Hivi karibuni kocha
mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametoa mipango mizuri kwa maendeleo ya soka.
Kim ameliambia shirikisho la soka nchini kuwa anahitaji kuona kikosi cha timu
ya taifa ya vijana Serengeti Boys ikishiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania
Bara.
Kocha Kim anasema,
mpango wake ni kutaka kuona wachezaji hao wanakuwa wanacheza mechi za ushindani
kwa kila wiki ya mwezi ili kuweza kujijenga kiushindani na kimbinu. Kwa mujibu wa kocha
huyo, anasema kama wachezaji wa Serengeti Boys wataweza kucheza mechi moja kwa
wiki, kisha wakafanikiwa kushiriki michuano yote ya Ligi Kuu basi hakuna shaka
kabisa watakuwa kwenye ushindani mkali watakapopewa nafasi ya kuchezea timu ya
wakubwa.
Kocha Kim anasema,
wachezaji hao vijana wanatakiwa kuchezea timu ya taifa kwa muda kisha
wakifikisha umri wa kuvuka Serengeti
Boys basi watarudishwa kwenye klabu zao ili kupisha wengine waweze kutumika
katika kikosi hicho na kushiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Dhumuni la kocha huyo
ni lilelile kuwafanya wachezaji wengi vijana wakipata nafasi na kucheza soka la
ushindani wakati wote. Pia kocha Kim
anakusudia kujenga kikosi bora cha miaka ijayo hivyo hakuna wasiwasi kuwa kati
ya mwaka 2015 au 2017 tanzania inaweza kabisa kushiriki michuano ya Kombe la
mataifa ya Afrika pamoja na kombe la dunia mwaka 2018 nchini Russia au 2022
nchini Qatar.
Nilipotafakari
programu hiyo upesi nikakumbuka namna kocha Marcio Maximo alivyoweza
kuishirikisha timu ya taifa ya vijana kwenye michuano ya kombe la taifa ambalo
linashirikisha mikoa yote ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Moja ya faida hizo ni
kumjengea uwezo mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulinwengu ambaye alishiriki
kikamilifu kwenye michuano hiyo.
Kwa wengine sasa
wanaona Thomas Ulimwengu amekuwa mshambuliaji hatari na hodari zaidi, lakini
njia alizopitia zimemjengea umakini na uhodari katika soka, ambako sasa anaweza
kupambana na washambuliaji hatari klabuni kwake kama Kaluyituka, Given
Singuluma, na wengineo.
Kwa mtazamo wangu
uamuzi wa kocha Kim kuliagiza shirikisho la soka nchini TFF kuhakikisha
Serengeti Boys inashiriki mechi za Ligi Kuu Tanzania bara kuna lengo moja tu
kuhakikisha anakuwa na kikosi imara zaidi cha timu ya taifa ya wakubwa(Taifa
Stars).
Ukiangalia rekodi za
kocha Kim na namna anavyoweza kujenga kikosi chake katika timu ya taifa, hakika
amekuwa kocha wa kipekee sana. nasema hivi sio kwasababu ya matokeo mazuri,
bali muundo wake wa utendaji kazi na namna anavyoweza kutufahamisha makosa yetu
kwa hekima.
Kim anajua kabisa
tulichokosa ni misingi ya soka la vijana kwahiyo anachofanya ni kuhakikisha
tunakuwa na hazina ya kutosha katika soka la vijana kupitia timu ya taifa. Wakati Kim akisema
hayo wenyewe tunafahamu kuwa tuna michuano miwili muhimu sana ambayo inawajenga
vijana lakini bado haionekani kuwa imara kiushindani. Mfano michuano ya Copa
cocacola na michuano ya Uhai.
Hii ni michuano
inayohusisha timu za vijana ambazo kwa namna moja ama nyingine zinapata faida,
lakini hakuna mwendelezo wake. Kwahiyo kocha Kim
amegundua moja ya sababu za kushindwa kuwa na mwendelezo ni gharama za
uendeshajiu, kwahiyo anaamua kupunguza gharama hizo kwa kuitumia timu ya taifa
ili iweze kusaidia kuzalisha wachezaji imara.
Pia anaikumbusha TFF
kuwa hakuna njia ya mkato kama inataka wachezaji wazuri zaidi ya kuwekeza
ikibidi shirikisho lenyewe kuwa na kituo chake. Kwa mantiki hiyo
badala ya kuwkusanya vijana huko mitaani na kuwapeleka uwanja wa Karume, kocha
Kim anatumia timu ya taifa kama mahali pevu ambapo pataleta hamasa kwa vijana
na kuongeza ujuzi wao kipindi wakirudi kwenye klabu zao.
Pili, hii itazisaidia
timu zetu kama Yanga na Simba ambazo mara nyingi zimekuwa zikisubiri wachezaji
walioko timu ya taifa ndio wawasajili. Namna gani kocha Kim
ataweza kuwaendeleza wachezaji watakaofanya vema kwenye kikosi cha Serengeti
Boys? Hilo litateguliwa kwa kumuongezea mkataba mpya ambao utamfanya ajikite
zaidi kutengeneza timu imara za timu za taifa akishirikiana na makocha wazawa.
Nimalize kwa kusema,
hakuna jambo baya kama tutaruhusu kuondoka kwa kocha Kim Poulsen wakati huu
ambapo ametuonyesha falsafa bora kabisa ya soka letu. Ni vyema TFF na serikali
zinaona umuhimu wa kuongeza mkataba mnono kwa kocha huyu. Muhimu tuache blah
blah katika hili.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako