March 11, 2013

KUFUKUZA MAKURUTA 95 WA JESHI LA POLISI HAITOSHI


Markus Mpangala

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
Tukio la waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi kuwafukuza Makuruta 95 wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi kwa kile alichooita kugundulika kutumia rushwa kujipatia ajira, bado linaelea katika vichwa vya watu juu ya msingi wa maadili yetu.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Renatus Chalamila amehusishwa na rushwa katika kuajiri. Waziri Nchimbi amechukua hatua zaidi baada ya kumsimamisha kazi Kamishna huyo. Alisema pia taarifa za uchunguzi za Kamishna huyo, ambaye anashughulikia masuala ya ajira zimewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete ambaye ana mamlaka ya kumfukuza kazi au uamuzi mwingine wowote.

Japokuwa waziri Nchimbi ametaja pia maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi ambao wamehusishwa na makosa mbalimbali lakini binafsi nimeguswa na huku chini kabisa (Makuruta). Kwa maana nyingine harakati za vijana 95 ambao wamefukuzwa na waziri Nchimbi waliokuwa wakitarajiwa kuingia kwenye ajira ya ndani ya Jeshi la Polisi, linatuletea swali la msingi juu ya maadili na namna tunavyojenga usalama wetu nchini. Hii ina maana katika Makuruta hao 95 tulikuwa na watu wenye tabia tofauti, lakini baya zaidi wamekutana katika msingi wa kutoa rushwa ili wapate ajira.

Namna nyingine tunajiuliza mfumo wetu wa jira katika sekta za ulinzi na usalama ukoje na nani anawajibika kuutengeneza pale unapokwenda kombo. Makuruta 95 ni wengi au hata wangelikuwa watano tu, lakini ukweli tunabakia katika mwenendo mbovu wa jamii iliyochoka kufuata kanuni hivyo kila kitu kinatakiwa kwenda ‘fasta fasta’. Ni tabia hii ya ‘fast tracking’ inatufikisha mahali pabaya kabisa na kushuhudia vijana wadogo wakijihusisha na rushwa.

Naam kufukuzwa kwao ni ushahidi wa wazi kabisa jamii yetu imeoza na hata wale viongozi kule juu akiwemo Kamishna Renatus Chalamila, ni taswira iliyoko huku kondeni. Kama CCP leo hii imegubigwa na vikwazo vya ajira mpaka vijana wetu watoe rushwa ina maana mfumo wetu wa kutumia rasilimali watu umegubikwa na maadili duni. Wengi wanatoa ajira kwa misingi ya jinsia, wajihi, rushwa, na kadhalika.

Kwa namna nyingine sio sifa nzuri kwa Jeshi letu adhimu la Polisi. Mwanazuoni wa masuala ya kijeshi Sun Tzu kwenye kitabu chake cha ‘The Art of War” anasema kama jeshi likiingia vitani kisha likapoteza mwelekeo basi wakulaumiwa ni Jenerali wa jeshi husikal Sun Tzu anasema iwapo jeshi likiwa kwenye gwaride linatii maagizo yote; kushoto geuka, kulia geuka, au mbelee tembeaaaa!

Waziri Nchimbi
Iweje jeshi hilo likapoteza umahiri huo ndani ya uwanja wa vita. Bahati mbaya Sun Tzu alisahau kuwa katika uwanja wa vita kuna matukio ambayo yanaweza kubadilisha mwelekeo au tabia za jeshi. Kama mwanajeshi hakuwa thabiti licha ya mafunzo yake, basi haitashangaza kuona siku moja akishindwa kuingia uwanja vita sababu tu ya kukosa misingi binafsi ya kulitumikia jeshi.

KWANINI JESHI LA POLISI LIWE NYENZO?
Moja makosa makubwa yanayofanyika katika jamii yetu ni kushindwa kuelewa watoto wetu wanatakiwa kufanya kazi gani katika maisha yao. Wapo wazazi ambao hawajui na watoto nao hawajui wafanye kazi gani hata wanapofika kidato cha nne. Wengi wao wakishapata matokeo ya mitihani yao ndipo huanza kujiuliza wafanye kazi gani.

Kwa Makuruta 95 waliokubali kutoa rushwa ina maana kuwa walikuwa wanataka kulitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanya kazi nyingine hapo baadaye. Mtu makini akichambua hili na kuangalia mwenendo wetu kwa Jeshi la Polisi, wapo wanaojiunga sio sababu ya mapenzi yao bali kwakuwa wanataka ‘kutoka’ kimaisha hivyo mwelekeo uliopo ni CCP Moshi. Sina shaka kabisa, Jeshi la Polisi linaweza kufanya uchunguzi wa mambo mbalimbali ikiwemo hili. Ni rahisi kukukotoa idadi ya wahitimu wa Jeshi la Polisi kila mwaka na wanakopelekwa na muda wao kazini.

Kisha Jeshi la Polisi linaweza kuanza kufuatilia wahitimu hao kama wameendelea na kazi ya Upolisi kwa muda gani na wanafanya nini baada ya kujiondoa katika jeshi la Polisi. Ninasema hivi kwakuwa katika nyakazi zetu Jeshi la Polisi kwa baadhi ya watu wanatafsiri kama sehemu ambayo wanakwenda vijana walioshindwa maisha hivyo kwa muda fulani wanajua wataweza kupata nyenzo ya kufanya kazi nyingine.

Ni wazi wengi waliowahi kujiunga Jeshi la Polisi kwa uadilifu wamedumu na wanaendelea kuheshimu taalumu yao. Lakini wapo wengine wanalitumia Jeshi la Polisi kama nyenzo ya kufanikisha mipango ya maisha. Ni kweli wana haki, lakini hawa vijana wetu baadhi yao wanaweza kabisa kuwa ndani ya jeshi la Polisi kisha baadaye wakipata njia za kufanya shughuli nyingine (baada ya kuelimishwa na au kulifanya jeshi kuwa mtaji).

Endapo Jeshi la Polisi limeweza kugundua Makuruta 95 wameingia kwa rushwa safari hii ni vema likafanya uchuguzi mwingine juu ya wahitimu wake na vituo vyao vya kazi. 

HASARA
Hakuna hasara kubwa kama watu kutumia idara za usalama kama nyenzo ya kufanikisha mipango yao. Tunahitaji askari waadilifu na wenye kuipenda kazi yao. Tunahitaji watu ambao sio tu watakuwa wakilalamikia mishahara midogo bali kutumia kidogo hicho kwa uadilifu na kulinda maslahi ya nchi yetu.

Lakini hakuna hasara kubwa inayotokea kama kitendo cha Makuruta 95 hao au wale waliowahi kupitia CCP Moshi na kadhalika wanaoingia maisha ya kawaida ya mtaani. Katika mazingira haya, “hisia” za ongezeko la Uhalifu haliwezi kukosekana kabisa. Na ili kukabiliana nalo ni vema kutafuta njia mwafaka za mkunusuru Jeshi letu la Polisi ili lisiwe na linakusanya tu kama kokoro na kujikuta limejaza askari wasiowaadilifu.

Ni mbaya, na hatutakuwa tumeokoa jamii inayoamua kufikiria RUSHWA kwanza ndipo ipate ajira. Ni vyema katika tukio la Makuruta waliofukuzwa wafuatiliwe na kuhojiwa zaidi, na iwapo wazazi wao walihusika kuchochea (kama) basi nao wanatakiwa kupitiwa na mkono wa sheria. Kuwafukuza Makuruta pekee hakutoshi mheshimiwa Waziri Nchimbi. Nimemaliza.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako