September 30, 2017

NADHARIA YA FIBONACCI.

NA KIZITO MPANGALA
 
FIBONACCI alikuwa mwanahisabati mdogo nchini Italia. Aliraruliwa uhai wake na watu "wasiojulikana" kutokana umahiri wake katika hisabati. Wakati anararuliwa uhai wake alikuwa na umri wa miaka 21 tu na tayari alikuwa amekwishachapisha ubunifu wake wa namba katika kitabu.

Ingawa kazi zake nyingi hazikutambuliwa zilikohifadhiwa, lakini ubunifu wake maarufu wa kufinya namba umekuwa na umuhimu mkubwa katika uhandisi na usanifu wa majengo. Utafiti ulifanyika kwa kina na kuweza kuona kwamba kijana Fibonacci amechangia kadiri ya uwezo wa ubongo wake katika hisabati. Hisabati inaishi, ili kujua inaishi basi usione aibu kujufunza na kuona wapi inatumika.


Mfumo wa elimu katika nchi nyingi barani Ulaya, Amerika, na Australia umejengwa katika misingi ya udadisi mkubwa. Udadisi huo ni wa kutaka kujua kwamba anachafundishwa mwanafunzi anaweza kukitumia au kuona kinatumika namna gani. Ndio maana ukitazama vitabu vingi vya hisabati vilivyoandikwa maeneo hayo ni kama vile mapambo tu fulani au masimulizi ya picha mbalimbali lakini ndio msingi ulipolala.

Kinachofundishwa katika hisabati kinatolewa na uwezekano wake katika matumizi maishani mwetu. Hisabati ina msaada mkubwa sana. Ukweli ulivyo, hisabati haiwezekani kuelezwa kama hadithi, ni lazima iwe katika maandishi na kisha kutolewa maelezo kwa kina zaidi. Hisabati si sawa na hadithi ya Pwagu na Pwaguzi.

Pichani ni sehemu za majengo ya hoteli moja katika pwani ya Australia. Upande wa kushoto ndivyo inavyoonekana kutoka juu, na upande wa kulia ni sehemu mojawapo ya majengo hayo. Hisabati inaendana na sanaa. Ndio maana tunasema "kusanifu majengo". Ukitazama kwa makini jengo hili upande wako wa kulia lina umbo la gamba la konokono, ndivyo ilivyo.



Halafu mwonekano wa jumla wa hoteli hii kutoka juu ni kama vile aina fulani ya mduara ambao una mvuto wa kipekee. Yaani kama vile ghorofa lenye ngazi za kuzunguka ambapo mara nyingi majumba ya makasisi na makanisa yao yamebuniwa namna hiyo tangu zama za kati (Medieval Period) kule Ulaya ambapo walijifunza mambo mbalimbali kupitia maandiko ya waliowatangulia ndio maana wanathamini vitabu. 

Sisi nasi tunaweza kufanya hivyo, wahandisi wapo, kumaliza kozi sio mwisho wa kuitumia. Endelea kujiboresha kwa vitabu mbalimbali kuhusiana na kozi yako, furaha yako isiwe tu kupata GPA ya juu zaidi, furaha na ufahari wako uwe katika kutenda ulichojifunza. Jiapishe mwenyewe kwanza!

Hisabati inaishi. Wahandisi wetu wajionee fahari katika hilo na utendaji. Kuitwa injinia uwe injinia kwa ukweli wa dhamira yako. Hivyo basi, tusichoke kuhimiza hisabati mashuleni ili udadisi uongezeke katika roho ya maarifa kwa wanafunzi, na mwalimu uwe mtu mpya mara kwa mara, jiboreshe kwa vitabu mbalimbali ili nawe ujionee fahari zaidi na furaha ya somo hili. 

Mwambie mwanafunzi kwa nini tunahitaji duara? Kwa nini tunahitaji mraba? Kwa nini tunahitaji vekta? Kwa nini tunahitaji matriksi? Kwa nini tunahitaji uwiano? Kwa nini tunahitaji mstatili? Kwa nini tunahitaji pembe mbetuo? Kwa nini tunahitaji pembe mkabala? Kwa nini tunahitaji logarizimu? Kwa nini tunahitaji hyperbola? Kwa nini tunahitaji parabola? Kwa nini tunahitaji ellipse (duara dufu)? kwa nini tunahitaji Kalikulasi? na kadhalika.

Tujiweke katika uimara wa mambo yetu. Ukiwa mtu wa rasilimali watu uwe mwanarasilimali watu kweli. Ukiwa mhasibu uwe khasibu kweli. Ukiwa mchoraji uwe mchoraji kweli. Na kadhalika. Lakini rai yangu ni hisabati. Watu wengi wanahimiza wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, jambo nzuri sana. Lakini sayansi ina hisabati ndani yake kama kiungo muhimu kama vile nyanya kwenye himaya ya mpishi. Basi wanafunzi na walimu na watu wengine wenye kupenda hisabati na matumizi yake basi waipende kwa dhati kama vile mpishi anavyopenda kijiko jikoni. 

Shukrani kwa Mungu kwa kumuumba kijana Fibonacci na kumjalia kipawa cha hisabati. 

© Kizito Mpangala.
(Mwanahisabati)

0692 555 874

No comments:

Post a Comment

Maoni yako