January 22, 2013

TEKNOLOJIA YA GOLI ITAMALIZA UTATA WA MAGOLI?


Na Markus Mpangala

Mwaka 1986 Diego Maradona alifunga bao la mkono, lakini mwamuzi hakuona akakubali kuwa ni bao halali. Waingereza walilalamikia hilo, lakini mwamuzi alishapitisha uamuzi wake ni bao halali. Tangu hapo Maradona amekuwa akisema bao lake hilo ni la ‘mkono wa mungu’. Mwaka 1966, kiungo wa England, Geoff Hurst apiga shuti kali likagonga mtambaa panya na kugonga chini kisha kurudi uwanjani. 
Diego Maradona

Lakini wakati mwamuzi wa mchezo hajaamuru chochote wachezaji wa England wakaungana na kiungo huyo kushangilia na mwamuzi akakubali ni bao halali. Lakini mpira ule ulipogonga mtambaa panya kisha kugonga chini wala haukugusa mstari. Geoff Hurst akaingia kwenye rekodi ya dunia kwa
kufunga mabao matatu katika mechi ya fainali. Rekodi hiyo imefikiwa na kinda wa Brazil, Oscar Dos Santos ambaye alifunga mabao matatu wakati wa mechi ya fainali ya kombe la dunia kwa vijana chini ya miaka 20 dhidi ya Ureno. 
Lakini miaka 44 baadaye yaani mwaka 2010 katika michuano ya kombe la dunia nchini Afrika Kusini, ni England iliyonyimwa bao.
Frank Lampard alifumua shuti kali likagonga mtambaa panya kisha litua ndani ya lango huku kwa kasi ya ajabu golikipa wa Ujerumani, Manuel Neuer alidaka kiustadi mkubwa.
Mbwana Samatta, akikabiliana na beki wa Zamaleki ya Misri
Mwamuzi wa pambano hilo alikataa kuwapa bao England. Waingereza walichachamaa baada ya michuano hiyo huku wakikumbuka kipigo cha mabao 4-1 walichopata kutoka kwa Ujerumani. 
Waingereza wakasahau kuwa wao walitwaa kombe la dunia kupitia bao lenye utata, kwani walifanikiwa kuifunga Ujerumani ya akina Franz Backenbauer na  Gerd Muller. Lakini ilipotokea kwao kunyimwa bao wakapayuka dunia nzima. Na sasa majadiliano ya kutumia Teknolojia ya goli yakachukua mkondo wake.Teknolojia hiyo maarufu kwa jina ka Jicho la Kipanga (Hawk Eye) ilipenyezwa katika korido la FIFA ili ipate uungwaji mkono. 
Nadhani teknolojia hiyo ilipaswa pia kutumika kutambua mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji wa Kilimanjaro Stars, John Bocco dhidi ya Burundi kwenye michuano ya CECAFA inayoendelea nchini Uganda. Tukiacha hilo, ni wazi sasa teknolojia ya goli (Hawk Eye) itakuwa njia mbadala huku tukikumbuka shirikisho la soka la Ulaya linatumia waamuzi watano katika pambano moja. 
Waamuzi wawili wanakaa nyuma ya goli, yaani mmoja mmoja kila upande. Hivyo ukiongeza na mwamuzi wa akiba wanakuwa watano. Naam, Jicho la Kipanga(Hawk Eye) imeshakubalika na kuthibitishwa na FIFA. Kwahiyo, FIFA imesaini  Mkataba Matumizi ya Teknolojia ya kutambua goli (Hawk Eye). Teknolojia hiyo itafanyiwa majaribio nchini Japan, ambapo baadaye itajaribiwa kwenye michuano ya klabu bingwa dunia itakayofanyika nchini humo. 
Dhumuni la teknolojia hii ni kutoa msaada kwa waamuzi ili kuamua kama Mpira umevuka mstari wa Goli na hivyo kuwa Goli halali. FIFA imepiga hatua mbele baada ya kusaini Mikataba na Kampuni mbili za Waundaji wa Mitambo itakayotumika ya kutambua goli. Mitambo hiyo inajulikana kwa jina la GLT (Goal Line Technology).
Kampuni za zilizoshinda tenda hiyo ni Hawk-Eye Innovations na Fraunhofer ISS (GoalRef), ambapo mitambo yake itatumika kwenye Mashindano ya FIFA ya Klabu Bingwa Duniani huko Japan kuanzia Desemba 6 hadi 16 mwaka jana. 
Franz Beckenbauer
Katika hali hiyo wengi wanaweza kusema ni suala zuri kwa maendeleo ya mpira wa miguu. Lakini vilevile tunapaswa kuwaangalia waamuzi na mamlaka yao katika mechi na soka kwa ujumla. Kwa hali halisi kwanza teknolojia hiyo itaondoa kabisa malalamiko ya mabao ambayo yanakataliwa na waamuzi. Lakini vilevile itasaidia waamuzi kuwa na nafasi bora kuondoa malalamiko yoyote ambayo yatachangiwa na uamuzi wao. 
Tekonoliia hiyo inatumika pia katika mchezo wa Tennis ambapo humsaidia mwamuzi kuangalia mpira kama umegusa mstari au umeangukia nje ya mstari au ndani ya uwanja. Teknolojia hiyo inasaidia sana waamuzi wa Tennis kuamua pointi halali kwenye kutafuta Seti. Tumeona hayo kwenye michuano mingi kama US Open, Wimbledon, Ausralia Open, Beijing Open, Olimpiki, na michuano kemkem
inayosimamiwa na shirikisho la Tennis. Hata hivyo kwa suala hili bado naona tunawahitaji sana waamuzi ambao wanaweza kutuletea matokeo mazuri dimbani. Licha ya kuletewa teknolojia hii bado tunahitaji kuwaamini waamuzi ingawaje kuna nyakati wanakera. Pia teknoloajia hii inaamua magoli tu, lakini haitoi nafasi kwa rafu mbaya au mchezo mbaya wa mchezaji fulani ambao mwamuzi anashindwa kuona. 
Mathalani Mwinyi Kazimoto, David Beckham, Dickson Daudi, na wengineo wamekuwa waathirika wa ukosefu wa teknolojia ambayo ingeweza kusaidia namna bora ya kubaini uchezaji mbaya kwa baadhi ya wachezaji.
Madhara ya teknolojia hii ni kuongezeka kwa malalamiko mengine ya uamuzi wa waamuzi. Hali ambayo itawapotezea uwezo wao wawapo dimbani. Ni hatua nzuri kwa Hawk Eye lakini ni wakati mzuri pia kuchambua makosa mengine dimbani yanayostahili kutegemea kamera ili kuepusha madhara kwa wachezaji.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako