February 02, 2018

UCHAMBUZI WA KITABU: DIWANI YA SIWACHI KUSEMA

MWANDISHI: MOHAMMED K. GHASSANI
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA
NA MARKUS MPANGALA

MWAKA 2017 nilipatiwa zawadi ya vitabu vitano vya ushairi kutoka kwa mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), Mohammed Khelef Ghassani. Vitabu hivyo ni Siwachi Kusema, Machozi Yamenishiya, Kalamu ya Mapinduzi na Adamo. Leo tunachambua diwani ya  “Siwachi Kusema; Uhuru U kifungoni” ambayo imechapishwa mwaka 2016 na kampuni ya Zanzibar Daima Publishing yenye makao yake mjini Bonn nchini Ujerumani. Diwani hii imepewa nambari ISBN 978-15-34660-16-8.


‘Siwachi kusema’ ni mwendelezo namna ya mwandishi huyo ya kusema na kuyasemea yale yanayotokea mbele katika jamii yake. mambo ambayo yanaikwaza jamii hiyo kutokana na sababu mbalimbali. 

Mathalani katika dibaji ya diwani hii mwandishi anasema, “Mwanadamu anayelazimishwa kwasababu yoyote ile kuacha kutoa kauli yake juu ya yale yanayojiri mbele ya macho yake, yale yanayomuhusu na kuyaathiri maisha yake, bsi huyo ni mithili ya mtu aliyezibwa pumzi kwa matambara au mateka aliyetiwa jiti la roho. Huwa si mtu huru, si mtu kamili, si mtu mtu,”(Uk.Xi).

Mkusanyiko wa mashairi uliopo katika diwani hii umegawanyika katika maeneo tofauti. Kuanzia mapenzi na ndoa,ukiwa au upweke wa baadhi ya watu hapa duniani, siasa na haki za binadamu, masuala ya dini, misaada kadhalika.
Tunaweza kutazama mifano hayo katika baadhi ya mashairi. 

Shairi la ‘Mwanangu Nakupe Mke’ (Uk.14) mwandishi anaandika,
“Mwanangu nakupa mke, nakuwekea kikao,

Awe wako uwe wake,wamoja toke oleo,

Basi maneno yashike, na wasia nikupao,

Mkeo awe ni nuru.


Hapa tunaona mfano hai wa mapenzi na ndoa ambapo wazazi hutoa wosia kwa vijana wao mara waingiapo katika ndoa. Mwandishi anajenga taswira ya kuondoa migogoro ndani ya ndoa mpya na change ambayo kila mmoja anatakiwa kulinda. Kuona hivyo mzazi anaamua kutoa wosia ili kijana wake aweze kuhimili na kuepuka migogoro ya aina yoyote. 

Mwandishi anaendelea
“Mwanangu nakupa mke, awe ni mke mkeo,

Umtake akutake, ndoa ni watakanao,

Mufurahi na mucheke, mfano wafurahio

Rabbi Nshallah!

“Mwanangu nakupa mke, awe kwako kifungiyo,

Jicho ‘sikuruke, moyo ‘sikwenende mbiyo

Epuka ‘siadhirike, mwana tunza heshimayo,

Mwana ‘sinitukanishe.

Kama ilivyoada mwandishi wa diwani hii hakuacha nyuma kabisa kuwakumbuka watu wote wanaofikwa na matatizo ya kuondokewa na wapendwa wao, wapenzi wao, wake zao,ndugu zao na kadhalika. Misingi yake imejengwa katika namna mbili; mosi wale wanaochwa kimapenzi na wale wanaofiwa na ndugu au wazazi wao. 

Mwandishi ametumia shairi la “Mapenzi Hayana Pima”(Uk.24) na “Naitwa Mwana Ghassani”(Uk.28).
“Alisema akulishe, robo wakia ya pendo,

Kiasi akudodeshe, ‘sitamukiwe uhondo,

Kisha huyo afungashe, kilo zake kwenye mwendo,

Tahamaki kwa marundo, amekupa urandishe, (Uk.24).

Aidha, katika shairi la ‘naiwa Mwana Ghassani kuelezea masikitiko ya kufiwa kwa mzazi wake yeye na pamoja na mwandishi wa kitabu cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni’ Harith Ghassani. Mshairi anafunguka na kuelezea masikitiko ya ukiwa au upweke waliokuwanao watoto baada ya kutokwa na mzazi. 

Mwandishi anaandika yafuatayo;
“Ndimi mwanao hakika, Muhamadi wa Ghassani,

Ndimi naliyeandika, uloona risalani,

Na Harithi wangu kaka,mmoja wetu ubini,

Na Baba yetu Ghassani, ni kweli ametutoka.

“Ghassani alotutoka, kwangu mimi kama ami,

Zama walizoondoka,wavyele wetu Yamani

‘Kasogea Afirika,pande hizino za pwani

Waligawana watwani, na gele wakageleka (uk.28).

Suala la haki za binadamu ni miongoni mwa masuala muhimu yaliyomo katika diwani hii. Ghassani anatukumbusha masuala ya siasa, haki za binadamu pamoja na matendo ya viongozi yanavyioweza kuwa chachu ya mema au mabaya. Mwandishi ametumia shairi la “Kwa Jina la Katiba” (uk.54).

Kwa jina la Katiba,hukusanyana raia

Kwa misururu mirefu, safu za kutanda njia,

Hupaza sauti zao,kwa hasira wakalia

Nao hupigwa mayowe,kwakutumia katiba.

Kwa kuienzi Katiba, leo tuna mayatima

Kwa kufuata katiba, jela nafasi hazina,

Watu hutunga katiba,thumna ikawa nakama,

Na dhalimu hudhulumu,kwasababu ya katiba.

Na ‘Dola’ huwekwa mbele,nyuma ukawapo umma,

Haki umma ulonayo,ni hadi dola kusema

Ndiko kukituma kitu,kisha nacho ‘kakutuma

Kwamba huvunjwa katiba ili palindwe katiba (Uk.54)
Kwenye suala la imani au dini mwandishi hakumsahau mola wake. Ametumia shairi la “Sina Ahadi na Mungu,”Uk.50 kuikumbusha jamii yake umuhimu wa ibada, kumcha Mungu pamoja na kuwa waungwana.
Sijaagana na Mungu,kwamba atanibakisha,

Nitimize lengo langu,pumzi zisijanisha

‘Kitimu dhamira yangu,bado ninayo maisha

Hilo ni la Mola wangu,siwezi jiaminisha.

MWISHO

No comments:

Post a Comment

Maoni yako