November 10, 2013

HALI TETE CHUO CHA UALIMU SONGEANa, Stephano Mango, Songea
Ni takribani miezi nane sasa tangu nianze kufuatilia uendeshaji wa chuo cha Ualimu Songea kama kinaweza kuendana na kauli mbiu ya sasa ya Serikali ya Big Result Now (Matokeo Makubwa Sasa). Nimelazimika kukifuatilia Chuo hicho kutokana na mgogoro mkubwa uliopo kati ya wafanyakazi (wakufunzi) na mkuu wao wa chuo Ubaya Suleiman.

Mgogoro huo umetokana na uongozi mbovu usiozingatia misingi ya uongozi na Demokrasia katika vyuo vya ualimu Tanzania kwani Mkuu huyo wa chuo amekuwa na lugha za matusi,vitisho kwa wafanyakazi na wanachuo, kutopokea ushauri kwa washauri wake, mbinafsi, kutowaamini watendaji wake kwa nafasi alizowateua, kufanya kazi kwa kutumia vyanzo visivyo rasmi,

Matumizi mabaya ya fedha za Serikali na vyombo vya usafiri. Pamoja na hayo mkuu huyo wa chuo amediriki kuwapeleka baadhi ya wafanyakazi wake kwenye vyombo vya dola (polisi) (kuwatishia) akiwatuhumu kuwa wanataka kumuua. Baada ya mgogoro huo kutopata suluhu kupitia vikao vya ndani, Jitihada zifuatazo zilifanyika na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuleta hali ya amani na utulivu wa chuo;

Tarehe 27/04/2013 walifanya kikao na mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, tarehe 15/05/2013 na tarehe 01/06/2013 walifanya kikao na Bodi ya ushauri ya Chuo, hata hivyo suluhu ya mgogoro huo haikupatikana.

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome aliunda tume ya watu watano ikiongozwa na Mkaguzi Mkuu wa shule na vyuo wa nyanda za juu kusini ambaye alifahamika kwa jina moja la Lyapambile, kuja kufanya utafiti wa chanzo cha mgogoro, lakini mpaka sasa tume hiyo haijatoa majibu ya uchunguzi wa jambo hilo

Tume hiyo haikuishia hapo tarehe 13/08/2013 wafanyakazi walifanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, ambaye baada ya kusikiliza mgogoro huo aliahidi kuleta suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo ili kuleta amani na utulivu(peace and Tranquility) chuoni hapo. Lakini cha kushangaza hadi sasa yapata miezi mitatu hakuna kilichofanyika hali ambayo imeendelea kuwavunja moyo wafanyakazi wa chuo hicho.

Licha ya jitihada zilizofanywa, Mkuu huyo wa Chuo Ubaya Suleiman anaendelea kuwanyanyasa wafanyakazi wake na kusema pigeni kelele lakini wakuning’oa mimi hapa hayupo na lugha zingine ambazo sio za ustaarabu anazitoa, na kuwafanya wafanyakazi wenzake wahoji nguvu aliyonayo katika utendaji, mfano wa lugha zake mbovu ni “kwani mizizi yangu ni mirefu”. Kitendo hicho kinawafanya wafanyakazi wa chuo na wadau wengine watilie mashaka juu ya sifa za uteuzi wake kushika nafasi kubwa kama hiyo.

Tunamuomba Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Shukuru Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo kumuondoa mkuu huyo wa chuo madarakani na kumtafutia shughuli nyingine ya kufanya kwa ustawi wa chuo cha ualimu songea, taaluma ya ualimu Tanzania na ili kuleta ufanisi wa kauli mbiu ya serikali ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now)

Sababu zinazopelekea hilo ni nyingi ila kwa sasa nitazitaja chache ili kuweka kumbukumbu sawa, ya kwanza Novemba 1, 2013 Mkuu huyo wa chuo bila kuwasiliana na Mtaaluma wake wa Chuo Maiko Luoga, alidiriki kuwaandikia Barua Wakufunzi kuwataka watunge Mtihani wa Moko wa Ualimu viwango vya Baraza la Taifa la Mitihani(NECTA) kwa lugha ya kejeri hali ambayo imesababisha maudhi na utulivu wa akili miongoni mwa wafanyakazi katika kufanikisha utungaji wa mitihani hiyo

Kitendo hicho licha ya kuwa ni kinyume na utawala bora , lakini pia kimekiuka maagizo ya Bodi ya Chuo ambayo yalitolewa tarehe 28/8/2013 (……. mambo yote yanayohusu fedha yaendeshwe kwa uwazi na ushirikishwaji mkubwa miongoni mwa wanaidara / taasisi kwani inaonekana mambo yanaenda kwa usiri mno).

Sababu ya pili amekuwa na vitisho vingi katika utendaji wake na maneno ya kuudhi dhidi ya viongozi wenzake , mfano wa maneno yake ambayo anayatamka huku akigonga meza kuashiria ubabe na kiburi cha madaraka ni kama vile,(…. Ukiingia ndani ya kumi na nane zangu nakumaliza, Angalieni msije mkaumia wengine tunambavu za chuma, Nipo tayari kuua inzi kwenye kioo cha TV hata kama itavunjika potelea mbalimbali raha yangu ni kuhakikisha inzi amekufa, Mkitoboa mtumbwi nitahakikisha kabla sijazama mimi nawazamisha ninyi kwanza, Angalia wengine watakaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno watafune, Amekuwa akitishia kung’oa mtu kwa kumwendea (kumpandia)wizarani ndani ya siku mbili na kumchukulia barua ya uhamisho kwenda vyuo vya pembezoni mwa Tanzania, Mimi nafanya haya hata niking’olewa kwa muda mfupi potelea pote nitakuwa nimejenga historia).

Sababu ya tatu ni kutokuwa na uwazi, ukweli na ushirikishwaji kwa njia ya kidemokrasia miongoni mwa idara zake katika chuo hicho na hasa katika fedha ambazo zinakuja kwa ajiri ya manunuzi ya vitu mbalimbali, fedha ya kuendeshea mafunzo ya ualimu kwa vitendo(BTP)

Fedha hiyo licha ya kuchelewesha kuitoa kutokana na ufisadi wake lakini pia hakuitoa yote na wala hakueleza kwa uwazi na ukweli, hali ambayo haikuwezesha wakufunzi kwenda kufanya kazi stahiki kwenye maeneo kusudiwa ya kuwatahini wanachuo ambao walikwenda kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo.

Sababu ya nne ni uwezo wake wa kiuongozi kwani kumekuwepo na mashaka mengi katika Wasifu wake wa kielimu na kiutendaji, hali inayopelekea kuendesha Chuo katika misingi binafsi bila kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu za Wizara.

Kutokana na hayo yote Chuo hicho kimejikuta kikiingia kwenye mgogoro wa muda mrefu na mkubwa na kupelekea shughuli zote za kiutendaji chuoni hapo kutofanyika katika viwango vyenye ubora na kwa wakati na hasa pale anaposafiri mambo huwa yanasimama, kwani mara nyingi utendaji wote anaufanya yeye mwenyewe na wakati mwingine huwa anajiita Chief Accountant na kumuona Makamu wake kuwa hana uwezo wala mamlaka ya kutoa maamuzi kwa mustakabali wa chuo

Ni mengi ambayo nimeyabaini na ushaidi upo wazi kuwa Mkuu huyo wa Chuo hafai kuendelea kuongoza Chuo hicho kwani Wakufunzi, Wafanyakazi na Wanachuo hawana imani nae, na wanafanya mambo mengi bila morari ya utendaji kutokana na mazingira mabovu ya utendaji kazi katika chuo hicho

Nimefanya jitihada za kukutana na baadhi ya Wakuu wa Idara Chuoni hapo na kupata majibu ambayo yanaonyesha ukataji wa tamaa kutokana na mazingira mabovu ya kiutawala ambayo yanaonyeshwa na Mkuu wa Chuo hicho katika kufanikisha mpango mkakati wa matokeo makubwa sasa,

Pia nimebahatika kuwauliza viongozi wa Bodi akiwemu Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo ambaye amejitambulisha kwa jina la H,Lugome naye pia ameonyesha masikitiko makubwa sana juu ya utendaji wa Mkuu wa Chuo hicho
Lakini pia Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti ambaye pia ameshiriki kusuluhisha mgogoro huo katika kikao chake cha April 27, 2013 lakini ameshindwa na kukata rufaa kwa kulipeleka swala hilo kwa Mkuu wa Mkoa ili aweze kuliingilia kati

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu Philipo Mulugo alipo tafutwa kupitia simu yake ye kiganjani yenye namba hii 0754315922 alijibu kuwa swala hilo bado halijafika mezani kwake na endapo likifika basi atachukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria dhidi ya Mkuu yoyote wa Chuo ambaye atakwamisha malengo na ufanisi wa kazi nchini

Kutokana na hayo na mengine mengi ni dhahiri kuwa utendaji wa kazi katika chuo cha Ualimu Songea kilichopo eneo la Matogoro Mkoani Ruvuma wilayani Songea ni mgumu miongoni mwa Wafanyakazi na kusababisha hali ya sintofahamu katika Saikolojia zao na mustakabali wa Elimu ya wanachuo

Ni vema sasa mamlaka zinazohusika zikachukua hatua stahiki za kumaliza mgogoro huo ikiwemo na kumuondoa Mkuu huyo wa Chuo ili kurudisha Amani na Utulivu chuoni hapo miongoni mwa wanajumuia wanaokizunguka chuo hicho ili kuweza kufanikisha mikakati mbalimbali iliyopo nchini ya kuhakikisha kuwa elimu bora inafikiwa nchini hapa

Mwandishi wa Makala hii anapatika kwa 0755-335051 AU 0715-335051
Barua pepe,stephano12mango@yahoo.com
www.stephanomango.blogspot.com
Top of Form
Bottom of Form

No comments:

Post a Comment

Maoni yako