Kwa hakika kimaisha, litatufikisha mbali,
Hivyo kulifnaikisha, yatupasa kukubali,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
2. Ni muda mrefu sasa, tangu rai zitolewe,
Bado lugah imekosa, kutufundisha yenyewe,
A’dha hakuna hamasa, za kutosha tuamue,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
3. Ingawa vinohusika, vyombo huleta mkazo,
Kungali kunaoneka, kuna bado pingamizo,
Ama yanayotendeka, wapo huyapa kikwazo,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
4. Kumfunza mswahili, kwa lugha yake mwenyewe,
Kwa masomo mbalimbali, hufanya mengi ajuwe,
Kukuza zake akili, pasi cha lugha kiwewe,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
5. Tumeona mashuleni, rai za wengi walimu,
Zinasema lugha ngeni, zaonekana ni ngumu,
Zitunzwapo masomoni, hukanganya kielimu,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
6. Kwa mfano Kiingereza, hakieleweki vema,
Kingali chawatatiza, wanafunzi wakisoma,
Sababu inatokeza, hakina msingi mwema,
Kufundisha Kishwahili, masomo kutekelezwe.
7.
Pamoja na kukubali, ni lugha ya biashara,
Iliyo na sifa kali, UNO mapaka Sahara,
Bado kwetu Kiswahili, twatumia hadi bara,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
8. Hivi sasa Kiswahili, chatumika duniani,
Karibu kila mahali, kinafundishwa vyuoni,
Chaonekana ni mali, hata huko Uzunguni,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
9. Hapa kwetu Tanzania, ni lugha ya Ki-taifa,
Tulishajitangazia, tulipopata wadhifa,
Ndiyo ma’na twatumia, mpaka kwenye tarafa,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
10.
Pampoja na yote haya, si busara kudunisha,
Tunapoyonea haya, ni nyuma
twairudisha,
Huko ni kuwayawaya, pasipo
kutajirisha,
Kufundisha Kiswahili, masomo
kutekelezwe.
11. Tutakubali wasomi, tuko tumegawanyika,
Wengine tunakihami, Kiswahili
kwa dhihaka,
Na wengine kama mimi, tunakipa
madaraka,
Kufundisha Kiswahili, masomo
kutekelezwe.
12. Tupo sisi tulosoma, zamani kwa Kingereza,
Jinsi kilivyotuzama, ukweli twakitukuza,
Ndipo Kiswahili mama, wengine twakipuuza,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
13.
Na tupo pia wa sasa, wenye zetu taaluma,
Sisi twapania hasa, Kiswahili kukizima,
Twakiona kimekosa, ile sifa ya kusoma,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
14.
Sawa! na tuone hivyo, tuangalie lakini,
Japo twakiona sivyo, watu wanakithamini,
Na hivi sasa kilivyo, chatumiwa Marekani,
Kufundisha kiswahili, masomo kutekelezwe.
15.
Yafaa ieleweke, Kiswahili ni cha umma,
Na pia ikubalike, ‘hata kama tumesoma’,
Vizuri tueleweke, lugha hii ndiyo njema,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
16. Ni vipi tumkabili, mwananchi kijijini,
Kama wasomi wa kweli, tuna taaluma ngeni,
Jee, huyo mswahili, tutachomfunza nini?
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
17.
Tunakubali kusema, upo ugumu kuanza
Lakini tutatazama, jinsi gani ya kufanya,
Tukielewa lazima, wasomi wetu kufunza,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
18. Wenzetu Waingereza, walifanya sisi kama,
Mapaka wakaeneza, lugha watu wakasoma,
Kila nyanja waliweza, zitumie taaluma,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
19.
Kama huko walitoka, kwa nini sisi tushindwe,
Ikiwa zafahamika, sababu lugha
iundwe,
Basi nasi tutafika, tunapotaka
ipandwe,
Kufundisha Kiswahili, masomo
kutelezwe.
20. Si kweli kwamba sarufi, yetu haitoshelezi,
Wala kusema herufi, za Kiswahili si wazi,
Ukweli tunayo safi, isimu kimatumizi,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
21. Kwamba mimi naamini, kuwa pamoja ni dawa,
Yatubidi kwa imani, tuafikiane sawa,
Tukiwa na madhumuni, ya Kiswahili kukua,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
22.
Kweli zetu jitihada, nyingi tumeshazitenda,
Kweli pia ipo shida, kwa wengineo kupenda,
Hivyo na tutoe ada, swala hili kulishinda,
Kufundisha Kiswahili, masomo kutekelezwe.
© Charles Mloka (31/12/1982)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako