Albert Sanga, Iringa |
Nimekua
nikiandika makala za hamasa kuhusu ujasiriamali ikiwa ni hatua ya kukabiliana
na mabadiliko ya kiuchumi ambapo kuna upungufu mkubwa wa ajira, lakini pia kuna
mfumuko wa gharama za maisha kiasi kwamba hata walioajiriwa wanapata wakati
mgumu kumudu vema maisha ya kila siku.
Moja
ya swali ambalo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara ni hili, “Sanga unataka kila
mtu awe mjasiriamali?” Jibu langu katika swali hilo limekuwa ni hili siku zote:
“Ndio, natamani kila mtanzania awe mjasiriamali”.
Nafikiri
ipo haja tuangalie kinagaubaga dhana hii ya ujasiriamali kwa mtazamo mpana.
Ujasiriamali umegawanyika katika makundi mawili. Mosi ni ujasiriamali wa
kibiashara (entrepreneurship) na pili ni ujasiriamali wa kikazi
(intrepreneurship). Kundi
la kwa linahusisha wajasiriamali waliojiajiri na kundi la pili linahusisha
wajasiriamali walioajiriwa. Wajasiriamali walioajiriwa wanaitwa “Wajasiriakazi”
na wajasiriamali waliojiajiri walipaswa kuitwa “Wajasiriabiashara”.
Wataalamu
wa Kiswahili itabidi waliweke sawa hili kwa sababu neno “Ujasiriamali”
linatumika kiupendeleo kwa kuwalenga wale tu waliojiajiri wakati linatakiwa
kuyafaa makundi yote mawili. Nadhani sasa utaelewa ni kwa nini ninasema
natamani kila mtanzania awe mjasiriamali. Leo katika makala haya nitajikita
kueleza dhana ya ujasiriamali kazini. Hivyo
basi kila ninapohamasisha watu kuwa wajasiriamali, haimaanishi huwa ninawananga
wale walioajiriwa, la hasha! Mtu yeyote aliye mweledi wa uchumi na kiimani anafahamu
umuhimu wa kila mtu kusimama katika nafasi yake kutimiza kusudi la taifa na
kusudi la Mungu. Hakuna aliye bora zaidi ya mwenzake; aliyeajiriwa ama
aliyejiajiri, mfanyakazi ama mwajiri, wote wana umuhimu sawa.
Kwa
sababu hakuna ujasiriamali kama hakutakua na watendakazi. Kwa hiyo waajiri
(wajasiriamali wa kibiashara) wanahitajika kwa wingi na wafanyakazi
(wajasiriamali wa kikazi) wanahitajika pia. Kwa maana hii taifa linahitaji
kuwapata wafanyakazi ambao watawiana na ndoto za taifa na wajasiriamali katika
kujenga uchumi na kuleta maisha bora. Miaka
ya karibuni dhana ya ujasiriakazi imekuwa ikipata umaarufu mkubwa, ingawa ni
watu wachache ambao wanaielewa vema dhana hii. Watafiti wengi wanakubaliana
kuwa dhana ya ujasiriakazi ni jamii ya dhana ya ujasiriamali(entrepreneurship)
lakini hii ikiwa inafanyika ndani ya taasisi, makampuni, na serikalini
ikihusisha “usimamizi wa rasilimali kiubunifu”.
Dhana
ya ujasiriakazi inaonesha kuwa ilijitokeza na kushika kasi duniani miaka
takribani thelathini iliyopita. Ujasiriakazi unahusisha uundaji, uendelezaji na
utekelezaji wa mawazo na tabia mpya katika maeneo ya kazi. Ubunifu unaweza
kuhusisha kubuni bidhaa mpya ama huduma, kubuni mfumo mpya wa utawala ama
mpango mpya ama mikakati inayohusiana na wafanyakazi katika eneo husika. Wajasiriakazi
ni watu ambao si lazima wawe wagunduzi wa bidhaa ama huduma mpya isipokuwa ni
watu ambao wanabadilisha mawazo ama fikra kwenda kwenye uhalisia wenye faida.
Ni watu ambao ukiona huduma ama bidhaa basi ujue kuwa wapo nyuma yake.
Ni
watu ambao huunda timu za kiutendaji ili kuhakikisha kuwa wanafanya juhudi
kushughulikia mawazo yao kuwa katika uhalisia. Wajasiriakazi si lazima wawe
watu wenye uwezo wa juu sana kiakili (geniuses), lakini ni watu wa upeo wa
kawaida kiakili. Kwa
mtazamo huu tunaona kuwa dhana ya ujasiriakazi inajikita zaidi katika kutoa
msukumo mpya na kuwezesha maeneo ya kazi kuwa na ubunifu na njia mbadala za
kutekeleza majukumu yake. Muunganiko wa wafanyakazi katika maeneo husika
yanapelekea kutengenezwa kwa sura mpya ya taasisi, ama kampuni ama kitengo cha
serikali.
Wafanyakazi
wajasiriakazi ni wale wanaohitaji uhuru na urahisi wa kutumia rasilimali za
maeneo yao ya kazi, wenye hamasa kutoka ndani (self motivated) na wanaoguswa
kwa mafanikio chanya ya maeneo yao ya kazi. Mara nyingi hawa huwa wana ujuzi na
maarifa mazuri ya kurasimisha madaraka, wanajiamini, wanafanya utafiti wa
kimasoko na kihuduma, hawaogopi kufukuzwa makazini na wanajikita katika
kuthamini uwepo wa wateja ama watu wanaowahudumia.
Kiujumla
mahitaji ya dhana ya ujasiriakazi yanajikita katika kuibuka kwa mambo
yafuatayo. Uwepo wa makampuni mengi ya kibiashara yanayoshindana kwa mbinu za
kisasa pamoja na watu kupoteza imani na mifumo iliyozoeleka na kikiritimba ya
kiutawala na kiuongozi katika taasisi mbalimbali (binafsi na serikalini). Vile
vile ujasiriakazi unapata mashiko kutokana na kuibuka kwa watu wenye akili na
uwezo mkubwa ambao wanaanzisha makampuni kwa kutumia mbinu zilizoibwa kutoka
makampuni makongwe. Lakini kubwa kuliko yote ni kiu ya watu kuona kuwa kila
eneo la biashara ama huduma linakuwa na ufanisi.
Mfumo
wa dunia wa sasa unalazimisha kutekelezwa kwa vitendo dhana ya ujasiriakazi
katika maeneo mbalimbali kutokana na sababu mbalimbali. Kwa upande wa makampuni
ya kibiashara, inaonekana kuwa ushindani wa kibiashara kwa sasa umekuwa ni
mkubwa na uliotete mno kiasi ambacho kila mfanyakazi anahitajika kuwa mbunifu
kwa ajili ya kuyasaidia makampuni husika.
Viongozi
wa kisiasa nao wanajikuta katika mbinyo wa kutimiliza dhana hii ya ujasiriakazi
katika mifumo wanayoiongoza, kutokana na matakwa ya wapiga kura wao. Wananchi
katika miaka ya sasa ambayo inaongozwa na mageuzi ya utandawazi wamekuwa makini
mno katika kubaini mahitaji yao halisi. Wapo makini sana na ahadi wanazopewa na
viongozi wao, wapo makini na muda, na wapo makini sana na mienendo ya
kiutekelezaji wa ahadi mbalimbali zinazotolewa.
Miaka
ya sasa wananchi wamechoshwa na ukiritimba uliokuwa kama utamaduni katika ofisi
mbalimbali za serikali. Mtindo wa mtu kufuatilia faili mwezi mzima kisa
anashinikizwa kutoa rushwa “kiaina” umewachosha sana wananchi. Wengi wa
wananchi wamebahatika kupata elimu, wanawasiliana na dunia, wanajifunza huko
kwingine mambo yanaendaje, wanahoji, wanataka kujua kwa nini huku kwetu mambo
yawe hivi?
Ni
jambo lililo dhahiri kabisa kuwa kutekelezwa kwa dhana hii ya ujasiriakazi
katika maeneo mengi (hasa ya serikali) kunaweza kuleta shida na kuchukua muda
mrefu sana kukamilika. Hata hivyo wadau wa maeneo ya kazi ni vema wakaungana na
mtaalamu katika masuala ya ubunifu wa kijasiriakazi, James Brian Quinn, ambaye
alibaini vigezo vifuatavyo katika kuwawezesha wafanyakazi kuwa wabunifu katika
maeneo ya kazi.
Anataja
vigezo hivyo kuwa ni mazingira mazuri ya kufanyia kazi na maono, mtazamo katika
masoko yanayohudumiwa na mwisho ni muundo wa taasisi husika. Quinn anasema kuwa
makampuni na taasisi zilizofanikiwa zimekuwa na maono kamili na
yanayotekelezeka kwa huduma na bidhaa wanazozalisha, wanatengeneza na kutoa
huduma kwa kuzingatia mahitaji kamili ya mteja. Kigezo
kingine ni kuwa na mibadala mingi katika kushughulikia mambo yahusianayo na
majukumu yao. Kwa mfano, kitengo cha elimu katika wilaya ama mkoa kinaweza kuwa
na mkakati wa kutatua tatizo la upungufu wa walimu na uhaba wa madarasa.
Ikiwa
afisa elimu wa ngazi husika atakuwa ni mjasiriakazi atahakikisha kuwa anakuwa
na njia zaidi ya moja kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinatatulika kwa ukubwa.
Mbali na pengine kusubiri kuletewa tu fungu kutoka serikalini atakuwa na plan B
na C ya ama kuitisha harambee ama kutafuta ufadhili. Huyu ndio mjasiriakazi
kazini.
Yapo
mambo ya msingi ambayo yanapaswa kufanywa katika maeneo ya kazi ili kufanikisha
kusimika ujasiriakazi. Mambo hayo ni kujiwekea malengo ambayo ni lazima
yajadiliwe na kukubalika na wafanyakzi wote pamoja na viongozi wao. Kuwepo na
mfumo unaoelekeza na kushughulikia mirejesho ili wajasiriakazi wajisikie
kutambulika na kuthaminiwa.
Jambo
jingine ni kwa viongozi wa maeneo ya kazi kuhakikisha wanasisitiza kuwepo kwa
majukumu ya mtu mmoja mmoja. Mara nyingi kutoa majukumu kiujumla huwa
kunapunguza uwajibikaji kwa sababu kila mmoja anahisi hahusiki moja kwa moja.
Ili kuinua ari na hamasa ya wajasiriakazi kufanya kazi kwa bidii ni lazima
kutoa zawadi na tuzo kulingana na ufanisi wa kazi.
0719 127 901,
stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Maoni yako