NA MARKUS MPANGALA
MIAKA kadhaa iliyopita nilishindwa kuwaelewa kabisa watendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) hapa nchini. Nilikuwa siwaelewi kwa sababu siku moja niliwahushudia wafanyabiashara fulani kutoka Songea mkoani Ruvuma, wakizunguka vyumba vya ofisi vya taasisi hiyo kwenye jengo la Ushirika liliko Barabara ya Lumumba, Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kwa madhumuni ya kusajili kampuni yao.
MIAKA kadhaa iliyopita nilishindwa kuwaelewa kabisa watendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) hapa nchini. Nilikuwa siwaelewi kwa sababu siku moja niliwahushudia wafanyabiashara fulani kutoka Songea mkoani Ruvuma, wakizunguka vyumba vya ofisi vya taasisi hiyo kwenye jengo la Ushirika liliko Barabara ya Lumumba, Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kwa madhumuni ya kusajili kampuni yao.
Jenista Mhagama |
Pili,niliwahi kumsaidia rafiki
yangu, Albert Nyaluke Sanga, ambaye ni mfanyabiashara mkubwa mkoani Iringa, ili
apate leseni ya biashara. Haikuwa leseni yake binafsi, bali aliamua kumsaidia
kijana mmoja aliyekuwa na ndoto za kuwa mfanyabiashara, lakini alikosa pa
kunzia.
Rafiki yangu huyo anapenda
kuwasaidia vijana wanaojishughulisha na ujasiriamali kwa sababu anaamini hiyo
ndiyo njia pekee ya kuwakomboa, badala ya elimu yao na kuondokana na matembezi
ya kusambaza bahasha za kuomba nafasi za kazi.
Tangu kuzaliwa kwake hadi leo,
akiwa kwenye umri wa utu uzima, hajawahi kuajiriwa kokote, kwahiyo anahimiza
vijana wamtumie kuwasaidia ushauri.
Wakati tukishughulikia hilo,
ndipo nilijiuliza swali ni kwa vipi taasisi kubwa kama BRELA inaendesha mambo
katika njia za kizamani ambazo zinasababisha gharama kubwa na kutoharakisha
upatiakaji wa huduma?
Kwamba mfanyabiashara
alilazimika kufunga safari kutoka Songea hadi Dar es salaam kushughulikia
usajili wa kampuni. Baada ya miaka hiyo, angalau sasa utendaji wa mamlaka hiyo
umebadilika licha ya kasoro za hapa pale ambazo ninaamini zitabadilika siku za
usoni.
Angalau sasa unaweza kujisajili
kupitia ofisi zao zilizoko mikoani, kwa njia ya mtandao au kufanya huduma za
malipo ya usajili kwa maelekezo yaliyoko katika tovuti yake. Kitu kimoja ambacho ninapenda
kuyaambia mashirika ya umma, ni kwamba bado yana mwendo wa kobe katika matumizi
ya tovuti, pamoja na mitandao ya kijamii. Mara kadhaa nimekuwa nikijiuliza hilo
bila majibu.
Angalau nimewahi kuwasilisha na
mashirika kadhaa yenye kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii, lakini
nilichowaambia ni kusisitiza matumizi sahihi ya kurasa hizo kwa madhumuni ya
kutoa taarifa, sio kuanzisha kama fasheni.
Kama tunatoa takwimu, basi
tuhakikishe tunawafikia wengi kwa kuwa kundi kubwa linahamia kwenye ulimwengu
wa digitali. Hilo ni lazima, tutake, tusitake
zama zimebadilika na waendeshaji wa mashirika hayo watalazimishwa na
wakati.
Hivyo basi, kwa kuwa BRELA
wamefanya mabadiliko hakika ninawapongeza. Hatuanzishi mashirika ya umma ili
yawe kikwazo kwa Watanzania badala yake yatoe mwongozo, ushirikiano na huduma
madhubuti kwa watanzania.Baada ya hayo, tugeukie upande
wa Sekretarieti ya Ajira hapa nchini. Hapo ndipo palipojaa mambo ya kushangaza.
Bado Sekretarieti inaendesha mambo yake kizamani sana.
Pengine naweza kusema zile zama
za kutumia kompyuta zilizokuwa kubwa kama makabati ya nguo, wakati tunaishi
kwenye zama za kasi za mitandao na kusogeza huduma kwa wahitaji. Nimeona kasoro nyingi kwa
Sekretarieti ya Ajira inapowaita kwa usaili waombaji wa nafasi za kazi. Kwa mfano
ni jambo la kushangaza Sekretarieti ya Ajira inapowatangazia vijana wa
Kitanzania nafasi za kazi, kisha inataka wote waje Dar es salaam kufanya usaili
na mitihani.
Mtanzania aliyeko wilayani
Nanyumbu mkoani Mtwara, au aliyeko wilayani Karagwe, mkoani Kagera
analazimishwa kusafiri kutoka huko hadi Dar es salaam kuhudhuria usaili wa
Sekretarieti ya Ajira.Huu ni utaratibu wa kizamani
sana, nadhani ulifanyika katika zama za kati za awe (Middle Stone Age) yaani
miaka 25,000 iliyopita, enzi za Homo Sapiens.
Sekretarieti ya Ajira inao
uwezo wa kuwa na matawi yake katika mikoa yote. Serikali inayo majengo mengi
ambayo yangeweza kutumika kuendesha shughuli za sekretarieti hiyo, kuliko
kuwakamua vijana wa Kitanzania kiasi kikubwa cha fedha huku wakikosa kazi hiyo
huambulia hasara tu.
Mathalani, wangeweza kuwa na
matawi katika Kanda ili kurahisisha utoaji wao wa huduma. Kanda ya Kaskazini,
Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Mashariki na Zanzibar. Uwezekano wa kuendesha zoezi la
usaili na mitihani kwa ajili ya kuchuja waombaji wa ajira, linafanyika katika
Kanda husika. Hatua hiyo itapunguza umaskini na kuwapa ahueni vijana
tunaotafuta ajira serikalini.
Kwa mfano, waombaji ambao ni
vijana na hawajapata ajira, wanatakiwa kupanda mabasi kutoka Bukoba hadi Dar es
Salaam kwa gharama ya shilingi 62,000 kwa safari moja. Anatakiwa alale Dodoma
ndipo afike eneo la usaili kufanya mitihani yake. Ukiongeza ghamara ya safari
ya kurudi alikotoka, ina maana analipia 62,000 tena, ikiwa na maana 124,000 bila
kula, kunywa wala kulala!
Vijana hao hao wanatakiwa
kurudi tena Bukoba au Nanyumbu kwa gharama kubwa zaidi wakati Sekretarieti ya
Ajira ingeweza kuepusha gharama na usumbufu kama huo. Tumeona watu takribani
56,000 wanagombea nafasi 400 za kazi zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato nchini
(TRA). Wametoka kila upande wa nchi hii, na kwa gharama kubwa, lakini mwisho wa
siku wameambulia dhiki na shida tu.
Mtu anatumia shilingi 46,000
kwa safari moja kutoka Songea hadi Dar es salaam. Akimaliza kufanya usaili,
anatakiwa kulipia tena shilingi 46,000 kurejea Songea. Hapo hatujahesabu
gharama za chakula na malazi, ambayo kwa hesabu ya haraka haraka ni shilingi
200,000. Hivi Sekretarieti ya Ajira haiwezi kuepusha umasikini zaidi unaowakaba
waombaji hawa?
Nafikiri wakuu wa Sekretarieti
ya Ajira wanapaswa kukubaliana nami kuwa wanaendesha mambo kizamani sana. Jambo
ambalo linachangia vikwazo visivyo na sababu, pamoja na ukosefu wa ufanisi.
Tatizo letu tunapenda sana kuona watu wanashindwa, badala ya kufanikiwa. Hizi
ni fikra zilikuwapo enzi za Ujima na ukabaila (Primitive Communalism na
Feudalism) na sio nyakati hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kusema hivyo sina maana ya
kuwatetea waombaji pekee, bali hata watendaji wa Sekretarieti wanatakiwa
kufahamu majukumu yao yamebaki Dar es salaam pekee, kwani ukiritimba na
utendaji wa zama za mawe ambazo zinarudisha nyuma ufanisi wao.
Nafikiri katika karne ya 21,
hatupaswi kujenga taifa la kutegemea huduma kutoka makao makuu pekee. Ni lazima
tutoe huduma zetu karibu na wananchi. Tunahitaji kusogeza huduma kwa wananchi,
sio kila kitu hadi kifanyike Dar es salaam tu.
Ni lazima Sekretarieti ya Ajira
wamsaidie Rais John Magufuli katika kupambana na umaskini, pamoja na ukosefu wa
ajira. Haiwezekani Serikali ikatangaza nafasi za kazi 50,000, halafu ikataka
waombaji wote wafunge safari kwenda kufanya usaili Dar es salaam.
Siamini kuwa Sekretarieti ya
Ajira haiwezi kuwa na wasimamizi watatu wa usaili na mitihani katika mkoa wa
Mwanza kuliko watu 40 maskini wasio na ajira kusafiri hadi Dar es Salaam
kufanya mitihani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako