October 21, 2017

MBUNGE WA CHEMBA AONDOA HOJA YA KUONGEZA MUDA WA UBUNGE

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MBUNGE  wa Chemba Juma Nkamia (CCM)amesema ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba unaohusu kuongeza ukomo wa Bunge. 
JUMA NKAMIA
Nkamia ambaye aliwasilisha kusudio hilo  katikati ya mwezi uliopita mjini Dodoma kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016,kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12  iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda wa bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza wa uongozi wa vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.

Kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp,alisema ameamua kuondoa kusudio hilo  baada ya mashauriano  na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

“Ndugu viongozi wenzangu naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na maelekezo  ya viongozi wa juu wa chama(CCM) na hali ya kisiasa  katika nchi kadhaa za Afrika  Mashariki  nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika bunge lijalo,”aliandika Nkamia.

Mbali na andiko hilo gazeti hili pia lilimtafuta Nkamia kupitia simu yake ya kiganjani ili kumuuliza kama  na sababu nyingine zaidi ya alizozitaja kupitia ujumbe  huo mfupi na lini atakuwa teyari kuwasilisha tena muswada huo alisema.

“Naomba ibaki hivyo hivyo kama ilivyo kwenye meseji  sina cha kuongeza,kuhusu ni lini nitapeleka tena nayo subiri kwa sababu nimesema nimesitisha kwa muda maana yake nitawasilisha tena nitakapokuwa teyari,”alisema Nkamia.

Hoja ya  Nkamia ambayo ilianzia  katika Bunge lililopita ilikuw aikipingwa na wanazuoni pamoja na wanasiasa wakongwe akiwemo Spika Mstaafu wa Bunge Pius Msekwa.

Msekwa ambaye alikuwa akiongea na televisheni ya Azam  mwishoni wa wiki hii alisema  chama cha CCM hakiwezi kukubaliana na maoni au mpango wa kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kikatiba kwa sasa.

Msekwa alisema kwa uzoefu wake bungeni tayari anaona kuna tafakari nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.

Alisema hoja hiyo inabidi iangaliwe kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli kuwa, iwapo kiongozi atakuwa mbaya, maisha yanaweza kuwa ya mateso kupitia kiongozi huyo na kuongeza kuwa hilo hata Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliliona hilo.

“Ni kwamba miaka kumi tu inatosha, ili kama mtu ni mbaya tuvumilie kwa hiyo miaka kumi, na siyo kwamba haikufikiriwa. .na sidhani kama CCM itakuwa na nafasi ya kujadili hilo kwa sasa” alisema Msekwa. Mbali na Msekwa wasomi wakiwemo Dk.Benson Bana nao walimpinga huku akisema kuwa lengo lake lilikuwa ni kujipendekeza kwa Rais Dk. John Magufuli ili ampe uwaziri.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako