September 30, 2017

BATAMZINGA SI MWEWE

1    Wako wapi wanaume, majemedari ya nguvu,
Wenye nguvu ya umeme, wasofikwa na uchovu,
Watu wasio kinyume, ubongo uso mbovu,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wako wapi wanawake, watalamu wa urembo,
Kwao haki itendeke, wakaziimbe na nyimbo,
Mioyoo iridhike, pasi kushikiwa fimbo,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume watukutu, ni vema watakasike,
Mioyo yao ya kutu, inayo mengi makeke,
Miili ya ukurutu, ni vema isafishike,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake wajeuri, ni vema wasafishike,
Walojawa na kiburi, vizuri warekebike,
Wasiopenda sifuri, jamani wabadilike,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume na umende, vema kando wajiweke,
Sikieni chonchonde, mizigo msijitwike,
Mateke siyo makonde, naomba nieleweke,
Btamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake wasagaji, nawambia mara mia,
Wala mimi siyo jaji, salamu nawapatia,
Kwenye miji na majiji, wengi wamejichimbia,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Nawambia mara mia, wanawake wasagaji,
Asili mwajikania, shababi hamuhitaji,
Fedha mwajitazamia, na ndio wenu ulaji,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume wabakaji, nanyi pia nawambia,
Mchanga siyo theruji, msemo huu natia,
Batamzinga wa maji, mwewe hawezi ingia,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Nanyi pia nawambia, wanaume wabakaji,
Wakubwa kuwakimbia, leo mimi nawahoji,
Raha gani jibakia, mwataka kuvishwa taji?
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Maneno haya shahada, batamzinga si mwewe,
Niwafanyie ibada, na mapepo mkemewe,
Nikakuvisheni shada, mkaruke kama mwewe,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake wachunaji, visingizio lukuki,
Mnaupenda ulaji, na mkinyimwa ni chuki,
‘Bebi’ jina la hitaji, ukipata hushikiki,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada

Wanaume wakabaji, ni mashati kushikana,
Mchanga siyo theruji, siku mtapatikana,
Kwenye miji na majiji, daima mwapatikana,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake wasaliti, kwa kigezo cha ndarama,
Kandambili siyo buti, jirekebisheni jama,
Sifagilie mauti, mkianza kuyapima,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume wapigaji, bakora kwa wake zao,
Na wale watukanaji, wakilewa pombe zao,
Hakika pombe si maji, wanaonea wake zao,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake wachezaji, mechi uwanja wa fisi,
Bado tunawahitaji, taifa linawamisi,
Msijifanye magwiji, kuwang’ang’ania fisi,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume watekaji, sikilizeni jamani,
Mnayataka mataji, mtunukiwe mjini?
Mwaangalia ulaji, mliopewa gizani,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Maneno haya shahada, batamzinga si mwewe,
Nisikilize we dada, kaka sikiliza nawe,
Niwafanyie ibada, mwondokane na kiwewe,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume mafisadi, wanawake pia wamo,
Mwadhaniwa ni masudi, kuiachama modomo,
Kuacha hamna budi, siyo mpaka mkono,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume walaghai, mabinti kuwahadaa,
Ili kwamba wafurahi, baadae waambaa,
Tawafanya matapishi, kishawasha mshumaa,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake na dharau, kwa maneno midomoni,
Waniambia nyang’au, taipu yenu hamoni,
Tafakari angalau, uyaone ya rohoni,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume wenye nia, huchapa kazi daima,
Ni ngumu kung’ang’ania, mapenzi ya mshumaa,
Ya kesho hufikiria, kwa baraka za Rabana,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Mwanawake mwenye nia, maisha kusonga mbele,
Daima hujitambua, ya kwamba ni mwanamke,
Anamuomba Rabana, mwanaume bora apate,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanaume wako wapi, waendesha pikipiki,
Hivi mnakosa vipi, wateja hawafikiki,
Kajifungeni mishipi, mkanukie miski,
Batmzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wanawake wa vyuoni, rekebisheni mavazi,
Hamuendi shindanoni, wala kutafuta wenzi,
Tulieni darasani, na poleni kwa zingizi,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Mwanaume makini,  huitambua thamani,
Ninasema kwa yakini, thamani yenye amni,
Hababaiki kichwani, asili imo kichwani,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada,

Wengi watanilaumu, eti kwamba natukana,
Nimesema kwa nidhamu, ni nasaha kupeana,
Rai yangu siyo ghamu, machache kukumbushana,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Japokuwa siyo wote, wenye nia njema wamo,
Tutafakarini sote, kama mwewe ni pono,
Mwewe atabaki mwewe, pono atabaki pono,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Batamzinga na yeye, habadiliki mwewe,
Sasa mimi na wewe, tutafakari tuone,
Ndoa ya mume na mume, kama safi tuoane,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Kugeuza hiki vile, ajuaye ni Rabana,
Mambo ya asili wewe, usipende kubishana,
Ndoa ya mke na mke, hii wapi uliona?
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Mengi nimeyanena, na mengine sijanena,
Tafakari kwa upana, shairi hili kijana,
Tena la muhimu sana, akubariki Rabana,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Dada na kaka amini, aminini mkiwaza,
Tafakari kwa makini, kweli yatakuongoza,
Wanawake sikieni, wanaume natangaza,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Wasalamu natamka, awabariki Rabana,
Mie sasa naondoka, tafakari kwa upana,
Wazo litakufika, kusema ninakazana,
Batamzinga si mwewe, maneno haya shahada.

Kizito Mpangala

No comments:

Post a Comment

Maoni yako