March 13, 2013

UCHUMI NA BIASHARA: "UCHUMI" NDIO LUGHA YA AFRIKA MASHARIKI

Albert Sanga, Iringa

Wiki mbili zilizopita nimekuwa nikiandika waraka wa kiuchumi kwa wafanyakazi. Kwa ujumla wake waraka huo utakuwa ni mrefu hadi sehemu ya kumi. Kutokana na urefu huo nimejipangia kutouleta kwa mfululizo wa wiki zinazofuatana. Badala yake nitakuwa nikiuleta kwa wiki tofauti tofauti mpaka uishapo mwaka huu.

Leo ninapenda tuperuzi nafasi ya uelewa wetu sisi watanzania linapokuja suala la uchumi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Unapotaja Afrika Mashariki ni kwamba kuna mambo ya msingi ambayo yanaushikilia uhusiano huu. Pamoja na mambo mengine nguzo kuu ya uwepo wa jumuiya hii ni suala la uchumi. Ndio maana tunaongelea soko la pamoja, kuunganisha sarafu zetu, kusafiri kwa mitaji pamoja na rasilimali watu.

Mambo mengine yanayojadiliwa na kushughulikiwa katika ushirikiano huu yanasaidia tu kuboresha lengo kuu la msingi; ambalo ni kuboresha uchumi wa ukanda huu. Kwa tafsiri ya mkato ni kuwa lugha ya Afrika Mashariki ni uchumi. Ili kunufaika na jumuiya hii ni lazima kuijua lugha hii, ni lazima kuyajua matendo ya kiuchumi, ni lazima kuelewa mwenendo wa kiuchumi na ni lazima kutambua nafasi ya mtu mmoja mmoja katika uchumi.

Wakinga tuna msemo mmoja usemao, “Kama wewe sio mchawi, hakikisha unamfahamu mganga mzuri”. Si lazima uwe mjuzi ama mtaalamu wa mambo ya uchumi na lugha za uchumi wa darasani ili kuijua lugha ya Afrika Mashariki; bali unaweza kujifunza na kujizoesha kutoka kwa ‘waganga’(wataalamu) na baadae nawe ukawa ‘mchawi’ (mtumiaji).

Je, watanzania tunaijua kwa kiasi gani lugha inayotumika Afrika Mashariki? Je, tunaelewa maana na matendo ya kufanya tunaposikia viashiria vya masoko ya hisa, masoko ya mitaji, sarafu ya pamoja, ushirikiano wa kodi na ushuru au tunapoambiwa mtiririko wa rasilimali watu? Kwa bahati mbaya sana ni kuwa kutojua lugha hizi hazitoi msamaha wa kuhurumiwa linapokuja suala la utekaji wa fursa zilizopo kwenye jumuiya hii.

Hebu tuangalie baadhi ya mifano michache ya lugha ya Afrika Mashariki. Unaposikia masoko ya mitaji na hisa kichwani kwako ni lazima kuje maneno kama DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) , USE (Uganda Stock Exchange) na NSE (Nairobi Securities Exchange). Haya ni masoko ambayo kunatokea ununuzi wa hisa na ubadilishanaji wa mitaji pale.

Hapo kuna makampuni ambayo yanapeleka sehemu yake kuwa miliki ya umma hivyo unaweza kununua ama kuuza sehemu za makampuni hayo. Kujua kuhusu DSE, NSE, na USE hakuhitaji mpaka uwe unamiliki hisa ama mtaji pale isipokua mwenendo wake unaathiri sana uchumi wa eneo hili na hivyo kuathiri ustawi wako binafsi kiuchumi.

Nikisema habari za hisa na mitaji mtu anaweza kudhani ninaongelea masuala ya kitaalamu sana. Kumbuka kua ninaongelea lugha ya Afrika Mashariki. Namna makampuni yanavyojiandikisha na kuuza mitaji kwenye masoko ya hisa na mitaji kunaonesha mtiririko na mwelekeo wa mitaji katika ukanda mzima.

Nasi tunajua kua ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai. Tai wanajuaje kua sehemu Fulani kuna mzoga? Jibu ni rahisi, wanatumia harufu kutambua. Je, unajuaje kua Uganda ama Rwanda kuna fursa za kuwekeza?

Ni kwa kuangalia mwenendo wa mitaji na hisa kama moja ya kiashiria kati ya vingi vilivyopo. Ubaya ni kwamba hata kama wewe usipoisikiliza harufu ya “mzoga wa uwekezaji” wenzako kutoka nchi zingine za Jumuiya wataisikiliza harufu iliyopo hapa Tanzania nao watakusanyika.

Ninapoongelea habari za DSE, USE na NSE naelewa kuwa si rahisi sana kwa wengi kuelewa fursa zilizopo ndani yake pengine kutokana na historia ya uchumi na mazoea yetu. Wenzetu Kenye NSE ilianza (japo sio rasmi) mwaka 1954 wakati sisi DSE ilianza mwaka 1996.

Wanzetu wana uzoefu mkubwa na lugha hii wameizoea kwa kiasi kikubwa. Pale NSE makampuni yaliyojiandikisha ni zaidi ya 50 wakati hapa kwetu DSE kuna makampuni pungufu ya 20 tena mengine yakiwa ni yale yale ya kule Kenya (Cross listing).

Kwa upande wa Uganda hawana tofauti na sisi kwa maana ya kuanza, kwa ni USE ilianza 1997 lakini spidi yao ya kuijua lugha hii ni kubwa mno. Mwaka 2010 USE ilikua ni kinara wa masoko yote ya hisa Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutumia kipimo cha ALSI (All Shares Index) ikiwa na mrejesho wa faida ya asilimia 74% kwa hisa zinazonunuliwa na kuuzwa.

Sina lengo la kukupitisha porini katika takwimu za kitaalamu lakini kuna kitu nataka tujifunze; Kenya walitangulia miaka mingi, Uganda ni wapya kama sisi lakini wanajifunza kwa kasi ya jabu. Wenzetu walishatangulia na wengine wanakimbia lakini sisi tunazinduka polepole mno.

Nikiri wazi kuwa mambo kama haya ya hisa na mitaji kiasili yaliibuka kutokana na ubepari, lakini kwa kua tumeamua “kuchanganyika” hatuna ujanja zaidi ya kuungana nao. Kumbuka kua, “Kama wewe sio mchawi hakikisha unawajua waganga wazuri”, hatuna ujanja inatakiwa tujifunze na kuizoelea lugha hii ili tuweze kuelewana na wenzetu wa hapa ‘Jumuiyani’

Katika robo ya mwaka jana makampuni mengi ya umma na binafsi katika nchi zote tano za Afrika Mashariki yameendelea kutoa ripoti zao za kifedha na kiutendaji kwa mwaka ulioishia Desemba, 2012. Hapa napo tunaweza kuitathmini hali yetu tuliyonayo katika lugha ya Afrika Mashariki kwa kuangalia namna tunavyozipokea ripoti hizo.

Nianze na namna jirani zetu Kenya wanavyozipokea ripoti hizo. Wakati makampuni 20 makubwa (yaliyopo kwenye 20 Shares Index) yakiachia ripoti zao nchini Kenya; kulikua na  gumzo mitaani kila mmoja akihaha kuzifuatilia, kuzisoma na kuzitafsiri. Wanahisa na wasio wanahisa wanataka kujua kampuni gani imefanya vipi, ipi imeizidi ipi, ipi ina fursa na gawio zuri kwa kuwekeza, ipi ina mikakati gani ya muda ujao na mengine mengi.

Gazeti moja la nchini Kenye lilipiga picha inayoonesha watoto wa sekondari katika mji wa Naivasha wakisoma ripoti ya mojawapo ya benki za biashara nchini Kenya. Walipoulizwa watoto hao mmoja wao alijibu hivi, “Mama ana hisa kwenye benki hii nataka nijue mwenendo wake”. Hapo ni Kenya!hadi watoto wa shule za sekondari wanaongea lugha ya Afrika Mashariki!

Hali ni tete kwa Tanzania kwa sababu ripoti za makampuni ya ndani ama ya wawekezaji huwa hazipokelewi kwa hamasa yeyote. Kwanza ni wachache ambao wanafuatilia ripoti hizo na achilia mbali uwezo wa kutafsiri maana na athari za ripoti hizo kwa Afrika Mashariki na watu wake.

Kule Rwanda na Burundi wenzetu ndio kwanza wanajenga upya nchi zao; hivyo sio rahisi sana kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu hisia zao katika lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; lakini kiu yao ya kuinuka kiuchumi na kijamii inaonesha namna ambavyo wanaweza kutupita.

Unaposoma ripoti za makampuni haya (Financial Statements) kuna ishara zinatoa ikiwemo, “Nenda katafute ajira sehemu fulani”, “Nenda kawekeze kitu fulani mahali fulani”, “Ondoka mahali fulani kwa sababu pameharibika”. nakadhalika. Kwa kutozijua lugha hizi tunabaki tumeduwaa tusijue cha kufanya wala kwa kuelekea. Kwa kua wenzetu wanaelewa lugha na matendo ya Ki-Afrika Mashariki ni rahisi na itaendelea kuwawea rahisi kunufaika na lugha hii.

Tatizo letu watanzania wengi tunatumia malalamishi kama silaha ya kujiokoa na hatari za Afrika Mashariki. Juhudi zetu katika kuteka fursa za jumuiya hii zimeota matege na tumekua na mtazamo mdogo mno kuhusu mambo tunayotakiwa kufanya.

Kwa mfano; kitendo cha kukazana kujifunza Kiingereza ama kukazana kununua ardhi kwa ajili ya fursa za Afrika Mashariki sio kibaya lakini ni mtazamo mdogo sana. Tukiijua lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; tutaona na kuoneshwa mambo mengi sana yatupasayo ndani ya Jumuiya hii.

Kwa leo nikomee hapa, lakini natarajia kuendelea na chambuzi mbalimbali kuhusu biashara, ujasiriamali na uchumi katika mtazamo wa ki-Afrika Mashariki huko mbeleni.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi Afrika Mashariki!2 comments:

 1. Hi there I am so grateful I found your webpage, I really found you by mistake, while I was looking on Digg for something
  else, Regardless I am here now and would just like to say thanks for a incredible
  post and a all round enjoyable blog (I also love the theme/design), I don’t
  have time to read through it all at the minute but I have book-marked it and also added in your
  RSS feeds, so when I have time I will be back to read more,
  Please do keep up the great b.

  Feel free to visit my web page :: 49701

  ReplyDelete
 2. What you posted made a bunch of sense. However, consider
  this, suppose you were to write a awesome headline?
  I mean, I don't want to tell you how to run your website, however suppose you added something that grabbed a person's attention?
  I mean "UCHUMI NA BIASHARA: "UCHUMI" NDIO LUGHA YA AFRIKA MASHARIKI" is a
  little plain. You could look at Yahoo's home page and watch how they write post titles to get viewers interested. You might try adding a video or a related picture or two to grab people excited about what you've got to say.
  In my opinion, it might make your website a
  little livelier.

  Stop by my web site: 88119

  ReplyDelete

Maoni yako