NA HONORIUS MPANGALA
KITAALUMA na hisia zangu
zimenifanya niwe mtu tofauti kabisa kuhusiana na matumizi ya baadhi ya maneno
hapa nchini. Mengi hutumiwa na viongozi wa ngazi za juu kuwaona wale waliopo
chini au wasio na vyeo kama wao kuwa
wenye kiwango fulani cha dhiki kinachostahili kuitwa cha chini. Ni hapo
ndipo nakuwa na hisia tofauti sana juu ya kutumia maneno fulani dhidi ya kundi
jingine hasa lile ninaloongoza au viongozi wanaloliongoza.
Japokuwa nimekuwa mtu nisiyependezwa
na na hili neno “Wananchi wa hali ya chini”' lakini najiuliza hao wa hali ya
juu ni akina nani, wanafanya nini kutokuwa na hali ya chini na njia zao zikoje
ili tuwaambie wa hali ya chini wajifunze kwenda huko juu?
Suala elimu katika nchi yoyote
ni muhimu na linatakiwa kupewa kipaumbele sana. Kiuhalisia mazingira ya
wanafunzi kwa shule nyingi zinazomilikiwa na serikali zimekuwa na changamoto
kubwa na kupelekea hata matokeo mabaya kwa shule hizo. Lakini unakuta baada ya kutazama
wapi walipojikwaa wao wanakawaida ya kulaumu mwendo Wa aliyedondoka kuwa
hatazami vyema au hatembei vyema.
Tangu iliposemwa elimu bure maisha
ya wanafunzi yamekuwa na changamoto zake na wazazi waliipokea katika mitazamo
yao hii hoja. Kutokana na kuzoea kupewa pewa tangu zama za wakaloni, waafrika
wengi wamekuwa wavivu wa kujitafutia wao na kutatua changamoto wao huku
wakitegemea tusaidiwa kama ilivyokuwa katika maisha ya ukoloni au kwa wale
waliokuwa wanaishi karibu na Taasisi za kidini zilivyokuwa zikitoa misaada.
Maisha yamebadilika wananchi
kama wangetambua kuwa maendeleo ya kila mahali yanategemea nguvu zao
wakisaidiwa na serikali na wakaishi hivyo basi changamoto nyingi zingetatuliwa
na wao wenyewe.
Baada ya tamko la elimu bure
wazazi nao wameacha kila kitu ,unakuta mzazi anashindwa hata kumrekebishia
mwanae sare ikiyochanika au kufumuka akielekezwa anajibu elimu bure. Wako wanaofikiria
elimu bure hata vitendea kazi vya mwanafunzi navyo hutoka kwa serikali.
Kwa upande wa serikali nao
wanawajibika katika kuhakikisha kuwa watendaji wao wanafanya kazi ya kutatua
changamoto, zinazojitokeza katika taasisi zao. Kata ina diwani lakini diwani
hana hata idadi ya upungufu wa watumishi anaohitaji kuwa nao katika kata yake.
Sasa unajiuliza huu uwakilishi wake uko kwa namna ipi.
Shule hazina madawati,
wanafunzi wanakaa chini tena sekondari kitu ambacho kinashangaza sana. Zamani
ilikuwa wanafunzi wanaripoti na dawati na ilisaidia wanafunzi wote kukaa kwenye
madawati, leo hii wanakaa chini ajabu sana.
Hii elimu bure wananchi wanatakiwa
kuitathimini wenyewe vyema. Miaka ya nyuma tulikuwa tunaona wananchi
wakijitolea kufyatua tofali na kujenga nyumba za watumishi lakini leo hakuna
mwananchi anayetaka kushiriki katika shughuli za kimaendeleo katika jamii
husika.
Tusingeona upungufu wa madarasa,
nyumba za waganga, walimu na hata nyumba za watendaji wa vijiji kama serikali
ingekuwa iko wazi kwa wananchi juu ya miradi ya maendeleo. Tatizo kila jambo
hulifanya kwa kuegemea katika masuaka ya kisiasa na kuacha uhalisia wa
kiutendaji ndiyo maana wananchi hawana muda wa kushiriki katika miradi ya
serikali kwa kujitolea badala yake hushiriki inapokuwa kwa malipo peke yake.
Tujitafakari kama hii nchi
inajengwa na wananchi au kila mwananchi anajenga familia yake. Na kuiacha nchi
ikijengwa na serikali? Tukitafakari kwa undani unagundua hili ni tatizo la
kutojiweka wazi kwa wananchi juu ya mipango wanayoifanya kwani inakuwa a chembe
ya kisiasa.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako