RAYMOND NDOMBA, SONGEA |
Mawazo yangu
ni haya; Pamoja na sababu nyingi zilizosababisha matokeo hayo ya aibu kubwa.
Wazazi wanapaswa kubeba lawama kubwa. Wengi wao hawafuatilii maendeleo ya
watoto wao, pia makuzi na malezi mabaya.
Miaka
ya hivi karibuni (kuanzia mwaka 2000), Wazazi wengi katika wilaya ya Nyasa
hawajali elimu, hawajigusi katika ufuatiliaji wa watoto wao kielimu na hata
kitabia (Angalia matokeo ya mitihani ya Taifa ya shule za msingi na sekondari
kunzia miaka hiyo ya 2000 kwa shule kongwe ndani ya wilaya).
Wazazi
wanapenda tu kuona mtoto anakwenda shule ila sio kufuatilia ili afahamu mtoto
huyo anafanya nini huko shuleni. Hawajigusi hata kujua kama mtoto kalala ndani
au yuko wapi nyakati za usiku (saa 1 adi 6 usiku). Binafsi katika janga hili,
asilimia 75 za lawama zangu nazielekeza kwa wazazi.
Mwezi
wa 8 na 9, 2017 nimekaa sana Nyasa. Nimetembelea Tingi, Chimate, Kwambe,
Likwilu/Kilosa, Mango, hadi Lituhi; katika maeneyo yote niliyopita wazee kwa
vijana wako sambamba na wanzuki (Mabobo). Muda wote na siku zote za wiki wao ni
mitungi tu.
Sehemu
kama Kwambe, Matenje, Mtipwili, Ruhekei, Kilosa, Maporomoko Liuli, Lundu,
Mbaha, Lituhi nk; nimeshuhudia wazee kwa vijana wakiwa wanakunywa komoni/wazuki
(Mabobo) kuanzia saa 2 asubuhi. Wazazi wengi wamejiweka mbali kabisa na mambo
yanayo husu taaluma.
Kwao
kazi ya malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wao kitaaluma ni jukumu la
mwalimu. Kitu ambacho si sahihi. Kila mwana Nyasa aliangalie tatizo hili kwa
jicho la pekee. Tukawaelimishe wazazi wetu, ndugu zetu na watoto wetu juu ya
umuhimu wa ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya kitaaluma na kitabia ya watoto
wetu waliopo shuleni.
Katika
hili, binafsi napingana na wale wanaoelekeza lawama zao kwa Mbunge wa Jimbo la
Nyasa, Stella Manyanya. Tatizo hapa lipo kwetu wenyewe (wana Nyasa). Ili
tuitatua changamoto hii, yatupasa tuanze kuangalia upya makuzi na malezi ya
vijana wetu kuanzia ngazi ya familia pamoja na kufuatilia mienendo yao kitabia
wakiwa nyumbani na hata shuleni.
Hatuwezi
pata matokeo chanya kwa watoto wenye tabia hasi, hatuwezi pata vijana wenye mitizamo
ya kimaendeleo toka kwa familia isiyo fuatilia malezi, makuzi na mienendo ya
mtoto wao kitabia na kitaaluma na hatuwezi pata matokeo chanya toka kwa
viongozi wa elimu wenye uwezo mdogo kitaaluma.
Baadhi
ya wakuu wa shule na maafisa walishindwa kwenda kujiendeleza kitaaluma kwa nia
ya kulinda vyeo vyao. Na baadhi yao walichangia sana kushuka kwa kiwango cha
elimu kwa vile walikuwa wanashindwa kusimamia majukumu yako ipasavyo na wengine
kushindwa kuwawajibisha walimu wengine walio wazidi kitaaluma.
Baadhi ya Majengo ya Mbamba Bay High School yakiendelea kujengwa. |
Tukiacha
kubadilika na kuchukua hatua mapema hata hiyo “Mbamba Bay High School” ambayo
inajengwa kwa kasi na majengo ya kisasa, itakuwa ni jiko la kuwapika vijana
toka nje ya wilaya ya Nyasa.
Mwaka 2016 vijana wa kidato cha
nne Lundo Sekondari waligoma kufanya mitihani ya muhula kwa madai eti
itawapotezea muda wa kujisomea kwa ajili ya maandalizi ya mtihani wa Taifa.
Nini chanzo cha tabia kama hii na wanafunzi wale walitoa wapi ujasiri wa
kuwagomea walimu wao? TABIA TABIA TABIA.
Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu James cha Mtakatifu Agustino-Songea, Ruvuma
Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu James cha Mtakatifu Agustino-Songea, Ruvuma
No comments:
Post a Comment
Maoni yako