Na Zitto Kabwe, Dar es Salaam
Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya
alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi,
vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa
facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji
wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA
tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa
utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo
katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake
katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera
za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi
wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza
kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania
wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona
katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya,
wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM
zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?
Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake
viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe
kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na
mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe
nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari
ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi
kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.
Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala
haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali
na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa
nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau
kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? Tumesahau kuwa
mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha
kuwa katika hatari kabisa?
Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi
dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la
biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo
anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za
Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za
kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za
Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau
hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali
huru ya Tanzania? Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na
Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu
ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu
Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata
ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na
yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana Haki
kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.
Mtwara na Lindi
wanakosea wapi?
Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga
mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe. Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao
zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha
kikundi cha Watanzania wachache sana. Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na
watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri
wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la watu.
Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji
wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho. Watu wa Mtwara wasijitenge
wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge ni umoja.
Serikali isiyosikia
Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya
kuzalisha umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya
Watanzania. Kwa kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara
wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili
kuhusu mradi huu wa Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa
mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa
imegunduliwa katika Kitalu namba 7( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam
katika Wilaya ya Temeke. Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa
na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za
shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija?
Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba
Dar dhidi ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na
kuusafirisha umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida
ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na
bwawa la Mtera? Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es
Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa
gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au
Mtwara?
Picha zote kwa hisani ya Said Msonga
Tuwasikilize watu wa
Mtwara
Watanzania sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni
wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru.
Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na watu wa
Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la
kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila kuathiri umoja wa
Taifa letu.
Ujio wa Sera, Maono
na Uongozi Mbadala
Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu
nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo
mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali
zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo
wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.
Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa
matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe
kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa
hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika sera. Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea
2015 na tukishika Dola wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa
pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa
kushirikiana nao kuleta maendeleo.
Siyo katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji,
elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa
mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na
zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara
ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.
NB: ZITTO KABWE ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema.
NB: ZITTO KABWE ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako