September 30, 2017

UTUNZI WA VITABU NA KISWAHILI CHA PROFESA SHAOPING

NA KIZITO MPANGALA

KESI YA ALMASI ni kitabu kilichoandikwa na Profesa Rao Shaoping wa China. Kitaaluma yeye ni mhandisi. Alijifunza Kiswahili nchini Tanzania kwa muda wa mwaka mmoja na ushee, mwalimu aliyemfundisha aliitwa Ali Omari Mzee.
Profesa Shaoping ndiye msimamizi wa kazi za TAZARA wakati inajengwa. Alikuwa akimtafsiria Mwalimu Nyerere mazungumzo aliyokuwa akijadiliana na wenzake. Pia alikuwa mkaliamani kwa Mh. Salim Ahmed Salim, Mh. Rashid Kawawa, Spika Adam Sapi kwa mazungumzo aliyokuwa akijadiliana na Wachina wenzake. Na mwaka 2013 Profesa Shaoping alikuja tena nchini Tanzania kumtembela Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Profesa Shaoping anasema hivi "ninaipenda Tanzania. Ninawapenda watu wa Tanzania". Profesa Shaoping anayafahamu maeneo mengi nchini Tanzania ambayo amewahi kutembelea, maeneo hayo ni kama vile Kisuwa cha Saa Nane, Arusha, Ifakara, Iringa, Kimbwe, Kidatu, Mikumi, Makambako, Mbarali, Tunduma, Zanzibar, Moshi, Dodoma na kadhalika.

Profesa Shaoping ameandika kitabu hiki kwa bidii mno. Anasema tangu tuwe Koloni la Mjerumani na baadae Mwingereza, wageni hao hawakuwa na morali ya kutunga riwaya za Kiswahili lakini yeye kama mgeni alipenda sana kuacha kitabu kwa Kiswahili, naam, ndicho hiki hapa pichani.



Rai yangu ni hii:
Ninampongeza sana Profesa Shaoping kwa uhodari wake huu. Profesa Shaoping hana shahada ya Kiswahili. Amejua lugha hii kwa ya Kiswahili kwa kufundishwa kwa lengo la kuwa na mawasiliano mazuri na watu wa Tanzania wakati alipokuwa akisimamia kazi za kuisuka TAZARA unayoiona sasa. Alifanya bidii na ameweza. Safi.

Sasa yule anayesema ni msimaizi wa lugha ya Kiswahili nchini hapa kwa niaba ya serikali furaha yako ni nini kuwabana wenye lugha watambe nayo na kuipamba?Unafurahia lugha hii ya Kiswahili itumike na wageni ambao hawana shahada ya Kiswahili lakini wanafanya vizuri kama Mswahili mwenyewe asiye na shahada ya Kiswahili? Utungaji siyo shahada. 

Profesa Shaoping ameandika vizuri sana japokuwa hana shahada ya Kiswahili na kwa maana hiyo yeye sio Mswahili kamili lakini anajua, sasa inakuwaje Mswahili kamili anayejua zaidi kuliko Profesa Shaoping abanwe banwe wakati lugha ni yake na kila siku anaitumia?

Kama ni kusisitiza matumizi mazuri ya lugha basi ni jambo la kuelekeza na kutoa agizo kwamba sarufi izingatiwe vizuri lakini si kudai Mswahili lazima awe na shada ya Kiswahili ndipo aandike. Kuna wengi wana shahada za Kiswahili lakini hawaandiki na tena wengine hawana ubunifu wa kufanya hivyo ingawa wana shahada za Kiswahili.

Ukisoma diwani za mzee Shaaban Robert ingawa hakuwa na shahada ya Kiswahili ameidadavia lugha kwa ubora mzuri tu. Sasa basi kufukia vipawa vya watu kwa kigezo cha usomi ni ujinga. 

Leo watu wanasafiri angani huko kwa ndege, lakini msingi wa ndege ulibuniwa na vijana wawili tu ambao hata sekondari hawakuingia. Walianza kuwa mafundi baiskeli kuziba pancha, baadae wakatambua kwamba wana nini cha pekee.
Leo marubani au mafundi wa ndege wanapatikana kwa shahada, safi na utendaji unaonekana vyema. Sasa kwenye waandishi mnataka wawe wabaandika kwa lugha ya kigeni ndipo mseme ni wasomi? Ebo!

Wasomi wenyewe hawaandiki sasa kwa nini wenye vipawa mnawakaba? Haya ni MAZISHI YA LUGHA YA KISWAHILI, na wanaoizika ni maharamia wanaojiita wasomi wa Kiswahili. Huu msiba ni wa kulazimisha. 

Saadani Abbas Kandoro alikuwa na shahada ngapi za Kiswahili? Ameandika diwani nzuri sana. Ujuzi lazima uzingatiwe. Vinginevyo itakuwa kama upande wa uhandisi ambapo kandarasi nyingi ni za kigeni, tena wengine hawana kiwango cha kutosha cha usomi lakini ubunifu kutoka ndani mioyo unawafanya wamakinike na bidii yao. Kiswahili ni lugha ya taifa kama tusemavyo, ndivyo ilivyokuwavyo, ilivyo, na itakavyokuwavyo.

0692 555 874

No comments:

Post a Comment

Maoni yako