August 08, 2010

Dr Slaa ataweza?

Jana nilikuwa katika msafara wa mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA. Nilikuwa nasoma sana saikolojia za mashabiki wake na wanachama wake pia. nilikuwa nawasoma sana kadiri muda ulivyokuwa unakwenda.

Kwa hakika binafsi namkubali sana Dr Slaa, na ninaumia sana kwa hatua yake ya kugombea urais badala ya kujenga kwanza ngome huku chini(bungeni). hata angegombea udiwani, mimi naamini tunajenga mzizi, lakini hakuna jinsi ni lazima tukubali wakati unakwenda na sasa ni miaka takribani 17 tangu kuanza vyama vingi.

Hata hivyo natambua sisi watanzania ni WANAFIKI.... sitanii na wala situkani..... naamini Dr Slaa kwa jinsi anavyoendesha mambo ndani ya bunge na namna anavyowasilisha tafiti zake. Nasema anastahiki kwenda Magogoni huku bloggers tukipiga jaramba pale Luthuli.

Je tumejiandikisha kupiga kura?(unafiki wa kwanza), je tumeweka dhamira ya kumchagua Dr Slaa(unafiki wa pili). Mimi nitamchagua, na wewe anza sasa.....

swali linabaki Je Dr Slaa ataweza?

3 comments:

 1. NI mpaka aweze ndio jibu la uhakika litakuwepo.:-(

  ReplyDelete
 2. Nami nitamchagua. Bila ubishi ingawa nina kadi ya chama cha kijani, nina uhuru. Kadi sirudishi ila kura siwapigii.

  ReplyDelete
 3. George Jinasa21 August, 2010

  Binafsi, sina tatizo na SLAA wala CHEDEMA. Hata hivyo, kwa maoni yangu SLAA na CHADEMA bado hawajafanya maandalizi ya kutosha kustahili kuchukua dola. CHADEMA bado ina miguu katika sehemu chache sana za nchi hasa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Kigoma kidogo. Kipindi cha miaka zaidi ya 15 CHADEMA imekuwepo ni kikubwa. Tilitegemea chama kingekuwa na nguvu nchi nzima au sehemu kubwa ya nchi kama kimejiona kuwa tayari kuchukua dola.

  Japo rekodi za SLAA nazikubali kuwa ni nzuri, bado ajaweka mikakati inayoeleweka katika ngazi ya chama na yake binafsi kama amekomaa na ana maandalizi ya kutosha ya kuchukua dola.

  CCM kutokana na bahati mbaya au nzuri ya kihistoria kimesheheni katika kila sehemu ya nchi, vijijini na mijini. Ni chama cha wakulima kama kilivyo chama cha wafanyakazi. Ni chama cha wakristo kama kilivyo chama cha waislamu na wapagani. Ni chama cha watanzania weusi kama kilivyo chama cha watanzania wenye asili za kihindi, kiarabu na kizungu. Ni chama cha Tanzania bara kama kilivyo chama cha Tanzania Zanzibar. Ni chama cha matajiri, masikini, wasomi na mbumbumbu kama mimi. Vyama vingine havina bahati hii. Na mambo hayo ambayo CCM kimebahatika kuwa nayo ni msingi wa amani, umoja wa kitaifa na utulivu wetu. DR SLAA pamoja na wapinzani wenzake kama wanataka kwenda ikulu ni bora wakafanya mikakati kwanza kuvitoa vyama vyao katika sura isiyo ya makusudi ya ukanda na kuvifanya vya kitaifa kwa maana inayoonekana kwa vitendo siyo vitabuni.

  Jambo moja naliona kuwa la msingi kwa CHADEMA na SLAA pamoja na wapinzani wengine waliyoweka wagombea uraisi. Watumie kampeni zao kusambaza chama katika nchi nzima. Wasiwe na haraka haraka sana ya kwenda ikulu.

  Nimalizie kwa kuitakia CHADEMA pamoja na vyama vingine vya upinzani uimara katika siku za usoni ili viweze kutoa upinzani imara na hata kuchukua dola na kuipumzisha CCM. Kwa sasa hivi kura yangu ya maana naipigia CCM mpaka nitakapopata chama mbadala kilichojiimarisha kuweza kuchukua ikulu. Sipigi kampeni wala si mwana chama wa chama chochote kwa hiyo kwa wengine siwasemei. Kila mtu apembue mtama na pumba na afanye chaguo sahihi bila kishawishi cha pesa.

  Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

  ReplyDelete

Maoni yako