October 18, 2017

RIWAYA YA WANG LIPING

KITABU: DOUDOU NA MAMA WAKWE ZAKE
MWANDISHI: WANG LIPING
MCHAMBUZI: KIZITO MPANGALA
Doudou Na Mama Wakwe Zake ni hadithi iliyoandikwa kwa lugha ya Kichina na mwandishi Wang Liping na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na wakalimani Chen Lianying na Han Mei. Kitabu hiki kina jumla ya kurasa 261 na kimegawanyika katika sehemu 24 za masimulizi yenye mtiririko mzuri ambapo sehemu inayofuata inategemea mhimili kutoka sehemu iliyopita. Kimechachapishwa na Zhenjiang Literature and Art Publishing House kikiwa katika lugha ya kichina na baada ya kutafsiriwa kwa Kiswahili kimechapishwa na Mkuki Na Nyota jijini Dar es Salaam Tanzania na kupewa namba za usajili (ISBN) 978 – 9987 – 08 – 284 – 1. Shukrani kubwa ziende kwa wakalimani  Chen Lianying na Han Mei kwa kutangaza lugha ya Kiswahili.

Ni hadithi inayofahamisha maisha ya kawaida ya Wachina lakini mafundisho yake yanafaa kwa kila mmoja wetu duniani. Hadithi hii kwa mara ya kwanza iliingia nchini Tanzania ikiwa kama mlolongo wa tamthiliya ambapo ilikuwa imefanyiwa marekebisho ambayo yalifanya mazungumzo ya wahusika yasikike kwa Kiswahili. Ilikuwa ikionyeshwa na shirika la habari la taifa (TBC) mwaka 2011.


Msichana Mao Doudou alikumbwa na mkasa wa kuachwa na mpenzi wake ambaye alikuwa mpenda pesa kuliko upendo kwa mwenzi wake. Katika hali kama hii maishani ni wazi kuwa ndoa ya aina hii haiwezi kusonga mbele endapo itatanguliza pesa mbele kuliko upendo unaostahili miongoni mwao. Miaka ya sasa ndoa nyingi zinakumbwa na tatizo hili ambalo huanza mwanzoni tu mwa mahusiano. Na mtu anayejitutumua kujionyesha ana pesa sana mbele ya mpenzi wake hakika huyo ni masikini wa fikra!

Tafuta mpenzi anayekufaa lakini usitume watu wakutafutie kisha wewe ukubaliane naye bila hata kuelewana kwa kina. Jambo hili ndilo liliomgharimu kijana Mao Feng na kupelekea kuachana na mpenzi huyo siku mbili tu baada ya harusi kufanyika. Mchakato wa kutafuta mchumba nchini China unafanywa na makampuni rasmi ambayo hukutafutia mchumba kwa kuilipa kampuni hiyo na kisha kujaza fomu maalumu. hiyo ni biashara ya kipekee sana ambayo huifaidisha serikali kwa kodi. Hivyo basi, mchumba tafuta mwenyewe, usijiiunize kwenye matatizo yasiyo ya lazima. 

Katika jamii zetu tumeona au tumefikwa na hali ya kuishi na mzazi wa kambo, hii ni kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinakuwa nje ya uwezo wetu kuzitatua. Mao Doudou baadae anapata mume ambaye ni Yu Wei na kuishi pamoja kwa misukosuko kutoka kwa mama wakwe zake. Lakini je, kwa nini MAMA WAKWE NA SIYO MAMA MKWE? Imezoeleka kuwa mama mkwe ni mmoja tu. Lakini hilo ni mtihani mkubwa sana endapo baba na mama wakaachana na kisha kuoa au kuolewa tena, kwa hali hii itakuwa ni MAMA WAKWE na siyo MAMA MKWE tena, vile vile ni BABA WAKWE na siyo BABA MKWE tena!

Katika hao mama wakwe, yupo mama mzazi wa kijana wa kiume ambaye anaishi na baba wa kambo pia yupo mama wa kambo wa kijana wa kiumbe ambaye anaishi na baba yako mzazi, hapo ndipo ugomvi unajitokeza kila mmoja anadai umpelekee mkwe. Ugomvi wa ndoa wa wazazi hakika mtoto usiuingilie, kwani Wahenga wa Kiswahili husema “wagombanao ndio wapatanao”. Ni vitendo vya aibu kugombana ovyo katika familia ambayo imekuwa na msingi thabiti tangu awali. Lakini kwa uvumilivu na busara kama alizozionyesha msichana Mao Doudou ushindi unapatikana kwa kishindo! Msichana Mao Doudou ni mfano wa kuigwa katika hadithi ya kitabu hiki.

Mapenzi ni matamu sana ikiwa huna ujeuri kwa mwenzako na yeye hana ujeuri kwako wewe! Kwa mahabuba yenye raha na amani mmoja wenu anaweza akakuambia ametembea duaniani kote kutafuta mpenzi lakini hajaona mpenzi mzuri kama wewe hapo mlipo! Safi kabisa. Hapa tumkumbuke nguli wa fasihi ya Kimombo bwana William Shakespeare katika mashairi yake aliposema kuwa kwenye mapenzi kunahitajika aina fualni ya uwongo ili umuweke mpenzi wako kwenye mstari ulionyoka na asitoke! Vitendo vya kudanganyana kiholela katika mapenzi ni ujinga. Hilo lilimkumba Mao Feng ambaye ni mtaalamu wa kuwabwaga wasichana hao akishakamilisha dhamira yake. Lakini wakati ulipofika wa kuachwa yeye aliona dunia ipo kichwani mwake ameibeba! Kwa hiyo, tujifunze na tuwe wa kweli. Hapa namkumbuka afande Issa Mnyongo alipotuasa kwa kusema “vijana kuweni wa kweli”

Umaarufu ni jambo la kujivunia kwa wapenda umaarufu na kujihisi kuwa ulimwengu mzima unawatazama. Mtu yeyote aliye maarufu kwa jambo lolote, tafadhali chunga sana umaarufu wako kwa kuwa kuna wakati umaarufu huo unaweza kuwa UMMA-HARUFU. Kijana Mao Feng kwa umaarufu wake aliweza kuwahadaa wanawake na kuwa mlevi kupindikia jambo liliomfanya aingie kwenye ndoa na mtu aliyemzidi umri kwa kiasi kikubwa na ndoa ikayeyuka siku mbili tu baada ya harusi. Makinika na fundisho linalotoka hapa.

Yeyote anayeitwa mama mkwe basi azingatie kwa nini anaitwa mama mkwe. Mama mkwe ni kiongozi, ni mzazi, ni mlezi, ni mshauri, ni mwalimu na kadhalika. Mama mkwe anayefikiri kwamba fedha ndio msingi wa upendo kwa watoto wake kuingia kwenye ndoa basi huyo hana sifa hizi zilizotajwa isipokuwa tu yeye takuwa ni mlanguzi, tapeli, mfitini, mchonganishi, mchochezi, mjanja, mwongo, mwenye chuki na kadhalika. Mao Doudou ni binti anayempinga mama yake hadharani kwamba fedha siyo msingi wa upendo kwa mume wake, Mao Doudou anasema (akiwa amekasirika); “mama sipendi useme hivyo! Ni kwa nini kina mama wengi wako hivyo, wao wanachoangalia ni pesa tu” Uk. 36. Makinika na fundisho linalopatikana hapa.

Mama mkwe mwenye nia njema na watoto wake walioingia katika maisha ya ndoa ni mfariji, ni mwalimu, ni kiongozi, ni mlezi, ni mzazi, ni mshauri, ni mwenye amani ya nafsi na kadhalika. Pongezi hizi apate mama yake mzazi Mao Doudou baada ya kukosolewa na binti yake huyo kuhusu mawazo yake katika fedha. Mama anabadili msimamo na kumfariji binti yake kwa moyo wenye faraja kwamba wanaweza kuishi kwa kuvumiliana bila hata fedha ingawa kuna wakati watahityaji fedha kwa matumizi mbalimbali. Mama anasema; “Haya, kama unaweza kuvumilia maisha ya kawaida yasiyo na fedha nyingi mimi siwezi kupinga”. Hapa mama amejitambua kwa kiasi kikubwa sana, anapaswa kumfariji mtoto na siyo kumjaza falsafa za maisha ya ndoa bila fedha hayaendi, hii si kweli.

Kila mmoja anapenda kupendwa na mtu wa jinsia tofauti kwa namna ya pekee yenye ukaribu wa pekee na kwa hali pekee. Hilo ni juio la kila binadamu ingawa wapo binadamu wenye umri mdogo ambao wanakua na baadae watatambua hilo. Hata mimi nahitaji kupendwa na mtu wa jinsia tofauti kwa namna ya pekee! Ndio ubinadamu huo. Tuwape pole wale wote waliopoteza wenzi wao kwa namna mbalimbali. Hali hii inaweza kukufanya uchanganyikiwe kwa wakati fulani. Dada Yu Hao katika kitabu hiki alipoteza mume wake katika ajali ya gari siku mbili tu baada ya harusi, hali hii imemsababishia aishi kwa mfadhaiko kwa muda mrefu na hivyo kupata matatizo ya akili. Poleni nyote mliokumbwa na matatizo kama hayo. Jamani mapenzi matamu!

Kijana wa kiume, kwa kuwa name ni wa kiume kama wewe wa kiume usomaye hapa, basi makinika na funzo hili alilolionyesha kijana Yu Wei kwa kujitambua kwa umakini mkubwa. Yu Wei alijiweka wazi kwa mpenzi wake Mao Doudou aliyempenda maishani. Hakumuahidi magari, fedha, majumba na kadhalika. Hii ilimfanya akubalike zaidi na familia ya Mao Doudou kwa uwazi wake. Hivyo basi, kijana mwenzangu wa kiume makinika na fundisho hili. Kuwa muwazi. Tabia ya kudanganya kwamba una magari, fedha nyingi, maduka makubwa, majumba makubwa na kadhalika itatupeleka pabaya katika maisha yetu. Uchunguzi ukifanyika utaona kwamba anayeahidi au kutamba hivyo hata mkokoteni wa kuvuta na punda hana! Kama kweli unavyo vitu hivyo, basi usivipe kipaumbele kwa mpenzi wako!

Kusema kweli kuishi pamoja na mama mkwe mtukutu ni taabu zaidi kuliko kufanya kazi nyingine, mbali na kuwa mtiifu na mvumilivu wakati wa kukosolewa na mama mkwe wa aina hii, ni lazima kuwa na uwezo mwingine wa kukabiliana naye! Mama mkwe wa namna hii ni hatari zaidi kwa wanawe. Mama mkwe sikiliza kwa makini, hata kama mkweo amekosea jambo au kama humpendi jitahidi kuwa naye karibu kwa amani na ujitathmini kwa nini humpendi. Katika kitabu hiki tunaona jinsi Cao Xinmei anavyomchukia Mao Doudou lakini Mao Doudou anajitahidi kumvumilia. Kwa hiyo, fundisho lake ni kwamba mama mkwe unapaswa kuwa mstahimilivu na mwenye busara unapokuwa na mkweo. Mkweo ni binadamu kama wewe na ukumbuke kuwa na wewe ulikuwa mkwe kwa wazazi wa mume wako. Kama ulitendewa jambo baya huko basi jitahidi sana usihamishie kisasi chake kwa mkwe uliyenaye hapo!

Wakati wa dhiki udhati ndio huonekana kwa kiasi kikubwa sana. Kumpenda ndugu, jamaa, au rafiki yako kwa dhati kusionekane wakati wa dhiki tu bali ni wakati wote. Ikiwa kama mwadhani ya kwamba kumpenda ndugu, jamaa, na rafiki zenu kunahitaji fedha za kigeni basi jueni ya kwamba mnakosea. Msijivike mavazi yanayosimulia fedha ili kuonyesha upendo kwa ndugu, jamaa, au rafiki zenu. Upendo siyo fedha na fedha siyo upendo! Makinika na falsafa hii ndogo yenye manufaa makubwa.

Wifi ni mtu mzuri sana katika familia na anao umuhimu wake kwa mkeo wewe kijana wa kiume. Wifi anaweza kumchombeza mke wako ili amakinike zaidi kwa mahabuba mazito kwako, anaweza kumchombeza mkeo ili ajihisi kuwa bila wewe mambo yake yote yanaharibika, anaweza kumchombeza ili ajisikie kuwa yupo kwenye ghala salama lisilo na wadudu wanaoharibu nafaka, anaweza kumchombeza ili ajihisi kuwa wewe ni jemedari wa majukumu yanayokupasa kwake bila kuchenga na ajihisi kuwa hakuja kwako kula na kunywa bali alifuata mapenzi ili kulainisha moyo wake! Haya ni matunda ya wifi bora. Lakini endapo wifi anakuwa kinyume na chombezo kama hizo basi kila kukicha anamsimanga mkeo, anamkejeli, anamtukana, anampa kila neno la kumkatihsa tama. Kwa hakika wifi kama huyu ni bomu kubwa sana. Hivyo basi, ninyi mawifi kaeni na mawifi zenu vizuri ili muishi kwa amani na furaha.

Pan Meili ni msichana anayetambua thamani ya kuonekana kwa asili na siyo kujiweka nakshi mbalimbali za urembo mpaka kujiondolea asili yake. Hivyo basi kina dada mnapaswa kujali asili ya mionekano yenu ili mjiepushe na magonjwa ya ngozi yanayotokana na matumizi yasiyo ya lazima ya vipodozi vikali au vilivyokwisha muda wake wa kutumiwa.

Mafunzo yanayopatikana katika kitabu hiki yanafaa sana katika maisha yetu. Akina dada igeni mfano wa dada Mao Doudou katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha ya ndoa. Msidanganyike kusema kuwa  maisha ya ndoa bila fedha nyingi hayaendi. Nanyi mama wakwe popote mlipo msiwatendee wakwe zenu vibaya, kama ni kuwaonya basi muwaonye kwa nidhamu na heshima ili muishi kwa amani na furaha daima.

Ushauri wangu kwa waandaaji wa tamthiliya ya SIRI ZA FAMILIA ambayo hurushwa na Clouds Media, ni kwamba wanaweza kuiweka tamthiliya hiyo katika kitabu itakapomalizika ili kutunza kumbukumbu kwa miaka ijayo kama mwandishi Wang Liping alivyofanikisha hilo katika maonyesho ya MAO DOUDOU NA MAMA WAKWE ZAKE.

© Kizito Mpangala

     0692 555 874, 0743 369 108

No comments:

Post a Comment

Maoni yako