February 02, 2018

MFUMO WA UFUNDISHAJI NCHINI UNATAKIWA KUBADILISHWA

NA KIZITO MPANGALA
KILA mara inapofanyika mitihani kidato cha pili, nne na sita matokeo yanapokuwa mabaya wanaolaumiwa ni walimu. Matokeo yakiwa mazuri wanapongezwa walimu. 

Tunakumbuka matokeo ya kidato cha nne yamewahi kubatilishwa wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya nne. Ilibidi NECTA wafanye usahihishaji upya ili kuja na matokeo mazuri kutokana na awali kuwa mabaya kwa nchi nzima.
Mwenendo mzima wa sekta ya elimu mara nyingi Walimu wamebebe lawama nyingi. Lakini ipo haja ya watendaji wakuu (yaani serikali yetu) kubadilisha mfumo wa ufundishaji unaotumiwa hapa nchini. 

Nasema hivi baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa ili mtu awe amebobea kwenye ufundishaji lazima awe na uwezo mkubwa katika somo fulani. Kwahiyo naongelea namna ya kuwabadilisha watu ili kuleta manufaa ya elimu, uwezo wao na kuwasaidia wanafunzi.

Ingefaa kila mwalimu hapa nchini awe anafundisha somo moja tu na kwa madarasa mawili tu kwa siku nzima. Somo hilo moja ndilo liwe hilo tu hadi atakapostaafu. Mbinu hii itasaidia ubobezi mzuri wa somo husika kwa walimu wetu.

Isiwe mwalimu wa Historia alazimike kufundisha tena somo la Uraia. Mwalimu wa Biolojia alazimike tena kufundisha somo la Kemia. Mwalimu wa Hisabati alazimike tena kufundisha somo la Fizikia. Mwalimu wa Kiswahili alazimike tena kufundisha somo la Kiingereza kwa kuwa tu eti anajua sana kuidadavua fasihi. Mwalimu wa biashara(Commerce) n alazimike tena kufundisha uhasibu (Accounts) ingawaje masomo haya yanashabihiana kwa namna fulani.

Kwa hiyo, ingelikuwa namna hii, mwalimu mmoja somo moja analolimudu kwa umaridadi, kwa madaha, kwa maringo kwamba anaweza kumkoga mwanafunzi na kumvuta atamani kujua zaidi, hakika wabobezi wangepatikana wengi mno tena si wa kubahatisha.

Vilevile ufundishaji ungekuwa wa kulifikiria darasa lote ila si tu kuwafikiria wale wanaofanya vizuri zaidi eti kwamba wataing'arisha shule katika matokeo ya kitaifa wakati wasioelewa ni wengi. 

Na pia wanafunzi wasiwe wanafundishwa kwa imani ya kwamba, kwa mfano: eti someni "Bernoulli’s Principle" mwaka huu itatoka kwenye mtihani, au kusema "jifunzeni sana misombo ya kikemikali yote ya benzini itatoka mwaka huu kwenye mtihani".

Au kusema "someni tu kitabu cha Takadini maana ndicho maarufu sana mtafaulu", au kusema "someni michoro yote ya maumbo yatokanayo na mvumo wa upepo, someni 'yardangs' kwa kina itatoka kwenye mtihani" na kadhalika.

Hapa tunakaririshana. Mwalimu mmoja alikuwa akitufundisha halafu katika mazungumzo ya kawaida alikuwa akituambia "Kama unakariri utakufa". Kauli yake iliongeza morali ya kuchanganua mambo na kuelewa somo kwa ufasaha.
Ninarudia kwamba ingefaa ngefaa sana kila mwalimu mmoja afundishe somo moja tu na kwa madarasa mawili tu kwa siku. Madarasa hayo mawili afundishe somo lilelile kulingana na usawa (levo) wa wanafunzi wa darasa husika.

Pia ufundishaji sasa uzingatie matumizi (application) au umuhimu wa somo husika katika maisha yetu ya kila siku. Hapo ikisemwa kuwa walimu hawatoshi basi muhusika ndio achakarike kuongeza walimu. Haitakiwi kama ilivyo sasa, katika shule moja mwalimu wa fizikia ni mmoja tu madarasa yote na pia anategemewa kwenye hisabati madarasa yote. Huo ni ufundishaji mbaya. 

0692 555874

No comments:

Post a Comment

Maoni yako