Na Markus Mpangala
Azimio la Zanzibar linafahamika kuwa
nyenzo iliyotumika kuua lile la Arusha.
Ingawaje viongozi wetu hawasemi
walichokubaliana kule Zanzibar, lakini hali haijifichi na inaonekana tunazidi
kusonga mbele.
Kuna mtikisiko wa kijamii unaendelea kwa
sasa, kutoka kwenye mitazamo na maisha ya ujamaa hadi kwenye kiwango cha chini
cha ubepari. Bahati nzuri ni kwamba ujamaa upo mioyoni mwetu yaani ndio maisha
ya watanzania.
Ni kwa sababu hii ndiyo maana Mwalimu
Nyerere aliuita ujamaa wa kiafrika. Sasa basi, katika azimio la Zanzibar viongozi
wetu bila shaka walikusudia kufanya mabadiliko katika uchumi. Bahati mbaya
mabadiliko hayo yalikuwa yanafanyika kwa kudanganywa na Benki ya Dunia na
Shirika la Fedha la Dunia.
Walichodanganywa viongozi wetu ni sera za
asasi hizo kuwa mwongozo wa uchumi wetu. Halafu hali ikiwa mbaya wanachofanya
ni kulaumu kuwa nchi imeshindwa. Sera za IMF na WB hazijali mazingira ya
mwanadamu wa kitanzania.
Maeneo mengi imetokea hali hiyo na hivyo
kuongeza kiwango cha ufukara kwa wananchi katika nchi husika. Ufukara huo
unachochewa zaidi na jinsi sera inavyopuuza hali halisi ya mazingira ya nchi na
utamaduni wa watu.
Sera za IMF na WB zinatokana na uzoefu wa
nchi za Ulaya na Amerika. Kule wataimba nyimbo kuwa ruzuku ni muhimu kwa mkulima
na wanakwenda nchi zetu za Afrika na kusema kama, ‘utampatia ruzuku mkulima
basi unampunguzia uwezo wa kuwa mbunifu.’
Lakini hatujiulizi kwanini wakulima wa Ulaya
wanapewa ruzuku na kadhalika. Sera za IMF na WB ndizo zilisababisha azimio la
Zanzibar kuonekana kituko mbele wa wajuzi wa mambo.
Azimio hilo lililo katika kibarua cha Azimio
la Arusha halikuja na mbinu mbadala ya kuweka msingi wa kukuza uchumi. Badala
yake likaja na mageuzi ya uchumi katika mkondo wa sera za IMF na WB.
Kimsingi hilo lilikuwa kosa na dosari
kiuchumi. Serikali yetu haikumwandaa au haikuhodhi moja kwa moja uchumi. Bali
ikadanganywa na IMF na WB kuwa jambo muhimu ni kufungua milango ya mageuzi ya
uchumi.
Milango iliyofunguliwa sio ile ambayo
ilifunguliwa na chama cha siasa cha ANC cha Afrika Kusini. Chama cha ANC
kilifungua milango ya mageuzi ya uchumi kwa sera yake, misingi yake na baadaye
kikawa kinapokea ushauri tu.
Sera kubwa ambayo iliing’arisha ANC ni
B.E.E. ( Balack Economic Empowerment). ANC ilikuwa wazi kabisa, hata kama sera hiyo
iliwalenga watu weusi wa Afrika Kusini, na kuwatenga wazungu ambao ni raia
halali wa nchi hiyo, lakini kilichofanyika ni kuziba pamba masikioni.
ANC ikasema inatambua kuwa B.E.E
inaonekana kama inabagua lakini ni wajibu wao kutimiza uwezeshaji wa watu weusi
katika mitaji ya kiuchumi. Mazao ya ANC ndio Tokyo Saxwalle, au familia ya kina
Khoza.
Mfanyabiashara Tokyo Saxwalle anafahamika
kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa na wawekezaji wa kiwango cha juu kutoka
jamii za waafrika. Ni kutokana na sera hiyo iliwezesha kuibua wafanyabishara,
wawekezaji na wajasiriamali wengine ambao walifanya kila jitihada kwa kutumia
sera ya B.E.E kufanikiwa.
ANC ikasema lazima watu weusi wawezeshwe.
Tafsiri sahihi hapa ni kuwawezesha wazawa. Hali hiyo ilitokana na miaka mingi
ya utawala wa kaburu kuwanyonya na kuwakandamiza watu weusi. ANC ilipania,
ikathubutu, ikatimiza dhamira yake.
Ni sababu hiyo tunaona baadhi wawekezaji wakubwa waafrika kutoka
Afrika Kusini, vinginevyo ubaguzi ulioanzishwa na makaburu ungeendelea
kuwafanya waafrika wabaki hohehahe.
Mfano wa pili ni Chujusong, Korea
Kaskazini. Tangu mwaka 1925 Korea Kaskazini chini ya chama cha kikomunisti
ilifanya jitihada kubwa ya kujenga uchumi huku ikitanganza kuwa ni Jamhuri ya Kisoshalisti.
Chujusong ni mpango wa kujitegemea
kiuchumi. Msingi mkuu ulikuwa kuhakikisha mitaji ya kiuchumi inakuwa huru ili
kuondokana na utegemezi kutoka nje. Sera hiyo ilichukua ngumu na kuhodhi
mwenendo wa nchi hiyo kujenga uchumi wake.
Polepole mabadiliko makubwa yakajitokeza
hadi Korea Kaskazini tunayoiona leo. Hapa kwetu sera ya wazawa tu ilitushinda, na
kwakuwa tulikuwa tumekosa uelewa wa kutosha tukadhani sera hiyo inabagua.
Laiti tungelikuwa na msimamo na uelewa wa
kutosha kuwa huo siyo ubaguzi sababu hata wageni walioingia nchini mwetu
waliwabagua wenyeji. Kwahiyo ili kukabaliana na pengo lililokuwepo zama za
ukoloni, ilipaswa serikali ya awamu ya pili ilipofungua milango kuruhusu
mageuzi ya kichumi, itunge sera za B.E.E.
Mpango wa kuwawezesha waafrika sio
dhambi. Mpango wa kuwawezesha wazawa sio dhambi. Wazawa hao maana yake tuwe na
wawekezaji sampuli ya Reginald Mengi.
Watu wa aina yake tuwe nao wengi ili
kuimarisha mitaji ya serikali na uchumi wetu. Tusipokuwa na misingi inayoakisi
ustawi wa taifa kiuchumi, itawezesha fedha nyingi za Tanzania kuishia mikononi
mwa wadokozi.
Na wadokozi wengine tulipowajua wakati wa
miaka ya 1990 ntumejikuta sasa nchi inabomolewa benki yake. Sasa baada ya
kuipoteza misingi hii tumejikuta tunahamasisha ujasiriamali.
Tunahangaika na ujasiriamali sababu
wakati wa kufungua milango ya mageuzi ya uchumi hatukujua mageuzi hayo
yanafanyikaje na uchumi utakuwaje.
Milango iliyofunguliwa ikawa ni kuruhusu
wachuuzi ambao walidhaniwa wawekezaji, wakawa wanachuma mali za watanzania.
Sasa, akili inapoibuka kipindi hiki tunajikuta kumbe wakati tunazika azimio la
Arusha tulipaswa kutamka kwakuwa lazima tuwezeshe wazawa. Lazima watu weusi
wawezeshwe kwenye mitaji. Na iwe sera sio huruma. Kwa sasa tumejikuta tunao
wawekezaji wengi kutoka nje, halafu wawekezaji wa ndani bado uwezo wao sio mkubwa sababu hawakuwa sehemu ya
mageuzi ya uchumi yaliyofunguliwa wakati ule.
Nionavyo, tunatakiwa kuwa na sera za kuondokana na uchuuzi wa
kijasiriamali. Lazima tujenge uwezo kwa wazawa. Lazima tuwaige ANC kwa sera ya
Black Economic Empowerment. Tujiulize, hivi kuna ofisi ngapi za Benki
ya Dunia na IMF katika nchi za Kiarabu? Jibu hakuna ofisi hizo kwakuwa
hazihitajiki. Tafakari. Nahitaji changamoto.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako