Na,
Albert Sanga, Iringa
Leo ni mwaka mmoja kamili umepita tangu nilipoandika
makala hapa safuni iliyokuwa na kichwa, “Njooni shambani mtajirike”. Ilikuwa ni
makala iliyotoa shime kwa watanzania kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwenye
kilimo cha miti.
Katika makala ile niliwaeleza watanzania upana wa
faida ya kuwekeza katika miti aina mbalimbali huku nikijikita katika miti ya
mbao, karatasi na nguzo. Nilichambua kwa
kina sana gharama za upandaji wa miti hiyo, muda wa kuvuna, soko lake lilivyo
na matarajio ya biashara hiyo kwa miaka ya baadae.
Leo ninaandika tena makala hii huku nikiwa na furaha
tele moyoni mwangu kwa sababu makumi ya watanzania waliuitikia mwito wangu na
wakachangamkia fursa hii. Kama ambavyo nilitamani iwe, ndivyo ilivyokuwa kwani
wengi wamenijulisha kuwa hawakulazia damu, walichangamka na kuanza kuwekeza.
Ingawa mimi ni mmoja ya watanzania ambao
wanajishughulisha na uwekezaji katika mashamba ya miti mkoani Iringa, kiu yangu
ilikuwa ni kuona watu wakichangamkia fursa hii mahali kokote inakopatikana.
Mikoa ya Tanga, Njombe, Mtwara, Tabora, Mbeya, Bukoba na kwingine kwingi
kunastawi miti ya aina mbalimbali.
Kwa hakika wengi wameendelea kufanya hivyo kwani
wamekuwa wakinijulisha. Wapo makumi waliosafiri hadi hapa Iringa kujifunza na
kujionea fursa hii inavyowanufaisha na kuwatajirisha watu; kati yao wapo
walioamua kuanza kuwekeza na wapo ambao walirudi makwao ili kujipanga kwa ajili
ya kuwekeza wakati ujao.
Furaha yangu ilikuwa kubwa zaidi pale ambapo wapo
waliofika kujifunza hapa Iringa kasha wakaenda katika maeneo yao na kuanza
kuwekeza. Wapo mamia ambao walizungumza nami kwa simu kutoka maeneo mbalimbali
wakiwa wamevutiwa na habari zile.
Nami kwa moyo mkunjufu nilishirikishana nao uzoefu
wangu na kuwahamasisha waanze hata kama ni kidogo kidogo mahali popote
wanapoona inafaa. Ni jambo la kujivunia na la fahari kutamka kwamba makala ile
imekuwa na ‘impact’ kubwa mno kwa mamia ya watanzania ambao walihamasika kuanza
kuwekeza katika miti kule Tanga, Tabora, Mbeya, Mtwara, Morogoro na wengine
wengi hapa Iringa.
Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara katika
makala zangu; ni kwamba muda wa kulalamika lalamika umekwisha. Mazoea na utamaduni
wa watanzania wengi kudhani kwamba tunaonewa wakati wote haujatusaidia mpaka
hapa kwa jinsi hii hakuna sababu ya kuendelea nao.
Mtindo wa kuishi maisha ya kutaka kuhurumiwa
yanatupotezea muda wenye thamani. Tumekuwa tukilalamika kuwa wageni (wanaokuja
kwa jina la wawekezaji) wanatupora ardhi; lakini tusichokitafakari ni hiki,
“Mimi kama mtanzania kwa nafsi yangu na kwa uwezo wangu nimefanya nini cha
maana katika ardhi ninayoweza kuipata hapa nchini ama ninayomiliki?”.
Bahati nzuri ni kwamba idadi kubwa ya watanzania
tunafahamu kuwa ardhi ni utajiri; lakini hatufanyi juhudi za makusudi kuuvumbua
na kuutumia utajiri huo. Tunayo mamilioni ya hekta za ardhi zenye rutuba na
zinazofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali lakini bidii zetu hazijatosha hata
tufike mahali tuseme ardhi haitutoshi.
Itakumbukwa kuwa wakati nikiandika makala ile mwaka
jana pia nilizindua kampeni ya kimazingira niliyoibatiza jina la “Green The
World And Become Rich”. Kimsingi kampeni
hii nililenga kuwahamasisha watanzania washiriki kikamilifu katika utunzaji wa
mazingira na wakati huo huo wakitengeneza utajiri.
Unapochukua fedha yako na kuwekeza kwenye shamba la
miti moja kwa moja unakuwa umetunza mazingira kupitia miti uliyopanda lakini
pia usiku na mchana kadiri miti inavyoendelea kukua unakuwa ukitengeneza
mamilioni.
Na hii ni namna moja nzuri ambayo watanzania
tunaweza kuwekeza kwenye ardhi. Leo unapanda miti inakaa miaka saba ama kumi
unavuna halafu baada ya hapo ardhi yako unaitafutia matumizi mengine. Si hivyo
tu, lakini katika hiki hiki kilimo cha miti; ndani ya shamba lako unaweza
kufuga nyuki, ukawa unavuna asali hukuku ukisubiri kuvuna miti yako.
Msukumo wa kuanzisha kampeni hii ya “Green The World
And Become Rich” niliupata baada ya kutafakari nafasi walizonazo watu wengi
wenye nia ya kuwekeza katika kilimo cha miti na katika ardhi kwa ujumla. Nilifahamu
kuwa sio rahisi sana kwa mtu kutumia fedha zake na kupanda miti kwa faida moja
tu ya kutunza mazingira.
Nilijaribu kufikiri namna ya kuongeza thamani; hivyo
ilinibidi nifanye kazi ya kuwaelimisha watu mbalimbali mambo mengi kuhusu miti,
biashara yake na namna inavyolipa. Ninafahamu kuwa mamia ya wanaoendelea
kuwekeza kwenye miti sehemu mbalimbali Tanzania, kufuatia kampeni yangu;
wanawezekeza kwa mtazamo wa kupata faida kifedha huko mbeleni.
Hilo ni jema sana lakini wakati huo huo mimi na wadau
wengine wa mazingira tunashangilia kwa sababu mazingira yanaimarika huku watu
wakitajirika. Vile vile Nilitambua kuwa wengi wanaweza wasiwe na taarifa sahihi
kuhusu kilimo hiki, kwa maana ya maeneo kinakostawi, taratibu za upataji
maeneo, lakini kubwa kuliko yote ni namna ya usimamiaji pindi wakiwa mbali.
Nilifahamu mtu angeweza kujiuliza maswali mengi
yakiwemo; “Nitawezaje kumiliki shamba Tabora wakati mimi kikazi nipo
DaresSalaam?”, “Nitawezaje kufahamu biashara ya mbao, magogo, pindi ukifika
muda wa kuvuna?”, “ Mbali na faida nitajuaje gharama za uendeshaji na je
nitazimudu?”.
Katika kampeni hii kulikuwa na majibu yote ambao kwa
wale waliovutiwa kuwekeza Iringa katika maeneo inakowekeza kampuni yangu,
nilijitolea kuwapa usaidizi wa kuwatunzia na kuyahudumia mashamba yao. Fursa
bado zipo nyingi, watanzania wenzangu tusilale.
Ninapoandika makala haya leo ninatumia wasaa huu
kuwakumbusha wale jamaa zangu wa kule Tanga, Tabora, Mbeya na kwingine ambao
waliniahidi kuwa wataanza kuwekeza katika maeneo yao mwakani (yaani mwaka huu).
Msimu ndio umeanza, kuandaa mashamba, kuaandaa miche
na maandalizi mengine. Hapo hapo mlipo fanyeni kitu katika ardhi zenu, wekezeni
kwa manufaa yenu na ya watoto wenu, isaidieni dunia kwa kuboresha mazingira
yake.
Wale waliofika Iringa wengi wao nilikuwa ninawapa
zawadi ya nakala ya sheria ya ardhi ya mwaka 1999. Na wengine waliokuwa
wakiwasiliana nami nilikuwa ninawapa semina fupi kuhusu sheria ya ardhi.
Kiujumla sheria hii inatupendelea mno wazawa tofauti na malalamiko mengi ambayo
huwa ninayasikia.
Pengine Watanzania tuna tatizo katika ubunifu na
inapotokea wengine wamebuni tunakuwa wepesi wa kudhani wametuibia. Mathalani,
tunaishi na ardhi tusiyoifanyia kazi miaka nenda rudi, akitokea mwekezaji
akabuni mradi Fulani katika ardhi hiyo; tunaanza kuja juu! Hatujiulizi tulikuwa
wapi na kwa nini hatukuchangamkia?
Kingine kinachotumaliza Watanzania wengi ni ile
dhana ya kudhani kuwa kilimo ni utumwa, shamba tunaona ni kwa ajili ya waganga
njaa na waliokosa nafasi ya kupata ajira nzuri. Hii ni dhana mbaya na
inachangia sana watanzania kutokuwa na mikakati ya kuitumia ardhi kikamilifu.
Hata hivyo nikiri kuwa wapo watanzania ambao
wanatambua thamani ya ardhi na wanaitumia ardhi vizuri kwa uzalishaji na
uwekezaji wenye tija. Lakini idadi hiyo haitoshi ukilinganisha na idadi ya
wasiotambua nguvu na utajiri wa ardhi ambao wanaendelea kulalamika ugumu wa
maisha na waliopoteza tumaini.
Jambo jingine linalotumaliza watanzania ni kutokuwa
na maono ya muda mrefu. Wengi wetu tunataka mambo ya papo kwa papo, hatupendi
kuangalia mambo ya vipindi virefu mbele. Mfano mzuri ni katika hili la
uwekezaji katika ardhi.
Mtu anaona ni kupoteza fedha kununua shamba leo
ambalo pengine linaweza kuja kutumika miaka ishirini huko baadae. Mtu anaona ni
kama kupoteza fedha kupanda miti leo ambayo atakuja kuivuna miaka saba ama
miaka kumi ijayo.
Wasichokumbuka wengi ni kuwa unachopuuza kufanya leo
kwa gharama ndogo miaka ishirini ama kumi ijayo hutakuwa na uwezo wa kukifanya
hata kama ukitamani. Mzee wangu mmoja hapa Iringa alinisimulia namna
alivyopuuza kununua kiwanja kimoja hapa mjini Iringa mtaa wa Miyomboni mwaka
1994.
Wakati huo anasema kiwanja hicho kilikuwa kikiuzwa kwa
shilingi laki nne; lakini mwaka jana, 2012 kimeuzwa kwa milioni 320! Mzee wangu
huyu anasema mwaka huo 1994 laki nne kwake zilikuwa ni hela ndogo sana lakini
akapuuza. Leo hii miaka 20 baadae kiwanja kile kile kimeuzwa mara mia nane ya
bei aliyoipuuza ilhali yeye (mzee wangu huyu) leo hana hata ujanja wa kupata
milioni kumi!
Kwa maneno yake anasema, “Ningekuwa na mipango ya
muda mrefu katika kuwekeza kwenye viwanja, ardhi na mashamba, leo mimi
ningekuwa milionea hapa mjini” Anachofanya mzee wangu huyu ni utekelezaji wa
ule msemo, “Majuto ni mjukuu”!
Watanzania tusilale, ushindi wetu kiuchumi umo
ardhini!
stepwiseexpert@gmail.com
+255 719 127 901
No comments:
Post a Comment
Maoni yako