October 27, 2017

NIYONZIMA SIO MSAADA MBELE YA MASHUTI YA NDEMLA


NA. HONORIUS MPANGALA
 
SAID NDEMLA

ILIKUWA ni Oktoba 20, 2013 ambapo mechi ya watani hawa wa jadi ilikuwa na matokeo ya kushangaza mashabiki. Mchezo ulimalizika kwa sare ya bao tatu kwa tatu. Hadi wanaenda mapumziko ilikuwa tayari Yanga anaongoza goli tatu zilizofungwa na Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza aliyerudi nyavuni Mara mbili. Kila kitu kwa Simba kilienda vibaya ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Wale waliokuwa na ushabiki uliopitiliza waliamua kuondoka uwanjani kwa kujua dhahama ya kichapo iko upande wao. Ikumbukwe ni msimu mmoja nyuma yaani 2011/12 Simba alitoka kuwafunga Yanga bao tano bila. Hivyo wengi waliamini zinarejeshwa ile oktoba 20. 


Ilikuwa Simba iliyoongozwa na Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kihwelo. Maamuzi ya kuusoma mchezo na kufanya maamuzo ambayo mashabiki walifikia hatua ya kulaumu kwa nini yanafanyika kwa wachezaji wale kiliwazidishia wasiwasi mashabiki. Bechi la Simba liliwainua William Lucian na Said Hamis Ndemla kuchukua nafasi za Abduhalim Humud na Haruna Chanongo.
Ilikuwa ni wasaa wa vijana hawa waliotoka katika kikosi cha vijana cha Simba kuwadhihirishia wapenzi na mashabiki wao kuwa walimu hawajakosea kuwaingiza mchezoni baada ya kubaini mapungufu yaliyokuwepo kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza. 

Ndemla alilishika dimba vyema kwa kukaba na kupiga pasi ndefu na fupi. Mambo yalibadilika ndani ya muda mfupi alioingia kwa eneo la kiungo. Aliwapoteza viungo wa Yanga akiwemo Haruna Niyonzima aliyesumbua kwa dakika 45 za awali. 


Hakutakuwa na la kustaajabisha kama utamsikia Ajibu akisema namkubali sana Ndemla na wakati huohuo Ndemla akisema anamkubali sana Ajibu. Hawa vijana ni vipaji tofauti na tunavyo watathimini katika mzani mwepesi kiasi hicho.

Ndemla alimfanya kocha wa Yanga wakati huo Erne Brandts ajikune kichwa pasipo kuwasha na nywele zake. Dakika ya 53 Bertram Mwombeki aliwainua mashabiki wa Simba kwa kupachika bao safi akipokea pasi toka kwa Amiss Tambwe. Wakati goli linapatikana ilikuwa Yanga wameendeleza kosakosa nyingi langoni mwa Simba.

Mabadiliko ya kiakili kwa sehemu ya ulinzi wa kati kwa Simba kulileta matunda kwani mrundi Gilbert Kaze na Mganda Joseph Owino walisimama vyema. Umakini wao ulifanya Ndemla ulifanya kazi kubwa ya kuunganisha timu kwa kusaidiana na Jonas Mkude akiwa ni kijana mwenzake toka timu ya vijana ya Simba ambayo ilichukua ubingwa wa Uhai na kuinyanyasa Mtibwa kwenye mashindano ya BancABC.

Yanga walipotezwa na Ndemla hakukuwa cha Niyonzima wala Mbuyu Twite katika eneo la kiungo,wote wakabaki wanafukuza kivuli cha kijana yule mwenye wajihi wa upole ambao kwa Ndemla kulikuwa na tafsiri ya tofauti katika miguu yake. Anapiga mashuti akiwa nje ya eneo la kumi na nane anatawanya vyema mipira kwa wakati.
'Show' ilikuja kushangaza zaidi baada ya goli la pili kwa Simba dakika ya 57 lililofungwa Joseph Owino. Kila kitu kilibadilika. Kila mchezaji aliamini inawezekana kushinda mchezo. Kona ya Ramadhani Singano ilitua katika kichwa cha Kaze na kuandika bao la tatu dakika ya 84. Ndani ya dakika zilizobaki ilikuwa Yanga ndo walitamani mchezo umalizike.
Kila mpenzi wa Soka kumbukumbu yake kwa Ndemla inaanzia katika mchezo ule. Kwa kipindi chote kiungo Huyo amekuwa na kiwango bora na kile kile kila anapopewa nafasi huonyesha kile alicho nacho. Unaweza kusema kama hana bahati na Makocha wanaoinoa Simba kwani makocha walio onyesha kumuamini na kumpa muda mwingi wa kucheza alikuwa ni Patrick Lewig na Goran Kopunovic ambao waliamini sana vijana katika kikosi cha Simba.

Licha ya kuwa kipenzi cha mashabiki ka ilivyo kwa Jonas Mkude lakini bado Kocha Omog hajampa muda mwingi wa kucheza huku nafasi yake ikionekana ikichezwa sana na James Kotei,Mzamiru yassin na Haruna Niyonzima. 

Katika kutazama jicho la kiufundi ingefaa sana kama Omog akaamua kumwanzisha Ndemla badala ya Niyonzima kama inavyokuwa. Haruna ni mchezaji mkubwa na mwenye uwezo mkubwa sana lakini kwenye mechi kubwa amekuwa akipania sana mchezo husika. 

Rejea katika mechi za Yanga dhidi Azam ambapo aliwahi kupata kadi nyekundu katika moja ya mechi dhidi ya timu hiyo. Pia alikuwa anapata wakati mgumu sana katika pambano la Simba na Yanga hadi kufikia hatua ya kutuhumiwa kutumika na klabu aliyoko sasa. Lakini kumbe kiufundi ilikuwa ni kuzidiwa au wapinzani kumfahamu soka lake na kumdhibiti barabara. 

Mechi ya ngao ya jamii ni moja ya mechi ambazo niliona Haruna akiendela kukamia 'kupaniki' kwenye mchezo akihitaji kufanya kitu dhidi ya Yanga lakini akawa anashindwa kwasababu ya kukosa utulivu wa akili. Katika Michezo sita aliyocheza Haruna hajawa nachango mkubwa sana katika matokeo ya Simba kutokana aina yake ya kiuchezaji kufahamika sana na wapinzani wake. Soka la shoka hapo ndipo unapoweza msababishia kadi Haruna kwasababu ya kutawaliwa na hasira.

Ulikuwa ni wakati wa Ndemla tena kupewa jukumu la kusimama mbele ya Mkude au Kotei ili awaongoze wenzake namna ya kucheza zilipendwa ya wasafi.Kwanza ni mtulivu wa akili pili ana uwezo wa kumudu hasira tatu ni mchezaji asiye na mambo mengi dimbani mtazamo wake unakuwa katika kulitafuta goli liliko.

Nyakati zote ninazo tazama mechi za Simba anapoingia Ndemla mashabiki hufurahia sana tofauti na zile hali zinazoweza jitokeza za kulaumu mabadiliko. Sababu kubwa mashabiki ni kwamba Ndemla anauwezo mkubwa wa kupiga mshuti kuelekea kwenye lango la wapinzani. 

Hilo halina ubishi awapo uwanjani anabadilisha mchezo toka falsafa ya Simba iliyozoeleka ya kupiga pasi nyingi na badala yake wanakimbia kwa kasi kuelekea lango wapinzani. Apatapo nafasi ya mpira nje eneo la goli hupiga mashuti makali kitu ambacho washambuliaji na viungo wengine hawafanyi hivyo.
Rejea mabadiliko ya Ndemla dhidi ya Mbao,Mtibwa na Azam alikuwa mtu kujaribu kupiga na ndio kawaida yake ya soka analolihusudu. Kila kiungo anakuwa na utambulisho wake awapo uwanjani. Nakumbuka sana alipoingia akitokea bechi kawenye mchezo wa Tanzania dhidi ya Malawi katika uwanja wa Taifa. Alipokonya mpira toka kwa mchezaji wa Malawi huku akiwa karibu na Himid Mao. Akadanganya kama anauruka ule mpira kumwachia Himid halafu akaukanya na kusonga nao huku akiwaacha wachezaji wa malawi wakitaka kumkaba Himidi. Mashabiki walilipuka kwa Shangwe na wakisema "huyu mtoto Fundi".

Licha ya kocha kuwa na uamuzi wake kwa kuwa na 'game plan' Fulani anapoikabili timu pinzani. Suala la kutazama mchezo upi unamfaa mchezaji yupi ni jema pia. Uchu alionao Ndemla katika kuendelea kuwaaminisha mashabiki wa Simba kwa yeye ni yuleyule wa Oktoba 20, 2013 anatamani sana kuudhihirisha katika mechi kubwa kama dhidi ya Yanga. 

Sura yake na kazi yake dimbani hukupa wasaa wa kuliona soka lote aheli wangecheza wachezaji wenye sura kama yeye. Maamuzi yatabaki kwa Mwalimu katika kutazama kikosi chake na kuamua ni yupi acheze. Hakuna ubishi kuhusu eneo ambalo kocha Omog anapata kigugumizi kupanga kikosi chake kama eneo la kiungo.

0628994409

No comments:

Post a Comment

Maoni yako