October 12, 2014

KWANINI AFRIKA HATUNA AFRICOPHONE AU BANTUPHONE?



Na Markus Mpangala, Dar es salaam

KUNA wakati unaweza kujiuliza utamaduni wa viongozi wetu kuzithamini jumuiya za nje ya Afrika unetokana na nini. Tunaweza kujitetea kwa namna nyingi ikiwemo uchumi duni unaosababisha tukose nguvu ya kitaifa.

Unaweza pia kuorodhesha sababu nyingi mno ambazo zinaweza kutunyima uwezo wa kuwa na jumuiya zinazotambulisha uwezo wa kiafrika kwenye siasa, uchumi, utamaduni na jamii.


Yapo maeneo tumeweza kuyalinda na kuonesha sisi ni waafrika halisi na tunalinda uafrika wetu. Bahati mbaya pia yapo maeneo yanayojenga nguvu na ubora wa Afrika hayajapewa kipaumbele.



Moja ya kazi za Cheik Anta Diop,

Mwanazuoni Cheikh Anta Diop alihubiri sayansi, siasa na utamaduni wa Afrika. Diop alihubiri uafrika kama Marcus Garvey, Malcolm X, na wengineo. Diop alihubiri ubora na nyakati zilizovurugwa katika historia ya mwafrika.

Kwamba Afrika kuna utamaduni, lugha, mazingira, staha na mambo yanayoweza kulibatumbulisha bara hilo kwa Uafrika wao.


Katika bara la Afrika ambalo linatajwa kugunduliwa kwa binadamu wa kwanza kuishi, lina sifa nyingine mbaya zaidi kwamba baadhi ya wakazi wake hawazipendi nchi zao.
Kwamba hawapendi utambulisho wao.

Hawapendi utamaduni wao na ndio maana hujishughulisha kubadilisha wajihi (kujichubua) na mengine yasiyowatambulisha kama waafrika.

Madai haya yamekuwa yakitolewa na wataalamu pamoja na wanahistoria wengi wa Ulaya pamoja na Amerika.
Sababu kubwa inajulikana kuwa waafrika wamejikuta kwenye utegemezi mkubwa wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.


Jambo zuri zipo jamii ambazo zinalinda tamaduni zao na zinajali zaidi. Hata hivyo katika Bara la Afrika kuna vituko vingi na kuonesha dhahiiri kutegemea mawazo na fikra za kigeni.
Katika Afrika kuna nchi zipo kwenye Jumuiya ya Madola. Kwamba ni nchi zinazofurahia kutawaliwa na ukoloni wa Uingereza.


Katika Jumuiya ya Madola kuna wanachama wanaokutanishwa kila mara kwenye mikutano yao. Nchi hizo ambazo ni makoloni ya zamani ya Uingereza kwa upande wa siasa.


Upande wa pili kuna Michezo ya Jumuiya ya Madola ambao huwakutanisha mataifa yote yaliyotaliwa na Uingereza. Kwamba mataifa hayo licha ya kupata uhuru wa bendera bado yamekubali kuwa chini ya himaya ya wakoloni.


Safari hii wakoloni wakiwa wanatawala kutoka nchini mwao. Katika maeneo hayo mawili kutoka sehemu moja; waziri mkuu wa Uingereza huendesha vikao na mikutano pamoja na marais wa Afrika hususani nchi zilizotaliwa na Uingereza.


Rais Julius Nyerere na Fidel Castro wa Cuba.

Kwenye michuano ya Jumuiya ya Madola Malkia Elizabeth II wa Uingereza kuwahutubia wanamichezo na wanaoshiriki michezo hiyo wakiwakilisha kutoka mataifa yaliyokuwa chini ya himaya ya ukoloni.


Michuano ya mwaka huu ilifanyika mjini Glasgow nchini Scotland. Malkia anatawala nchi hizo kwa namna nyingine katika michezo ya madola na katika uchumi na siasa kwenye jumuiya hiyo.


Hayo ni mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza, kwamba tunajinasibu kupinga ukoloni na kufundisha wanetu kuwa akina Kibanga waliwachapa makonde wakoloni hata wakatokomea.
Kwenye chaguzi mbalimbali ndani ya Umoja wa Afrika, mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza yanaweza kujipanga na kutamba kuteteana ikiwemo kupeana nafasi za vyeo na kupigiana upatu kwa wagombea wao.


Mataifa haya ndiyo yanajigamba ni wazungumzaji wa lugha ya kiingereza na yanaitwa kwa kifupi Anglophone.
Tukigeukia upande wa pili tunakutana na mataifa yaliyotaliwa na Ufaransa. Mataifa haya yanajigamba kuwa ni wazungumzaji wa lugha ya Kifaransa, na huitwa Francophone.


Aghalabu kwenye kinyang’anyiro cha uongozi ndani ya Umoja wa Afrika (AU) tunashuhudia mnyukano mkubwa baina ya pande mbili; Anglophone dhidi ya Francophone.


Kwamba wale wenye kundi la Francophone walipiga kampeni kubwa kwa ajili ya Jean Ping ambaye ni mgombea kutoka kambi yao wakati wa kinyang’anyiro cha Ukuu wa Tume ya Umoja wa Afrika.


Mgombea wa Anglophone, Dk. Dlamini Nkosozana-Zuma alimshinda Jean Ping wa kambi ya Francophone, hivyo kuwa mkuu mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika.


Kwenye nchi za Francophone, ulimwengu ulishuhudia wakiundiwa jukwaa jingine la Francafrique ambalo lilikuwa mahususi kuziweka pamoja na kujenga uhusiano baina ya nchi za Kiafrika zilizotaliwa na Ufaransa.


Francafrique ni sawa na ilivyokuwa ajenda ya Francophone. Ufaransa haikuishi hapo, iliwahi kumpa mwaliko aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa kuhudhuria mkutano mkubwa wa kundi la Paris Club.


Kundi hilo linahusisha wachumi wenye nguvu zaidi na wanaotoa misaada ushauri wa kiuchumi na madeni kwa mataifa mbalimbali.


Ureno nao hawajabaki nyuma. Mwaka 1996 nchi zote zilizotawaliwa na Ureno zilijumuishwa kwenye jukwaa lao, Lusophone Africa.


Nchi zinazounda Lusophone Africa ni Angola, Cape Verde, Guinea-Bissau, Msumbiji, na Sao Tome and Principe. Awali nchi hizo ziliunda umoja wao wa ushirikiano unaojulikana kama PALOP (African Countries of Portuguese Official Language).


Hilo lilikuwa kujibinafsisha kwenye himaya ya Ureno sambamba na mkondo wa Anglophone na Francophone.
Katika dhana hii kulikoni bara la Afrika hatuna Bantuphone wala Africophone? Kwamba imekuwaje rais kwa viongozi na wananchi wa Afrika kujitambulisha kwenye Jumuiya za wakoloni wao Anglophone (Uingereza), Francophone (Ufaransa), Lusophone Africa (Ureno)?


Kwa mantiki hiyo lazima tujiulize maswali, inawezekanaje waafrika wakakubali kuwa jumuiya za Bantuphone na Africophone hazifai kwao, badala yake kuzing’ang’ania zile za wakoloni?


Ni kitu gani kinakwamisha kuundwa jumuiya za kiafrika kama Bantuphone na Africophone kuliko kuwekeza akili zetu kwa jumuiya za kikoloni?


Swali hilo linaweza kujibiwa kirahisi mno, kwamba huenda waafrika wanajisikia fahari zaidi kuongozwa na wakoloni licha ya kudai walipambana ili kuwafukuza kwenye ardhi zao.
Wakoloni wanatumia mbinu za jumuiya hizo kama nyenzo ya kuendeleza ukoloni wao kwa mataifa. Sielewi ndugu zangu.


Baruapepe; mawazoni15@gmail.com

© Andunje wa Fikra, 2014

No comments:

Post a Comment

Maoni yako