January 28, 2013

HAKUNA AJUAYE SIKU YA MWISHO WA DUNIA


Na Markus Mpangala, Nyasa
Mchungaji Harold Camping wa Family Radio alisema kuwa mwisho wa dunia ungelikuwa ni Mei 21/2011. Akaongeza kwa kusema siku hiyo Watakatifu watakwenda mbinguni na hapo ndipo mwisho wa dunia utatokea. Katika mahubiri wa Mchungaji Harold Camping moja kwa moja yanashabihiana na yale ya Mchungaji Benny Hinn, naye mwenyeji wa Marekani.

Mchungaji Benn Hinn naye akafuata mkondo wa Harold Camping kwa kubashiri mambo mbalimbali, kwamba yatatokea, lakini hakuna lililojiri hata moja. Ubashiri wa Mchungaji Harold Camping ameweka kwenye kitabu chake cha  Time has an end. Na amehubiri kuwa Mei 21, 2011 ndiyo mwisho wa dunia.

Lakini naomba niwaambie neno hili; “Watu huniheshimu kwa midomo yao, ila mioyo yao iko mbali nami. Nao huniabudu bure wakifurahisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu” (Mathayo 15;8). 

Tunaishi nyakati hizi lakini hatujui tushike kitu gani kumuabudu Mwenyezi Mungu. Tumekuwa watu wa kutangatanga kwa kila aina ya mahubiri. Lakini haigombi kuyasikiliza ila mwana mwema husikiliza na kufanya tafakuri juu ya yale maagizo ya Baba wa Mbinguni. Pia niharakishe kusema sikupendelea kujikita katika dini hivi kwani wasomaji wetu wengine ni waumini wa dini zingine. Kwakuwa tunavunja mlango ili tujenge nyumba basi leo waniwie radhi nitasema machache.
Je, Biblia anayosoma Mchungaji Harold Camping ni ile ambayo sote tuisomayo? Hilo la kwanza, na kama jawabu ni ndiyo ni kwanini anataka kupingana na Biblia anayohubiri na kuwafundisha watu wake?
Je, tujiulize alifanya hivyo kwa Nasibu kwamba Mei 21, 2011 kuwa mwisho wa dunia? Ni muujiza ama neema gani aliyoshushiwa hata akasema kuwa siku hiyo ndiyo ile ambayo Mwana wa Adamu alisema kuwa ni Baba wa Mbinguni pekee aijuaye siku hiyo?

Iliandikwa hivi; “Walakini habari ya siku ile hakuna aijuaye, hata Malaika walio Mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake” (Mathayo 24:36). Kwa vyovyote itakavyokuwa na kwa namna yoyote yanavyokujia mahubiri ya namna hii, kitu cha kwanza yanakupa hofu. Kwahiyo matokeo yake ni kuchanganyikiwa kwamba unabii unakuja tarehe hiyo ya Harold Camping?
Lakini tutumia Biblia hiyo kuangalia unabii unaohubiriwa, kama ambavyo tulivyoona Injili ya Mathayo kwamba ‘WALAKINI’ hakuna aijuaye siku ile, bali Baba peke yake. Hivyo angalia neno la Mungu linasema; “Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa, wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa”, (Mathayo 24; 40-41).
Kuna mambo mengi ynasemwa kuwa ni mwisho wa dunia, lakini mara zote hakuna ukweli wowote kwani hakuna ajuaye siku ile. Mwaka 1999 lilitokea shirika fulani la Bima huko Marekani, ambalo likuwa linachukua mali za watu waliosadiki kuwa mwisho wa dunia ni mwaka 2000.
Sijui ni kitu gani kilichowafanya waamini hivyo lakini ukweli haikutokea, ni Mungu pekee ajuaye. Wakaishia kuendelea kuishi kwa kubashiriwa, hata hivyo ilisemwa na mwana wa Adamu kuwa angalieni mtu asiwadanganye. Kwasababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.

Kwa mambo yanavyotokea na kwa jinsi tunavyojipa hangaiko ndivyo tunavyozidi kuona akina Harold Camping ndiyo tumaini letu. Waandishi wa Biblia hawakuwa magwiji wa Theolojia, hawakuwa Maprofesa wala madaktari walau wasanifu wa habari bali walielewa mafunzo ya Kristo wakayaandika na kuyafundisha kwa uhuru ili watu wajue na kurudisha waliopotea.
Na wakasisitiza kuwa  mkisikia yuko Jangwani asilani msitoke, wala mkisikia yumo ndani ya nyumba fulani, msihangaike kutoka. Sikiliza ndugu msomaji; ilisemwa kwamba desemba 31, 1999 utakuwa mwisho wa dunia, lakini haukutokea hivyo.

Ikasemwa Desemba 31, 2000 utakuwa mwisho wa dunia, lakini haikutokea hivyo. Sisiti kusema haya ni mafunzo ya akina Kibwetere wa Uganda na miungu bubu ya wahuni inayopigiwa kelele.

Mfano wa pili ni waumini wa UFO, ambao walikufa kwenye mji wa San Diego, Marekani mnamo Mei 26, 1997 kwa madai kuwa walikuwa wakisubiri kwenda mbinguni kwa dhehebu lao la ‘Lango la Mbinguni’.

UFO ni itikadi juu ya vitu vya anga visivyotambuliwa, wanaamini kuliko imani yenyewe, inatisha kweli kweli! Neno hili UFO ni kirefu cha Unidentified Flying Objects. Mwisho wa waumini hawa wa UFO wakawa ni kama akina Harold Camping wanaohubiri mwisho wa dunia ungelikuwa ni Mei 21, 2011.

Mfano wa tatu; Mchungaji Jim Jones wa nchini Marekani katika dhehebu lake walikufa watu 914 mwaka 1978 kutokana na imani hizo za mwisho wa dunia kuwa ni siku fulani. Dhehebu jingine lilijiita ‘Tawi la Daudi’, ambalo ilikuwa mjini Waco jijini Texas, yapata April 19, 1993 nchini Marekani lilikuwa katika mashambuliano ya risasi dhidi ya jeshi la Polisi na wengi wakauawa.
Sababu kubwa ilikuwa kuamini siku ya mwisho ni hii hapa, au ile kule na zaidi ipo pale. Hivyo hata kutii sheria za nchi tabu! Mahubiri ya Harold Camping siyo mageni, kwani Yuda alikwisha kuwavuta watu siku ile wakamsadiki kisha akawahadaa.

“Hata kabla ya hapo alipoondoka Theudia, akajidai kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu” (Matendo 5; 36-37).

Hivyo ukitazama wafuasi wa wachungaji hao waliangamizwa kabisa hawakusalia hata chembe. Na imeandikwa “Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini” (Mika 7:5). Ni upendo wa mwenyezi Mungu.
Lakini wafuasi wanaoamini kwamba siku hiyo ni ile aliyoitaja mhubiri Harold Camping, angalieni kwamba watambaratika hakuna akayesalia. Wengi hawajui kwamba wanadanganywa, wameweka kila kitu mikononi mwa Harold Camping wala hawajisumbui kujua ukweli. Na hao wengi ‘watakuwa siyo kitu.’

Ni dhahiri kwamba siku ya mwisho itawadia katika ulimwengu huu na hakuna atakayesalia. Bibilia inasema hivi; ‘Halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa’. Na hakuna kiumbe hai atakayesalia kati yetu tuliomo.

Imeandikwa “Basi alikaribia mahali niliposimama; nami niliogopa alipokaribia nikaanguka kifudifudi; lakini aliniambia fahamu, Ee mwanadamu, kwa maana maono haya ni ya wakati wa mwisho” (Daniel 8:17).
Wakati watu wakiwa katika mshangao huo wa siku ile (nasema ile maana haikutajwa siku rasmi katika Biblia) viumbe wote wataondolewa katika ulimwengu huu na kupotezwa kabisa. “Basi yoyote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi” (Mathayo 24:3).

Vilevile imesemwa “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,”(2 Timotheo 3:1-2).

“Lakini siku ya bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuhimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? (2 Petro 3:10-12).

Na imeandikwa kwamba; “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na  kusema iko wapi ahadi ya kuja kwake? Kwa maana tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali hiyo tangu mwanzo wa kuumbwa” (2 Petro 3:3-4).

Sasa kwakuwa mahubiri ya Harold Camping yalida kuwa siku ya mwisho kuwa ni Mei 21, 2011 basi tutafakari mwenendo hu unaashiria nini. Kwa imani ya mwenyezi mungu na kwa mwongozo wa Biblia tumwachie Mungu aamue. Imeandikwa “Mbingu na nchi zitapita Kamwe; lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” (Mathayo 24:35).

“Mungu si mtu, aseme uwongo; wala si mwanadamu, ajute; iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? (Hesabu 23:19).

Je, ni Yesu yupi na Mungu yupi aliyetaja siku hiyo hata Harold Camping akatubashiria kuwa ilikuwa ni Mei 21, 2011 na kwanini haijatokea? Na hata kama tutajiuliza siku hiyo ni lini, hakuna anayejua. Tumeonywa kwamba dai la kujua siku ile lipo tangu zamani za wanafunzi wa Yesu, lakini hawakupata kuijua, na hakuna aliyeijua baadaye hata ufufuko wa Yesu.

“Si juu yenu kupata ujuzi wa nyakati au majira ambayo Baba ameweka katika mamlaka yake mwenyewe” (Matendo 1:7). “Nani ni mshauri wa Bwana? “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani,” (Warumi 11:33-34). 

“shauri la Bwana lasimama milele, makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi” (Zaburi 33:11). Imesemwa kwamba mawazo ya bwana siyo mawazo yetu, na kamwe siyo mawazo ya Harold Camping yatafikisha ulimwengu mwisho. Soma Isaya 55:8-11.

Na tumefundishwa katika; 2 Timotheo 3:1-5).  Watu wamepoteza maisha yao, kwakuwa wanasadiki kuwa siku hiyo ni ile aliyotaja Mchungaji Harold Camping.
Amri ya Bwana haina mshauri, yeye hutenda awezavyo na apendavyo ndiyo maana hakuna binadamu aliyetajiwa siku ile. Na ‘WALAKINI’ hakuna aijuaye wala Malaika wa Mbinguni, wala Mwana wa Adamu, bali ni Baba peke yake.

1 comment:

  1. hakuna anayeweza kutabiri mwisho wa dunia zaidi ya baba Mwenyezi Mungu....

    ReplyDelete

Maoni yako