September 30, 2017

MADAKITARI WENGI

1   Kijana mimi rijali, ninaishi Afrika,
Nipo hapa kwa asili, siwezi kubadilika,
Jambo hili nakubali, kichwani halitatoka,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Juzi nilipata shida, tatizo langu kusema,
Nilimueleza dada, akamueleza mama,
Nilingoja kwa muda, na kichwa kikiniuma,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Dada na mama wakaja, ili kuijua homa,
Mahoma nikayataja, yakamshangaza mama,
Madakitari kataja, basi homa itakoma,
Madakitari ni wengi, waniweka niiapanda.

Kwa mchungaji tukaja, yasemwa ni dakitari,
Mahoma nikayataja, asema nina kiburi,
Zikanijaa na hoja, nikawa natafakari,
Mdakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Mahoma ninayo mengi, kwanza ni maisha bora,
Ninataka pesa nyingi, ninaitaka ajira,
Niinunue na rangi, nikajifunze kuchora,
Madakitari ni wengi, waniacha niapanda.

Homa za vijana wengi, Afrika nako Asia,
Matarajio nimengi, hayajapata tulia,
Ndoto zimekuwa nyingi, ndani ya hii dunia,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Msikie mchungaji, na dawa yake jamani,
Anautaka ulaji, homa hizi maishani,
Anautaka na uji, nipeleke kanisani,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Anasema niokoke, homa zote zitaisha,
Kisha hela nimtoe, ndio malipo ya dawa,
Kesho yake nikamwone, vidonge kuniongeza,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Homa zilezile tena, kwa dakitari mwingine,
Tena bado sijaoa, anipatia mawenge,
Asema jini mahaba, hataki mie nioe,
Madakitari ni wengi, waniweka niapanda.

Kukosa kwangu ajira, kijana mie Afrika,
Asema jini Makata, anazuia ajira,
Nimesikiliza sana, nimeishia kununa,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Mpiga tunguri nae, anasema nimerogwa,
Tena homa zilezile, kweli amelikoroga,
Na kwenye ungo tupae, nionyeshwe aloroga,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Homa sijapata dawa, kwa madakitari wote,
Homa ya kuajiriwa, dawaye hakuna mwote,
Homa ya kutajirika, hainayo dawa kote,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Kwa dakitari mwingine, asema nina mapepo,
Ninataka niwaone, mapepo hawa walipo,
Hahitaji niwaone, eti ni kama upepo,
Madakitari ni wengi, waniacha njiapanda.

Mwote nilimopitia, sumuni  nimelipia,
Dawa wameshaikosa, wamebaki kujificha,
Nimewajaribu sana, na hawajafurukuta.
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Siwadharau kabisa, madakitari murua,
Imanini wajitosa, dawa hawajaijua,
Kwa nini wameikosa, dawa kuigundua,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Afrika funguka sasa, tuchape kazi jamani,
Kujifunza nako ruksa, tujinasue tunduni,
Imani zetu kabisa, zisituchoshe jamani,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Mungu hatatushushia, tusipofanya bidii,
Shughuli kukazania, na bidii haiozi,
Mwanatunguri tulia, si kila kitu uchawi,
Madakitari ni wengi, waniweka njiapanda.

Na Kizito Mpangala

No comments:

Post a Comment

Maoni yako