March 26, 2018

SIMBA, YANGA WANAIMBA KIMUNGU WANACHEZA KISHETANI.

Na. HONORIUS MPANGALA 
Nilikuwa nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo April 4, 2015 siku ya pasaka. Kulikuwa na mchezo wa wa mtoano kuelekea kwenye makundi klabu bingwa Afrika kati ya Tp Mazembe wenyeji dhidi ya Orlando Pirates. Mitaani kila uliyemwona alikuwa amevalia jezi ya Mazembe na akizungumza kuhusu Mazembe huku wakielekea uwanjani Estadio de Mazembe. 

Nilimuuliza mlinzi wa eneo nilioenda kuhusu mashabiki FC Lupopo hawawezi kwenda uwanjani? Akanijibu hata Mimi ni Lupopo lakini inapokuja uwakilishi wote tunakuwa wamoja. Akanieleza hata uwanjani huioni jezi ya Lupopo. Mechi ile ilimalizika kwa TP kupata matokeo ya goli tatu kwa moja yaliyofungwa na Ranford Kalaba,Mbwana Samata na Rogers Asale. 
SIMBA

Nilikaa na mlinzi yule tukisikiliza matangazo ya redio kwa lugha ya kifaransa naye alinitafsiria kwa kiswahili cha kikongo. Wakati magoli yote yanaingia katika lango la Orlando alikuwa akisimama na kushangilia. Huo ndio utofauti wetu na wao inapokuja suala la michuano ya kimataifa.
Sababu ya pili ambayo inapelekea timu zetu za kitanzania kuwa na wakati mgumu ni kwa upande wa wachezaji. Upande Huu unatokana na ile hali ambayo wachezaji wanaichukulia katika mchezo. Huweza kuingia uwanjani wakiwa wamejiamini sana lakini ni kelele za dakika chache toka kwa mashabiki wanao wafahamu zitawafanya wachanganyikiwe.

Maisha ya wachezaji wa kitanzania yako kawaida sio jambo geni kumwona mchezaji yuko mtaani akiwa amekaa na jamaa zake ambao ni marafiki. Sasa ikitokea marafiki wako uwanjani wanamtazama jamaa yao ,itatokea mchezaji hata taka kukosea achezapo. Lakini kama zitasikika sauti toka kwa anaowafahamu itazidi kumchanganya na kumfanya apotee kabisa katika mchezo.

Simon Msuva baada kurejea katika timu ya taifa alikiri ameshangazwa na ushangiliaji wa mashabiki wa Morocco. Akasema wana ushangiliaji tofauti kulingana na hali ya mchezo. 

Kama wanataka kusawazisha bao watakuwa na aina yao ya kushangilia au kama watahitaji matokeo watakuwa na ushangiliaji wao na hata kama timu inaongoza kwa magoli na muda unayoyoma wataimba na kushangilia kwa aina yake kama kuwatia hamasa ya kutopoteza mchezo.

Hili lilimshangaza sana kwani alizoea kutazama hapa Nyumbani kama Yanga ikicheza na Mbeya City basi mashabiki wa Simba watakuwa Mbeya City na kama watakuwa wanacheza nchini ya kiwango wataishia kuzomewa sana. Yeye ni mwathirika wa kuzomewa na mashabiki wake wakati anachezea Yanga ndio maana alilishangaa hili huko Morocco.

Mara kadhaa baada ya Yanga kucheza hatua ya makundi katika michuano ya shirikisho mwaka 2016 walikiwa na malalamiko kuwa TFF haiwasaidii katika michuano ya kimataifa. Hili limefanya kuwashangaza hata klabu ya Simba kule Misri walipoona ushiriki wa viongozo wa chama cha Soka cha Misri wakati wanaenda kupambana na wapinzani wao wa El Masry.

Msimu wa uliopita wakati Yanga walipangwa na Zanaco ilikuwa kama wangeitoa klabu hiyo ya Zambia. Ingefanya idadi ya uwakilishi kwa msimu huu iongezeke moja baada ya kuonekana maendeleo mazuri ya klabu hiyo kwani wangeingia katika makundi misimu miwili mfululizo katika mashindano mawili yaani michuano ya shirikisho na ile ya shirikisho.

YANGA
Nadir Haroub Ally 'Cannavaro' alipohojiwa baada ya mchezo dhidi ya Township Rollers alisema hizi mechi zinawahitaji kutumia vyema uwanja wa nyumbani. Timu inahitajika kupata matokeo mazuri ikiwa nyumbani kwani kutegemea ugenini ni kitu ambacho ni kigumu sana. 

Wakiwa Angola mwaka 2016 walikutana na manyanyaso ya akili toka kwa watu wa ulinzi na usalama nchini Angola. Na nyakati zote ukiona mambo yasiyokuwa ya kimchezo yakafanyika basi ujue hata wasimamizi wa mchezo husika ni kama wanakuwa wamepangwa kuto toa ripoti itakayo waingiza matatani. 

Wenyeji wa Yanga baada ya kufungwa magoli mawili Tanzania wakafanikiwa kupata ushindi wa goli moja wakiwa Angola. Lakini matukio ya ndani mchezo yalisababisha kupatikana kwa penati ambayo haikutarajiwa kulingana na mzingira yake. Lakini bahati ikawa kwao golikipa aliipangua. 

Kabla ya kupigwa penati hiyo wachezaji wa Yanga walimzonga mwamuzi hali iliyopelekea Askari kuingia na virungu uwanja na kutaka kutumia nguvu kutuliza ile hali.

Sasa Cannavaro anaposema huko ugenini kuna changamoto basi tumwelewe katika mazingira hayo. Watanzani hatujawa watu wa mipango mipango ili kufanikisha timu zetu kupata matokea katika michuano ya kimataifa. Hali hii imekuwa tofauti tunapoenda ugenini.

Moja vitu ambavyo Ismail Aden Rage hataki kuvikumbuka ni marudiano ya mchezo kati DC Motema Pembe ya DRC na Simba ya Tanzania. Mchezo ambao ulimfanya asitamani kwenda tena katika jiji la Kinshasa kwa Yale manyanyaso ya akili na mwili waliyokutana nayo. 

Ni katika mechi hii ambapo mwandishi mmoja wa kike kutoka Tanzania alifanyiwa vitendo vya unyanyasaji na mashabiki wa DC Motema Pembe. Licha ya uwepo wa watu wa usalama lakini mwandishi yule alichokutana nacho alipofuatwa na mashabiki hao anajua yeye na Mungu wake. 

Wakongo wa klabu hiyo waliamini kuwa wapinzani wao katika soka la Kongo klabu ya AS Vita wamewapa 'dumba' Simba ili wawafunge, sasa janga likamkuta mwandshi yule akiwa ameenda kujisaidia. Inasikitisha.

Kama hatutaki kuamini kuwa mchawi namba moja ni sisi wenyewe katika kuendekeza mambo ya kipuuzi timu zinapokuwa zinawakilisha nchi basi tukubali kuumia milele. Kama pia viongozi hawatatambua na kutoa elimu kwa mashabiki kuwa michuano ya kimataifa ndiyo inayoweza kutuongezea idadi ya timu kushiriki basi tumsubili yesu kuja kutujuza.

Kama tutashindwa kutambua umuhimu wa kuto waingiza wachezaji wetu matatani wawapo katika kuwajibika. Basi tumsuli mtume aje kutushika msikio na kutuambia wapi tunakosea. Maana katika mtazamo wa kawaida tunashindwa kutambua umuhimu wa vipaumbele vya soka letu ili liweze kujualikana kimataifa na hatimaye kuja kuwa kitalu kizuri cha kuuza wachezaji.
0628994409

No comments:

Post a Comment

Maoni yako