January 21, 2018

ERATOSTHENES WA KIRENE: MWANAHISABATI ALIYEISHI AFRIKA NA KUKADIRIA MZINGO WA DUNIA KWA KIVULI CHA MWANZI.

Na Kizito Mpangala

Eratosthenes alizaliwa mwaka 276 KK (Kabla ya kuazaliwa Yesu Kristo) mjini Kirene, Libya ya sasa. Kirene ni mji mashuhuri ulioundwa na Wagiriki wa kale walioishi Afrika ya Kaskazini hasa Libya ambako ndiko ulikokuwa mji wa Kirene maeneo ya Tripolitania ( sasa ni Tripoli), na Misri maeneo ya Alexandria ilikokuwa maktaba mashuhuri iliyotumiwa na wataalamu wengi wa Ugiriki ya kale. 

Alikuwa akifanya mazoezi mbalimbali ya viungo kila siku asubuhi na jioni. Alijifunza kusoma, kuandika, na kuhesabu. Ni kama vile falsafa ya elimu ya msingi inayotumiwa nchini Tanzania yaani KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu). Pia, alijifunza uandishi wa mashairi na vilevile masuala ya muziki.
Baadae alienda mjini Athens nchini Ugiriki kwa ajili ya kisomo. Alifundishwa falsafa ya maadili kulingana na matakwa ya jamii ya Wahelleni ambayo ni mchanganyiko wa tamaduni za Wagiriki na Warumi, kwa ujumla huitwa Utamaduni wa kihelleni (Hellenistic Culture). Falsafa hiyo ya maadili (Hellenistic Philosophy) iliitwa Stoicism kama ilivyoasisiwa na mwanafalsafa Zeno wa Ugiriki.

Ni falsafa ambayo iko tofauti na zile za Wagriki wengine kama akina Socrates, Plato, Aristotle na kadhalika, ambayo iliegemea zaidi katika upande wa kile kilichosemwa na mwanafalsafa husika. Lakini falsafa ya maadili kadiri ya matakwa ya Wahelleni ilijali kile alichokitenda mtu na siyo alichokisema.

Eratosthenes alikuwa mtaalamu wa hisabati, lugha, historia, jiografia,  mshairi, mnajimu na mtaalamu wa muziki. Daima alikuwa mtu wa kujifunza. Alikuwa mkurugenzi mkuu wa maktaba mashuhuri ya Alexandria nchini Misri. Maktaba hiyo vitabu vyake vyote vilikuwa vikiandikwa kwa mkono, hiyo ilitokana na kutokuwepo kwa teknolojia bora ya kuchapisha vitabu kama ilivyo sasa.  

Alijifunza pia falsafa za mwanafalsafa mashuhuri Plato na kuzipenda falsafa za Plato. Mwalimu wake mkuu wa falsafa alikuwa ni Zeno na mwalimu wake mwingine wa falsafa pia alikuwa ni Aristo wa Chios. Baada ya kuzipenda falsafa za Plato na kuzifuatilia kwa kina, Eratosthenes aliandika kazi yake ya kwanza akiwa mwanafunzi. Kazi hiyo aliiita Platonikos, ambapo aliandika misingi ya hisabati kulingana na falsafa za kihisabati za Plato.

Eratosthenes alipenda kujishughulisha na mambo mbalimbali kitaaluma na hivyo kumfanya awe na kichwa chepesi katika kufikiri zaidi. Alichunguza na kufuatilia sanaa ya ushairi akiwa na mwalimu wake wa ushairi, Kallimakhosi ambaye alikuwa mwananchi wa Libya ya kale akiwa na asili ya Ugiriki.

Eratosthenes aliandika mashairi mbalimbali hasa kuhusu historia ya miungu ya kale ya Ugiriki ambapo shairi liliitwa Hermes. Shairi lilingine lilihusu binti wa Athen aliyejinyonga, lilitwa Erigone.  Pia, aiandika kazi yake ya pili iliyofikiriwa kuwa ni ya kisayansi ambayo ilihusu umuhimu na mwanzo wa vita vya Trojan. Vita vya Trojan ni vita vilivyotokana na tamaduni za Wagiriki (Greek Mythology). Pia aliandika kazi ya tatu mbayo haikujulikana muda alioandika lakini alisifiwa sana kutokana na kiwango chake cha uandishi. Kazi hiyo aliiita Olympic Victors.

Uwezo wa kuandika ulimfanya atambulike zaidi na hivyo Pharao Ptolemy III Euergetes aliamua kumuomba awe mkurugenzi mkuu wa maktaba ya Alexandria waka 254. Maktaba ya Alexandria ni moja kati ya maktaba za kale zinazoheshimika sana duniani. Kwa sasa maktaba hiyo ni maktaba kuu ya taifa nchini Misri, ni maktaba iliyoanzishwa mnamo karne ya tatu kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo. Eratosthenes alikubali wadhifa huo wa kuwa mkurugenzi mkuu wa maktabani hapo.

Baada ya kupewa wadhifa huo ambao alimpokea mkurugenzi wa awali na mshairi, Apollonius Rhodius, Eratosthenes aliwekwa kuwa mwalimu wa watoto wa Pharoa Ptolemy ambapo mmoja kati yao akamrithi baba yake uongozi na kuwa Pharao wa IV yaani Pharao IV Philopator.

Akiwa kiongozi wa maktaba hiyo, Eratosthenes alitangaza kuwa vitabu vyote vinapaswa kuwekewa alama maalumu ili kutambua kitabu halisi na kilichotolewa nakala tu. Ndipo utaratibu wa namba za kimataifa za vitabu ulipoanzishwa. Namba hizo kwa sasa hujulikana kama ISBN ambapo ni kifupi cha “International Serial Book Number”. Aliamua kufanya hivyo kutokana na kuzagaa kwa vitabu mitaani ambavyo vilikuwa vimenakiliwa kwa usahihi kama kitabu halisi husika ambapo ilikuwa ni vigumu kutambua kipi ni halisi na kipi ni nakala ya ujanja.

Eratosthenes alijidhatiti kutunza heshima ya maktaba ya Alexandria iliyokuwa na wasomaji wengi kuliko maktaba ya Pergamom ya Uturuki. Maktaba ya Pergamom ni maaktaba kongwe nchini Uturuki ambapo kwa sasa ni maktaba ya taifa la Uturuki.

Eratosthenes alikusanya vitabu vyote vya michezo ya kuigiza (tamthiliya/dramma) vilivyoandikwa na waandishi wa kale kama vile Sophocles, Aesychylus, Euripides na wengineo, akavihifadhi katika maktaba hiyo ili kutunza kazi za waandishi hao.

Licha ya kuwa na roho hai katika masuala ya vitabu na falsafa, Eratosthenes alikuwa mwanahisabti mashuhuri na kuwa na mchango katika uga wa hisabati kwa ujumla. Alijifunza pia sayansi na kujenga urafiki baina yake na mwanahisabati na mwanasayansi mashuhuri duniani kote, Archimedes.

Tufe la armillari (Armillary sphere)
Mnamo mwaka 253 Eratosthenes aliunda tufe maalumu kwa ajili ya kujifunza nadharia mbalimbali kuhusu mfumo wa jua na sayari zake. Tufe hilo linafahamika kama “Tufe la armillari” (Armillary Sphere). Tufe hili liliongezewa tafakuri zaidi na kupata mgawanyiko wa muda kwa namna mbili ambazo zinatumika sasa. Namna hizo mbili za muda ya mtindo wa masaa 12 na ya mtindo wa masaa 24 kulingana na mistari husika ya longitudo na latitudo.

Eratosthenes aliushangaza ulimwengu katika kitabu chake kilichohusu mwendo-mduara wa magimba yaliyoko angani. Kitabu hich kiliitwa “On the Circular Motions of the Celestial Bodies” ambacho aliushangaza ulimwengu wa kale na wa kisasa ni kukokotoa na kutoa makadirio ya mzingo wa dunia kwa kutumia kivuli cha mwanzi. Aliweza kufanya hivyo kwa kutumia maarifa ya hisabati katika mada kuu ya Trigonometria kwenye mada ndogo ya Pembe mwinuko (Angle of elevation) ya jua nyakati za mchana kipindi cha kiangazi akiwa katika kisiwa cha Syene, kwa sasa ni mji wa Aswan nchini Misri. Eratosthenes aliamini kwamba, katika kila taifa mazuri na mabaya.

 Kielelezo kikionyesha jinsi mzingo wa dunia
ulivyopimwa na Eratosthenes.
Alikokotoa mzingo huo wa dunia akiwa nchini Misri. Alifanya hivyo kwa kutumia mwanzi mrefu  na kupima pembe mwinuko ya jua kutokana na kivuli cha mwanzi huo na kupata 70. Pia, aliweza kupima ukubwa wa nchi ya Misri, jambo ambalo liligundulika baada ya tafiti mbalimbali za kazi zake. Mzingo wa dunia aliopima ulikuwa ni kilometa 44,100. Miaka 200 baadae, wataalamu wa anga nchini Italia walifanya vipimo vyao na kupata jawabu lililozidi kidogo lile la Eratosthenes, majawabu hayo yalitofautioana kwa kilometa 2,000 tu ambapo wengi walisema kuwa Eratosthenes alimtuma mtu atembee kuanzia nchini Misri azunguke dunia yote na kuishia tena alipoanzia safari hiyo!

Miaka 117 baada ya kifo cha Eratosthenes, Christopher Columbus alisoma kazi za Eratosthenes kuhusu ukubwa wa dunia na akaziamini kulingana na ramani zilizochorwa na Toscanelli. Christopher Columbus aliamini kwamba mzingo wa dunia uliokokotolewa na Eratosthenes ulikuwa sahihi na akatoa uamuzi kwamba sehemu aliyofika alipokuwa akisafiri kwa mashua haikuwa Asia kama alivyodhani, aliamini kuwa ilikuwa ni dunia mpya! Dunia hiyo mpya iliitwa America pamoja na visiwa vya Caribean na Bermuda.

Mwaka 2012 mnajimu wa Italia, Anthony Abreu Mora alirudia upya ukokotosi wa Eratosthens na kupata mzingo wa dunia kilometa 40,074 ambayo ni tofauta ya kilometa 36.

Haitoshi katika mzingo nwa dunia tu, Eratosthenes anaheshimiwa mpaka sasa kuwa ni mwasisi wa somo la Giografia. Alisoma vitabu mbalimbali kuhusu safari za mabaharia mbalimbali katika maktaba ya Alexandria na kujifunza zaidi kuhusu dunia na maeneo yake. Aliandika kitabu ambacho kiliitwa GEOGRAPHIKA, kitabu hicho kiligawanyika katika juzuu tatu. Kutoka hapo somo la Giografia likawa linajitegemea rasmi. Aliamua kutenganisha mafunzo kuhusu muundo wa dunia pekee na maeneo yake. Alianzisha istilahi ambazo bado zinatumika mpaka sasa katika Giografia. Ukuu wa somo la Giografia na aliuanzisha yeye ingawa wataalamu wengine baadae walikuja kuongeza vipengele vingine.

Kitabu chake cha Geographika  juzuu ya tatu aliandika kile alichokiita Jiografia ya kisiasa (Political Geography). Ni Giografia ambayo huzungumza uhusianao kati ya nchi na watu, serikali na watu, mipaka na watu, pia hueleza ksababu za watu fulani kufahamiana katika eneo fulani kwa sifa zinazolandana au kutokana na hali ya hewa ya eneo husika na uhusiano wake na serikali. Pia masuala ya mipaka ya nchi, uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari na mafunzo ya matokeo ya uchaguzi (Electoral Geography).  

Akiwa mkurugenzi mkuu wa maktaba ya Alexandria, Eratosthenes alibuni aina ya kalenda ambayo ni chimbuko la mfumo wa sasa wa kalenda. Alikokotoa idadi ya siku katika mwaka mmoja kutokana na mwendo wa dunia na njia yake. Baada ya kukokotoa alihitimisha kwamba mwaka mmoja una siku 365 na kila baada ya miaka minne kutakuwa na siku 366.

Eratosthenes alikuwa rafiki mkubwa wa Archimedes. Archimedes na Eratosthenes walijishughulisha na uundaji wa silaha za kivita kwa kutumia maarifa ya hisabati hasa Jiometri. Archimedes alipokuwa anatoa kitabu kipya, alikuwa anaweka nakala moja kwa ajili ya Eratosthenes. 

Aliishi maisha yake mpaka kufa nchini Misri katika mji wa Alexandria. Hii ni baada ya kuombwa awe mkurugenzi mkuu wa maktaba ya Alexandria, hivyo alitumikia wadhifa huo hadi alipopatwa na ugonjwa wa macho hali iliyomsababishia kuwa kipofu mpaka kifo chake.

© Kizito Mpangala (0692 555 874)

No comments:

Post a Comment

Maoni yako