September 30, 2017

MTOTO UMLEAVYO

Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo,
Akilelewa hovyo, naye atakuwa hovyo,
Ukimdekeza hovyo, na atalemaa ovyo,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Mtoto mlee vema, aje kukusaidia,
Umzoeshe mapema, kufua na kufagia,
Tamsaidia mama, baba atafurahia,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Ukimletea ukali, atakuwa mwoga sana,
Atajiweka mbali, si jambo lenye maana,
Hapo huzuka kitali, sio vema kuchapana,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.


Kimzoesha matusi, ataona lugha bora,
Hatatukana Kirusi, Kiswahili kichobora,
Mfundisheni upesi, mambo mengi yalobora,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Vinasaba atarithi, kutoka kwa wazaziwe,
Dunia isimghuri, na wewe umuhimize,
Bidii kufanya kazi,  maishani imfae,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Marifa simnyime, kujifunza muhimize,
Tabia njema mweleze, maishani imfae,
Kuoga umfundishe, aje ajiogeshe,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

 Vibaya simburuze, atauona udhia,
Kwa hekima mwelekeze, naye atafurahia,
Pia muache acheze, afyaye kujikulia,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Mzazi nisikilize, mtoto wako mfundishe,
Utukutu makataze, mwilini asiumie,
Kucheza mwache acheze, mwiliwe uimarike,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Mfundishe nzuri njia, afuate kwa nidhamu,
Nayo njema tabia, aachane na dharau,
Maishaye furahia, kwa kuishika adabu,
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo.

Wasalamu natamka, wazazi menielewa,
Leeni bila kuchoka, bado hamjachelewa,
Japo jasho lawatoka, mazuri  mtapatiwa.
Mtoto umleavyo, hivyo ndivyo akuavyo


Kizito Mpangala    0692 555 874 

No comments:

Post a Comment

Maoni yako