December 07, 2017

KILICHOTOKEA KATIKA UCHAGUZI WA KATA 43 HAKINA TASWIRA NZURI 2020

NA HONORIUS MPANGALA 

TANZANIA ni nchi ambayo wananchi wake wamejengwa kwenye ushrikiano na mshikamano mkubwa sana katika aisha yao ya kila siku. Yawezekana misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa hili ilikuwa haswa ambayo inatufanya hata wale wenye mitazamo tofauti kwenda sawa na wengine. 

Tumekuwa tukipata viongozi wetu kwa njia za uchaguzi kwa kuwapa nafasi wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka. Uhuru wa kuchagua ni moja ya vipengele vilivyoko katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inayotumika hadi sasa. Katiba imeeleza kila mtu anauhuru wa kuchagua na kuchaguliwa.

Wananchi wa Kijiji cha Katumba Kata ya Ibighi
Katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 43 hapa nchini umenifanya nitafakari hatma ya Tanzania kwa yale ambayo nimepata kuyaona na kusikia toka maeneo tofauti. Hakika kuna mahali tumeteleza na tunapaswa kujisahihisha. Kuteleza ninakosema ni kwa yale matendo ambayo yamekuwa yakiibuka wakati wa uchaguzi mdogo katika maeneo tofauti.


Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi vyama vilivyoshiriki na Kata zao ni kama ifuatavyo; CCM-wagombea 43, Chadema-wagombea 42, ACT-Wazalendo-wagombea 18,,ADA-Tadea-mgombea mmoja, ADC-wagombea wanne, NCCR-Mageuzi-wagombea 6, NRA-wagombea wawili, SAU-wagombea wawili, TLP-mgombea mmoja, UDP-wagombea wawili, CHAUMA-mgombea mmoja, na CUF-wagombea 30, DP-wagombea watatu.

Siasa zimekuwa za mihemko ya hali ya juu kwa wafuasi na wanachama wao. Suala la kustahimili mihemko ni jambo ambalo wanasiasa wengi wa ngazi za chini linawashinda. Kitendo cha kushindwa kuhimili mihemko kinatoa tafsiri nyingine ambapo mauaji huweza kufanyika na baadaye watu kushindwa kuamini kinachotokea.

Matukio ya uvinjifu wa amani yamekuwa Mengi katika maeneo ambayo uchaguzi umefanyika  Novemba 26, mwaka huu. Kuanzia wilaya ya Mbinga katika Kata kama Mhongosi hadi maeneo ya mkoa wa Manyara, Arumeru na mkoani Tabora na kwingineko uchaguzi zimekutwa na changamoto ya utulivu wa amani kwa raia ambao ndo wapiga kura.

Kupanda kwa mihemko ya kisiasa kiasi kile kunafanya matukio kutokea watu wakifanyiana kila aina ya uhuni, uharibifu na hata kuuana ili tu kufanikisha azimio wanalolipanga kwenye chama chao au matakwa binafsi ya wanachama.

Picha nyingi zilizokuwa zikizagaa katika mitandao ya kijamii zikielezea matukio kulingana na mahali zilisikitisha hakika. Damu inamwagika, watu wanaumia, huku wengine wakisifia hali mbaya kama hiyo. Tupo katika hatari.

Nimejiuliza kama uchaguzi mdogo tena wa Kata 43 uko hivi itakuwaje kwenye uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani mwaka 2020? Vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaaje na  changamoto hizi ambazo zimejitokeza siku ya uchaguzi mdogo wa udiwani kwa Kata 43?

Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanakila sababu ya kukemea vikali haya yaliyotokea kwasababu waliokutwa na matatizo wakati wa uchaguzi ni binadamu kama wengine hivyo kama tume kutokutoa maelezo ya kukemea ile hali basi inaondoa utanzania wetu tuliozoea kuishi.
Vyama vyote vya siasa vinapaswa kukemea hadharani matukio yasiyo ya kiungwana na yale ya kijambazi kama kufanya uporaji na utekaji wakati wa kampeni na kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Ikiwa watu wanapitia katika kipindi kama hiki ambacho kila chama cha siasa kimahitaji makubwa ya kutumia nafasi yake kuwafahamisha wafuasi wao kuwa wenye kufanya siasa safi. Siasa ambayo hata baada ya uchaguzi mtaweza kukaa meza moja watu wakanywa na chai.

Viongozi wana kazi kubwa ya kuwaeleza wanachama wao  juu ya matunda na faida ya kuilinda tunu ya taifa ambayo ni amani.
Ni jambo linaloshangaza sana kuona wafuasi wengi wakitendeana unyama katika kampeni za uchaguzi mdogo badala ya kushindana kwa hoja pamoja na kuvumiliana.

Siasa sio matusi wala sio ugomvi lakini kwa hali iliyopo tunakoelekea naona kesho yetu ni ngumu  hususani uchaguzi ujao. Kwa sababu watu wataanza mapema kuwapa wakati mgumun hawa viongozi walioingia madarakani kwa kuona mbinu na njia zilizotumika katika ushindi wao ni zile zisizo za siasa safi.

Moja ya vitendo ambavyo huwaaminisha wapiga kura ni kuamini kama kuna wizi wa kura katika uchaguzi wowote. Jambo ambao kwa vipindi viwili nilivyoshiriki zoezi la upigaji kura na kuwa msimamizi wa uchaguzi nilipata majibu ni uzushi unaoenezwa na wanasiasa tu.

Mwaka 2010 nikiwa msimamizi msaidizi namba moja, aliyekuwa msimamizi Mkuu aliniachia zoezi la uhesabuji wa kura na nikalifanya katika mazingira ambayo kila wakala alikubali alichokipata na akasaini matokeo.

Mwaka 2015 pia katika uchaguzi Mkuu ambao Novemba 26 ulifanyika ule wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na walioshinda kipindi hicho kwa kupata matatizo mbalimbali. Nilikuwa msimamizi mkuu wa kituo.

Zoezi la kuhesabu kura nililifanya tena kwa mara nyingine na kwa kuhahikikisha kuwa hakuna udanganyifu unaweza kujitokeza huku macho ya mawakala yakiwa kwangu na zoezi kwenda vizuri. Sasa najiuliza huu wizi ambao unatamkwa mara nyingi vituoni unakuwa wizi wa namna gani kama mazingira ya uhesabuji kura yanakuwa mbele ya mawakala wote?

Tuna kila sababu ya kukemea vitendo ambavyo vinavyochafua taifa hili nyakati za uchaguzi. Pia vyombo vya ulinzi na usalama kutimiza majukumu yao ili kuondoa sintofahamu baina yao na wananchi.

Ulemavu ambao watu wanapeana sasa kutokana na uchaguzi mdogo utakaa katika mioyo yao na kupandikiza chuki mbaya katika vyama vya siasa  na tamati yake ni watu kuishi kwa kubaguana. Nalisema hili baada ya kushuhudia baadhi ya maeneo ambapo hata shughuli za kijamii kama misiba watu wa vyama vya siasa walizikana kutokana ufuasi wa marehemu au familia kwa ujumla.

Ni nini ambacho anaweza kujifunza mtoto mdogo anapoona msiba  umetanda kwa sare za chama cha siasa. Ni nyakati hizi ambazo kampeni za kunadi chama hufanyika hata misibani kwa watu kuwa na uwingi wao kwa kuvaa sare za chama. Ni taswira mbaya inayojengeka hata akilini mwa watoto wadogo wanapoona hali hiyo.

Mungu auepushie mbali haya matatizo na awape uwezo wa kuona na kitenda kazi vyema na kwa weledi vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu nambari 0628 994 409

No comments:

Post a Comment

Maoni yako