka 23, alichaguliwa kuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama cha
OVP.
Aidha,
Sebastian alipokuwa na miaka 24 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa
Austria. Miaka mitatu baadaye alipotimiza miaka 27, yaani mwaka 2013, aliteuliwa
kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Katika kipindi hiki aliwahi kuitisha mkutano wa
mawaziri 30 wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Ulaya uliofanyika nchini
Austria. Mnamo mwaka 2014, alichaguliwa kuwa mbunge kupitia chama cha OVP.
Kutoka
umri wa miaka 24 hadi 27, tofauti ni miaka mitatu. Kutoka umri wa miaka 27 hadi
31, tofauti yake ni miaka mitatu na nusu. Hii ina maana wakati mwaka huu ukiwa
wa tatu tangu akabidhiwe cheo cha uwaziri wa mambo ya nje, amechaguliwa tena
kuwa Kansela wa Austria.
Kwanini amekuwa Kansela?
Katika
umri wa miaka 31, Sebastian Kurz anakabidhiwa majukumu makubwa ya kuiongoza
Austria, baada ya rais wa nchi hiyo, Alexander Van der Bellen, kumuomba aunde
serikali ya kitaifa na chama kingine cha Freedom Party. Uchaguzi
uliofanyika mwaka huu ulikipatia chama chake cha OVP asilimia 31.4 ya kura
zote. Vyama vingine vilipata alama zifuatazo; Freedom Party (27.4%) na Social
Democrats (26.7%). Kutokana na ushindi huo,
haukumwezesha kuunda serikali, hivyo kulazimika kuungana na chama cha
Freedom Party kuunda serikali.
Ni mtaalamu wa nini?
Sebastian
ana shahada ya sheria aliyopata kutoka Chuo Kikuu cha Vienna mara baada ya
kumaliza mafunzo ya lazima ya Jeshi la Kujenga Taifa la Austria.
Mdogo kama Kim, Macron
Nchini
Ufaransa walijivunia kiongozi mwenye umri mdogo zaidi, Emmanuel Macron (39).
Nchini Korea Kaskazini pia wanajivunia kiongozi mdogo zaidi, Kim Jong-Un, mwenye
umri wa miaka 33. Pamoja na Canada ambao walimpa waziri mkuu mdogo kuliko wote,
Justin Trundeau mwenye umri wa miaka 45.
Pia ni kama Leo Vardarkar mwenye umri wa miaka 38 na raia wa Ireland,
ambaye aliteuliwa kuwa waziri wa Usafirishaji, Utalii na Michezo mwaka 2011.
Naam,
wananchi wa Austria wanamwona Sebastian Kurz kama Emmanuel Macron, Justin
Trudeau, Leo Vardarkar, Kim Jong-Un kutokana na umri mdogo, lakini wamebeba
matumaini makubwa ya uongozi wa nchi zao.
Nyerere, Salim na Kabila
Katika
suala la uongozi hapa nchini pia zipo rekodi za viongozi vijana. Mwalimu Julius
Nyerere alikabidhiwa urais akiwa na miaka 40. Salim Ahmed Salim alikabidhiwa
ubalozi wa Misri akiwa na miaka 22. Naye rais wa sasa wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, aliukwaa urais akiwa na miaka 29 tu. Kwa
namna fulani utaona kuwa, dunia imekuwa na mabadiliko ya hapa na pale kwa
viongozi wengi vijana kukabidhiwa majukumu makubwa. Sababu kubwa ni kwamba,
wanakuwa na vitu vya ziada kuliko wengine pamoja na kuaminiwa au kuwa sehemu ya
mtandao wa wanasiasa wenye kukabidhiana madaraka.
Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika ya habari.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako