February 03, 2018

JOHN LANGALIBALELE DUBE: MWANAFUNZI ALIYEAMINIKA KUWA NA TABIA CHAFU CHUONI MWASISI WA CHAMA CHA ANC, AFRIKA KUSINI.

Na Kizito Mpangala

John Langalibalele Dube alizaliwa mwaka 1871 kwa wazazi James Dube na Elizabeti Dube katika kitongoji cha Inanda,kwa sasa ni mkoa wa KwaZulu Natal. Jina lake la katikati yaani Langalibalele alipewa na wazazi wake likimaanisha “mwanga wa jua”. Baba yake alikuwa mchungaji katika kanisa la misheni ya Waamerika walioishi katika jamii ya Wazulu.
John Langalibalele Dube

Baba yake alikuwa kiongozi wa kabila la watu wa Qadi katika jamii ya Wazulu na jina lake lilikuwa Ngcobo Dube. Baada ya ujio wa Wamisionri alimua kujiunga na Ukristo na kisha akabatizwa kwa jina la JAMES DUBE. Huo ndio ulikuwa mwisho wa kuliongoza kabila hilo. John Langalibalele Dube alikuwa Mwalimu, Mhariri, Mpigachapa, Mshairi, Mwanafalsafa, Mwandishi wa Insha, na mwanasiasa nchini Afrika Kusini. 
 
John Langalibalele Dube alianza masomo katika kitongoji cha Inanda, na baadae akajiunga na chuo cha Adams (Adams College) kitongoji cha Amazimtoti kusini mwa mji wa Durban nchini Afrika Kusini. Akiwa chuoni hapo, walimu walipeleka lalamiko kwa wazazi wa John kwamba kijana wao ana tabia chafu chuoni hapo ambayo haiendani na sheria za chuo. Ndipo Mchungaji William Cullen Wilcox alipoteuliwa kuzungumza na kumkanya John Langalibalele Dube kwa tabia zake chafu (haikuwewa wazi ni tabia zipi hasa alizokuwa akizifanya). John alifuata nasaha alizopewa na kisha akabadili tabia.

Wamisionari wa Amerika walioondoka katika kitongoji cha Inanda, John aliambatana nao na kujiunga na chuo cha Oberline nchini Marekani. Aliambatana nao kwenda Marekani baada ya kupata ruhusa kutoka kwa baba yake Mzee James Dube ambaye alikuwa mchungaji na kiongozi katika chuo cha Adams. Wamisionari hao walikubali kwa sharti kwamba hawatamhudumia chochote kifedha, hivyo Mzee James Dube alipaswa kuingia mwnyewe mifukoni mwake.

Akiwa chuoni Oberlin, John Langalibalele Dube alijifunza upigaji chapa, alkini hakutunukiwa shahada yoyote chuoni hapo. Baada ya masomo yake alirudi nchini Afrika Kusini na kuanzisha gazeti yeye pamoja na mke wake Nokutela Mdima Dube. Gazeti hilo liliitwa Ilanga lase Natali (Jua la Natal) mwka 1903.
Kwa Waafrika waliopata elimu ya magharibi wakati ule, kulikuwa na “ugomvi nafsia” kati ya utamaduni wa kimagharibi na utamaduni wa kikabila katika makabila yao husika. Lakini John L. Dube alijitahidi kubaki katika imani ya Wazulu na walimuamini licha ya kuwa msomi wa elimu ya magharibi iliyokuwa ikikataliwa na viongozi wengi wa makabila. 

John Langalibalele Dube alianzisha chama cha kisiasa kilichoitwa South African Native National Congress (SANNC) mjini Bloemfontein ambapo alikuwa Rais wa chama hicho kuanzia mwaka 1912 hadi mwaka 1917. Miaka 6 baadae yaani mwaka 1923 chama hicho kikiwa na misingi ile ile, kilibadilishwa jina na kuitwa African National Congress (ANC) ambacho kipo mpaka sasa nchini Afrika Kusini. Alifundisha wafuasi wake umuhimu w umoja katika chama hicho na kilijiongezea nguvu baada ya kuanzishwa kwa Umoja wa Vijana wa chama hicho yaani ANC Youth League miaka ya 1940. Akiwa kama kiongozi wa maandamano ya kisiasa ya watu weusi, hotuba zake hazikuchapishwa na hazipatikani.
John L. Dube (katikati) akiwa na washirika wake wa SANNC kisha ANC


John L. Dube alisisitiza umoja kwa watu weusi kwa siku nyingi kabla ya ujio wa Marcus Mosiah Carvey Jr aliyekuwa mwandishi wa habari na mpiga chapa kutoka Jamaica ambaye alikuwa kiongozi wa maandamano yaliyoitwa Pan-Africanism, pia alianzisha utaratibu maaluamu ulioitwa Black Star Line mwaka 1914, uliokuwa na madhumuni ya kusaidia wananchi 
weusi wa Afrika kusini waliokuwa wanaishi ugaenini (Diaspora) kurudi nchini kwao ili kuitetea ardhi yao. Lakini kwa bahati mbaya Black Star Line ulifirisika na hivyo Marcus Mosiah Carvey alipelekwa gerezani na serikali ya Makaburu, ndipo ulpokuwa mwisho wa mpango huo.

Hakuisahau kazi yake ya kufundisha. Yeye pamoja na mke wake Nokutela Mdima Dube walianzisha shule nchi Afrika Kusini wakati huo. Shule hiyo kwa sasa inaitwa Ohlange High School katika mji wa Ohlange karibu na kitongoji cha Phoenix na EkuPhakameni. Hii ilikuwa shule ya kwanza kuanzishwa na walimu weusi nchi Afrika Kusini. John Langalibalele Dube alifundisha kwa bidii na baadae akatunukiwa shahada ya juu ya udakitari wa falsafa (Ph.D) kama zawadi kwa kazi yake ya kuelimisha jamii. Jambo lililishawishi zaidi kupata sifa hiyo ni kutoka katika kitabu chake kilichoitwa UMUNTU ISITA SAKE UQOBO LWAKE (Adui Mkubwa wa Mtu ni Yeye Mwenyewe)
Solomon Plaatje mshirika wa John L. Dube

John L. Dube alipendekeza elimu ya Afrika Kusini itolewe kwa mchanganyiko wa elimu ya magahribi na elimu ya kikabila kwa kulingana na utaratibu wa kabila husika lakini iwe na dhumuni moja kwa ajili wa wananchi wote. Nadharia zake kuhusu elimu zinapatikana katika vitabu vyake viwili ammabvyo vinaitwa UKUZIPHATHA na ISITA. Pia, ndiye mwasisi wa fasihi ya Wazulu (Zulu Literature) ambapo alikuwa mmoja kati ya waandishi wa Kizulu. Kitabu cha kwanza kuandikwa kwa lugha ya Kizulu kiliitwa ABANTU ABAMNYAMA LAPO BAVELA NGAKONA (Watu Weusi na Mahali Walikotoka) ambacho kiliandikwa miaka ya 1890 na mwandishi Magema Fuze na kilichapishwa mwaka 1922.

John Langalibalelel Dube pia, aliandika riwaya iliyoitwa INSILA kaSHAKA (Mtumishi wa Shaka) mwaka 1930. Pia, aliandika tawasifu ya mfalame Dinizulu na kuwa mwandishi wa kwanza wa tawasifu miongoni mwa jamii ya watu weusi. 

Johh L. Dube na mkewe wanapewa heshima kwa kusaidiana mwalimu mwenzao Enoch Sontonga kutunga wimbo ambao walikuwa wakiuimba katika shughuli zao za chama na pia kuwa wimbo wa shule yao. Wimbo huo ulianza
Mwalimu Enoch Sontonga
kutumika na chama cha ANC mwaka
1925 kama wimbo wa chama. Ni wimbo ambao ni ubeti wa kwanza wa wimbo wa taifa wa Tanzania. Uliimbwa Kizulu, lakini kwa Tanzania ulitafsiriwa kwa Kiswahili.

John L. Dube na mkewe Nokutela hawakupata mtoto lakini John alimpa mimba mwanafunzi wake katika shule yao na kupata mtoto, jambo hili lilifanyiwa uchunguzi na John hakuchukuliwa hatua za kisheria lakini mkewe Nokutela alichukia kitendo hiki na akaamua kuachana na mumewe huyo mwaka 1914 kisha akhamia mkoani Transvaal mapaka alipoanza kuugua homa ya ini na kuamua kurudi tena jijini Johannesburg kuishi tena na mumewe, mwaka 1917. Na arifariki mwaka huo huo. Naye John L. Dube alifariki mwaka 1946. Ndiye kiongozi mwasisi wa chama cha ANC.


© Kizito Mpangala (0692 555 874)

No comments:

Post a Comment

Maoni yako