MARKUS MPANGALA (DAR ES SALAAM)
NA HAPPY JOSEPH (CHANGCHUN, JILIN (CHINA).
WAKATI mwingine tunatakiwa
kulalamika ka kila jambo kutokana na muktadha halisi. Tunapaswa kupiga kelele
hata kama hazitakuwa na ufumbuzi, lakini angalau itakuwa inaweka rekodi sawa
kwamba uamuzi uliochukuliwa hakuwa sawa. Kila mmoja anaweza kulalamika,
na serikali inaweza kutuona walalamishi
zaidi, lakini kwangu mimi hili ni zaidi ya ulalamishi. Ni zaidi majuto. Ni
zaidi hisia kali, kwamba tunajenga elimu ya namna gani kwa kizazi kijao.
HAPPY JOSEPH katika pozi. Huyu ndiye nimeshirikiana naye kuandika makala hii kuhusu Elimu. Asante rafiki yangu kwa mawazo mazuri. |
Kwanza tulianza kulalamikia
eti kwamba mitihani ya kidato cha nne kuna watu wanapendelewa. Baadhi ya
watanzania wenzetu wakapayuka mpaka kutoa povu midomoni ati mfumo wa elimu
unawapendelea jamii au watu wa imani fulani. Kwangu mimi huu ulikuwa ujumbe
tosha, matatizo yaliyolimbikizwa sasa yamekuwa shubiri na kusababisha kushindwa
kufikiri sawasawa.
Matatizo tuliyyalea kwa miaka mingi yamesababisha kutafuta
majibu mengine ambayo hayana kichwa wala miguu. Matatizo ambayo yamelelewa kwa
ustadi na kukabidhiwa mikononi mwa shetani (ujinga). Waama, elimu yetu
tumeipeleka mikononi mwa shetani na hilo hakika sitachelea kusema. Akindika
kwenye kitabu chake cha ‘Mwalimu Mkuu wa Watu,” Mzee wetu Pacsally Mayega,
anasema, “Ndani ya kichwa mvivu ni karakana ya shetani, na mtu mvivu ni kama
jiwe lililopakwa mav,”.
Ni maneno mazito ambayo
yanavuta hisia zangu kuona serikali yetu tukufu inadhani ‘Divison V’ ni moja ya
ujanja mbovu kuboresha elimu yetu, badala ya kusema ukweli kwamba hilo ni
daraja sifuri kwa watui waliofeli. Tabu ya nini kufika hili?
Kwanini swerikali inajibebesha mzigo mzito kama huu? Naam, tuko mikononi mwa
shetani, huku Bunge letu tukufu likiidhinisha watanzania kufikishwa kwenye
pango la shetani. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Sifuni Mchome
alitutangazia madaraja mapya kwa mtazano wa serikali.
Zamani tulikuwa na A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F= 0-34
kwa upande wa kidato cha sita A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54,
S=40-44 na F= 0-39. Naam, sasa serikali yetu sikivu imesema madaraja yatakuwa
hivi; A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19, huku
serikali hiyo ikisema kuwa daraja sifuri limeondolewa ili kuweka mlolongo
mzuri.
Waaooooo! Tumefika mahali
kudhani mlolongo mzuri ndiyo mazingira mazuri. Tunashindwa kutibu maradhi na
kuongeza ugonjwa mzito, ambao utatuchukua muda kuondokana nao. Kwamba shida
yetu ilikuwa mlolongo mzuri ama tunatakiwa kupewa elimu bora?
Ni kweli kwamba serikali imefanya vizuri
kutuanzishia sekondari sisi watoto wa masikini tuliokulia ukanda wa ziwa Nyasa
na wengineo kote nchi. Shule za Kata ingawa baadhi yetu hatukusoma lakini
imewasaidia wale tuliowaacha nyuma kwani angalau wamepata elimu hata kama haina
ubora unaotakiwa.
Serikali ya CCM imeamua kwa
dhati kabisa kutupeleka katika dimbwi la tabasamu la shetani na kudhani inaokoa
kizazi hiki. Nchi yetu imeuwa ikijikita sana kwenye suala la Ilani za chama
kama msingi wa maendeleo badala ya sera.
Kilichosababisha kufutwa
mitihani ya kidaoto cha nne ilikuwa Ilani ya CCM si sera ya Taifa letu. Kufutwa
matokeo hakukuwa na maana kutabadilisha lolote kwani serikali yenyewe imejenga
mazingira ya kila ya namna ya kuwa mchochezi namba moja kwa wananchi.
Katika hoja hii nilikumbuka maneno
mazito ya rafiki yangu Happy Joseph aliyeko masomoni mjini Changchun, Jilin, nchini
China akisema, “Hivi kama kocha ameona timu yake haifanyi vizuri (wachezaji
wanapiga mashuti nje ya magoli), ataamua kupanua maagoli katika uwanja wa
mazoezi? Je, katika mashindano na timu nyingine katika uwanja mwingine ategemee
nini?
Anaongeza kwa kusema, “Elimu
ya sasa katika utandawazi huu si ya nchi Fulani, inapaswa kuwa na viwango vya
kimataifa. Lazima mtu ashindane na wa mataifa mengine. Tanzania haiwezi kuwa na
elimu yap eke yake, ndio maana tunapigwa change macho kwenye mikataba na
mataifa mengine,”
Kama walivyo wadau wengine
rafiki huyo huyu anatoa ushauri kwa serikali akisema, “Kwanza, Serikali ikae na
wadau wa elimu kupitia tafiti za kielimu zilizofanywa na taasisi mbali mbali mfano
Haki Elimu kuona matatizo ya elimu ni yapi, na mbinu gani zitumike kupandisha
kiwango cha elimu na si idadi ya ufaulu
hewa. Pili, Serikali kuwekeza zaidi katika elimu; hakuna aisyefahamu kuwa
hakuna Maabara, Maktaba, na walimu wenye nia katika shule za umma. Tatu, Serikali itazame upya mtaala wa elimu,
isiung'ang'anie, pia itazame mfumo wa elimu, kwamba ipi iwe lazima na ipi iwe
ziada.
Aidha, anasema, serikali
itazame maslahi ya Walimu na ubora wake.
Katika pendekezo hilo la mwisho ndiyo linanipa simanzi. Kwamba kujali
maslahi ya Walimu ni suala gumu ambalo serikali imeshindwa kisheria na kiakili
pia. Inaudhi kusema maneno hayo
lakini hakuna namna nyingine, kwamba serikali imeshindwa kisheria japo iliagizwa
hivyo na Mahakama Divisheni ya Kazi wakati ilipozuia mgomo wa Walimu kote
nchini. Katika majadiliano yake na Chama cha Walimu, ilikubaliwa kuwa serikali
itaongeza mishahara kwa kiwango cha asilimia 67.
Lakini katika hali ya
kustaajabisha serikali haikufikia kiwango hicho, bali ilikomea kwenye asilimia
24. Katika mkutano na waandishi wa Habari miezi kadhaa iliyopita, Rais wa Chama
cha Walimu nchini, Gratian Mkoba alisema kuwa jambo hilo liliwasikitisha walimu
huku serikali ikianza harakati za ‘Big Results Now’ ambayo iliitongoa huko
Malaysia.
Nia nzuri ya serikali
haibezwi, lakini kinachogomba ni mtindo unaotumika kuendelea kuwategemea
walewale wanaonyonywa na kudhani wanaweza kuleta mapinduzi. Walimu ndio wahanga
wa unonyaji unaofanywa kwani kwa mujibu wa mazungumzo ya mezani kati yao na
serikali ilikubaliwa malipo yao yafikie asilimia 67 kwa kile kilichoeelezwa
kuwa nchi yetu haina fedha za kutosha.
Labda, lakini kuomba kufika
asilimia 67 kisha kushindwa kutimiza bila sababu zozote hakuna jingine zaidi ya
kufikisha elimu mikononi mwa shetani. Mikono ambayo bila shaka itatuzalishia
magaidi kutokana na ukosefu wa elimu wmafaka na yenye tija kwa maslahi ya taifa
letu. Ni hatari kuichezea elimu kwa kiwango hiki halafu tukatarajia kukutana na
wanazuoni waliokomaa. Asenteni kwa kunisoma.
Baruapepe;
mwanazuoni27@gmail.com
@MAKALA HII IMECHAPISHWA GAZETI LA RAI, Novemba 7, 2013.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako