October 02, 2017

DUNIA KUSHUHUDIA TAIFA JIPYA LA KURDISTAN?


NA MWANDISHI WETU

SEPTEMBA 25 mwaka huu jamii ya wakurdi waliopo Kaskazini mwa Iraq katika jimbo la Kurdistan walipiga kura ya maoni kwa lengo la kujitoa  kutoka kwenye dola la Iraq na kuunda taifa lao.Uamuzi wa wakurdi wa Irak unashahibiana na ule wa wananchi wa jimbo al Catalunya (Catalonia) la nchini Hispania ambalo kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipigania kujitenga kutoka Uhispania na kuunda taifa lao.
Asilimia 93 ya kura zilionesha kuwa wakurdi wa Iraq wanahitaji kujitawala wenyewe. Tume ya uchaguzi ilisema idadi  ya waliyoshiriki kura ya maoni ilikuwa zaidi ya asilimia 72.Mamilioni wa wakurdi walishiriki kura hiyo licha ya onyo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na majirani zake. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema imesikitishwa na hatua ya serikali ya jimbo la Kurdistan kuandaa kura hiyo ya maoni.

Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Mrekani ilisema, "Mahusiano ya kihistoria kati ya Marekani na watu wa Kurdistan hayatabadilika kufuatia kura hiyo lakini tunaamini hatua hii itasababisha kutokuwepo na uthabiti na kuzidisha maisha magumu katika eneo la Kurdistan na watu wake." 



Maafisa wa kikurdi nchini Iraq walianza kuhesabu kura katika jimbo la Kurdistan na maeneo mengine yaliyokuwa na utata kuanzia saa moja usiku.
Kulingana na tume ya uchaguzi watu milioni 5.6 waliandikishwa na kuwa na haki ya kupiga kura katika vituo 2,065 katika jimbo hilo la Kurdistan na maeneo mengine yanayodhibitiwa na wakurdi Kaskazini mwa Iraq. Kura hiyo imefanyika licha ya kupingwa vikali na serikali ya Iraq inayoitaja kuwa kinyume na katiba ya nchi. 

Huku hayo yakiarifiwa Waziri mkuu wa wakurdi nchini Iraq Nechirvan Barzani ameikosoa serikali ya Iraqi na mataifa jirani wanaoipinga kura ya maoni iliyofanyika jana na inayotaka Uhuru wa jimbo la Kurdistan. Amesema serikali yake inatarajia kufanya mazungumzo ya kina na majirani zake wa kikanda kuhakikisha kunakuwepo na mahusiano mazuri kwa maslahi ya pamoja na heshima. Ameongeza kuwa watu wake wanatumia haki yao kuamua mustakbal wao, huku akisema wamechukizwa na misimamo ya mataifa mengi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Awali Naibu rais wa Iraq Nuri al-Maliki alisema kura hiyo ni kutangaza vita dhidi ya umoja wa watu wa Iraq.  Umoja wa Mataifa pia ulionya kwamba kura hiyo huenda ikayumbisha usalama.Hata hivyo Israel imekuwa nchi pekee iliyounga mkono kura ya maoni ya Kurdistan ya Uhuru wa jimbo lao na kujitawala wenyewe. Mapema mwezi huu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Israel inaunga mkono juhudi halali za wakurdi kupata taifa lao.

Nchi jirani za Syria, Iraq, Uturuki na Iran ambazo nazo zina idadi kubwa ya jamii ya wakurdi hazikupendezwa na hatua hiyo kwani zimedai inaweza kusababisha harakati za kutaka kujitawala kwa wakurdi waliopo nchini mwao
Iran imeongeza pia kuwa, Uhuru wa wakurdi unahatarisha usalama wa Iran kwani mataifa ya magharibi yanaweza kwenda kuweka kambi karibu kabisa na Iran.

Uturuki nayo ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa ikipinga kujitenga kwa wakurdi imeapa kuzuia usafirishaji wa mafuta toka Kurdistan kupitia Uturuki kwenda kwenye solo la kimataifa. Uturuki ndiyo lango kuu pekee la kupitia mafuta ya Kurdistan iwapo taifa hilo litazaliwa.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi za Uturuki, Iran na Iraq zilionya kuwa kura ya maoni ingehatarisha mapambano yao dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu ISIS na hivyo kuweka shakani mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.
Rais wa Taifa la Wakurdi, Masoud Barzani amesema kura ya maoni ni mafanikio tosha kwao kufikia lengo lao ingawa katiba ya Iraq haitoi mwanya kwa wakurdi kujitenga na kuunda taifa la Kurdistan.

Kwa mujibu wa Ibara ya kwanza ya Mkataba wa Kimataifa wa Montevideo wa mwaka 1933 (Montevideo Convention on the Rights and Duties of States), ambao umeorodhesha sifa za kuunda Dola, umeeleza hivi:

Mosi, wakazi wa kudumu (watu ambao wanaishi hapo au wana maisha ya kudumu).
Pili, mipaka isiyotiliwa shaka au kutokuwa na mgogoro (ingawa si lazima sana kwani wakurdi wamejumuisha eneo la Kirkuk ambalo linagombewa).
Tatu, uwapo wa serikali. Wakurdi wanayo serikali na Rais wao ni Masoud Barzani.
Nne, nafasi ya kuingia, kutambuliwa pamoja na kujihusisha na mataifa mengine. Kurdistan inatakuwa kuwa na sifa hii ya kutambuliwa na madola mengine.

Baada ya kuweka sifa hizo ndipo tunakuja na swali, je kura ya maoni waliyopiga Wakurdi itawasaidi kuunda taifa lao la Kurdistan?
Vikosi vya Wakurdi vya Peshmerga vimechukua udhibiti wa mji huo wenye utajiri wa mafuta ambao una waarabu wengi na sehemu zingine zinazodaiwa na Baghadad kwa zaidi ya miaka mitatu.

Wapiganaji wa kishia wanasema kuwa hawataruhusu mji wa kirkuk kuwa sehemu ya eneo huru la Kurdistan. Wakurdi ndio jamii ya nne kwa ukubwa eneo la Mashariki ya Kati lakini bado hawajapa taifa. Nchini Iraq ambapo wanachukua asilimia 15 hadi 20 ya watu milioni 37, wakurdi wamekumbwa na miongo kadha ya ukandamizaji wa serikali za kiarabu kabla ya kujitenga kufuatia vita vya Ghuba vya mwaka 1991.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako