October 17, 2017

MAONI YA MHARIRI: KWA WILAYA YA NYASA DUNIA HAIJABADILIKA?

Majuzi nimeona picha ya mwanadada mashuhuri katika mtandao wa Instagram, Mange Kimambi akionyesha majengo ya hospitali ya Lumeme wilayani Nyasa ikiwa na mazingira mabaya ya kufanyia kazi na ukosefu wa huduma muhumu. Pamoja na jengo lenyewe kutokamilika, lakini limekuwa likitumika hivyo hivyo.

Kwangu mimi ile ilikuwa habari kubwa sana kwa wilaya yetu ya Nyasa. Kama mwanahabari naamini kuripotiwa matukio au masuala yasiyofaa  ndani ya jamii ambayo haitoi habari za kutosha ni njia mojawapo kubwa ya kubadili mwenendo.

HAPA CHINI kuna Blogu ya JIMBO LA NYASA. Lakini habari za Jimbo husika ziliwekwa mara ya mwisho Januari mwaka huu. Nimejiuliza wasaidizi wa Mbunge wanafanya nini kama hawawezi kutoa taarifa za ofisi ya mbunge? Najiuliza hivi hatuoni umuhimu wa habari zetu zikiwa hadharani bila kujali mbaya au nzuri?

Je waanzilishi wa blogu ya JIMBO walikusudia tamasha au nini? BONYEZA HAPA KUTAZAMA.  Kimsingi habari za Jimbo la Nyasa ni lazima zitolewe wala kwa wananchi. Pili inadhihirisha "kuamini" kuwa NYASA ni ileile ambayo inaishi pasipo kuwa na habari zozote. Mtazamo huo si sahihi ndio maana wahusika wanaona "bora liende tu" huku wakisahau na kushindwa "KUMUUZA" mbunge. 

Nimejiuliza hadi leo hata kutengeneza ukurasa wa habari za mbunge kwenye mitandao hatuwezi kweli?  Hivi mahusiano ya mbunge na wapigakura wake yana maana gani? Naandika hapa kwasababu naamini wapo wahusika wanaofikisha ujumbe. Ningependa kuwakumbusheni kuwa "kutomuuza mbunge" katika ulimwengu wa kidigitali ni uzembe. Labda tunaweza kutembelea wananchi kila kona ya jimbo, lakini tunapawa kuelewa kuwa taarifa za huko ziwekwe sehemu maalumu kutunza kumbukumbu sio mambo ya "MASJALA" tena (hizo ni zama za kale mawe).

Kwa heshima nawakumbusha wasaidizi wa mbunge, kutoitendea haki blogu, kutozungumzia hata utalii ambao ni chachu ya kukuza mzunguko wa fedha wilayani kwetu ni UDHAIFU unaopaswa kurekebishwa.
Ninawatakieni majukumu mema. 
HABARI NI BIASHARA. HABARI NI UCHUMI.

MARKUS MPANGALA,
Oktoba 17/ 2017
Dar es salaam

No comments:

Post a Comment

Maoni yako