December 03, 2013

ZIWA NYASA LAPOTEZA TANI 74,000 ZA SAMAKINa Nora Damian, Dar es Salaam
UVUVI ni mojawapo ya sekta muhimu ambayo huchangia upatikanaji wa lishe bora, ajira, kipato kwa wananchi, kuongeza pato la taifa na kupunguza umaskini kwa ujumla.

Kwa kiasi kikubwa shughuli za uvuvi zimekuwa zikifanywa kwenye mito, mabwawa, ziwa na Bahari ya Hindi.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani, imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwamo za maziwa, ambazo zimekuwa zikitumika kwa shughuli za uvuzi na nyingine za maendeleo.
Miongoni mwa maziwa hayo ni Ziwa Nyasa, ambalo ni kati ya maziwa makubwa ya Afrika Mashariki linalopatikana katika nchi za Tanzania, Malawi na Msumbiji.
Kwa siku za hivi karibuni, kumekuwapo mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, ambapo Malawi inadai kuwa maji yote hadi upande wa Tanzania ni sehemu ya eneo lake la kitaifa, huku Tanzania nayo ikidai kuwa mpaka uwepo katikati kufuatana na uzoefu wa kimataifa.
Hata hivyo, licha ya mgogoro huo bado shughuli za uvuvi zimeendelea kufanyika kila siku.
Inaelezwa kuwa, ziwa hilo lina aina nyingi ya samaki lakini aina chache tu ndizo zinazovuliwa kama chakula, lakini aina mbalimbali hukamatwa na kuuzwa nje ya Afrika kwa wapenzi wa samaki.
Hivi karibuni, Wilaya ya Nyasa ilifanya harambee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukusanya fedha zakusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo sekta ya uvuvi.
Akizungumza katika harambee hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Ernest Kahindi anasema licha ya kuwa na rasilimali muhimu kama ziwa hilo, mito, misitu na nyinginezo, bado wilaya iko kwenye umasikini mkubwa.
“Wilaya yetu haina zao maalumu la biashara na wengi wanategemea Ziwa Nyasa kwa ajili ya kuendesha maisha yao, lakini bado utajiri huo haujawanufaisha,” anasema Kahindi.
Anasema ziwa lina uwezo wa kuzalisha tani 81,000 za samaki kwa mwaka lakini hivi sasa linazalisha tani 6,500 tu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, baadhi ya samaki wanaopatikana katika ziwa hilo ni Mandongo, Ntaka, Vitui, Ngorokoro, Dagaa, Kambale na Mbasa.
Anasema sababu kubwa inayochangia upatikanaji mdogo wa samaki ni ukosefu wa dhana za uvuvi za kisasa, ambazo zina uwezo wa kuvua kina kirefu na kwenda hata maeneo ya mbali.
Pia inaelezwa kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia makokoro, nyavu za macho madogo, uvuvi wa sumu na uvuvi wa mabomu.
Anasema kwa sasa kuna mitumbwi ya kuchonga 1,550, mitumbwi ya kujenga 74 na boti za injini 20 vifaa ambavyo haviwezeshi kupatikana kwa samaki wengi kutokana na kutokuwa vya kisasa.
“Ziwa bado halijafanyiwa utafiti wa kutosha lakini ni rasilimali muhimu ambayo inaweza kuinua maisha ya wananchi na ukuaji wa uchumi,” anasema.
Kulingana na takwimu za mwaka jana, zinaonesha kuwa tani 6,500 zilizovuliwa mwaka jana katika ziwa hilo ziliingiza Sh bilioni 4.5.
Kahindi anasema uwepo wa magugu maji upande wa Malawi nayo ni sababu inayochangia uharibifu wa ziwa hilo na kwamba kunahitajika hatua za haraka kuyazuia kwa sababu yanaenea kwa haraka.
Magugu maji ni mmea unaoota majini ambao huwa na rangi ya kijani ambayo huelea majini na wakati mwingine huweza kukwama katika vyanzo vya maji na kuharibu mazalia ya viumbe hai hasa samaki.
Anasema mikakati waliyonayo ni kuhamasisha wananchi kuachana na uvuzi wa hatari, kununua boti za kisasa na vifaa vingine vya kisasa ambavyo vitawawezesha wavuvi kwenda umbali wa zaidi ya kilometa mbili zaidi na kuvua kwenye kina kirefu.
“Mikakati hii inalenga kuwahamasisha wavuvi kutumia maarifa ya kisasa ya uvuvi ili kuongeza ufanisi na mapato yao, kutengeneza mazingira mazuri yatakayosaidia upatikanaji wa zana za kisasa za uvuvi bila vikwazo, kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kusindika samaki na umuhimu wa kuelimisha wananchi juu ya kupambana na uvuvi haramu.
“Kama haya yakifanyika, uzalishaji wa samaki utaongezeka kutoka tani 6,500 hadi tani 81,000 kwa mwaka na hivyo kuongeza pato la wananchi na kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla,” anasema.

1 comment:

  1. eeehhh jamani sasa itakuwaje bila samaki...Nukuu "Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, baadhi ya samaki wanaopatikana katika ziwa hilo ni Mandongo, Ntaka, Vitui, Ngorokoro, Dagaa, Kambale na Mbasa" nimekumbuka mbali kweli haya majina ya samaki

    ReplyDelete

Maoni yako