Na Mwandishi
Wetu, Handeni
MKUU wa wilaya Handeni, DC Muhingo Rweyemamu,
amewataka wananchi wa Handeni, mkoani Tanga kulitumia Tamasha la Handeni
linalotarajiwa kufanyika Desemba 14 mjini hapa kwa ajili ya kutafuta fursa za
kimaendeleo na kuwapatia maisha bora Watanzania wote kwa kupitia sekta ya
utamaduni.
Akizungumza jana mjini Handeni, Muhingo alisema
kutokana na tamasha hilo kufanyika mwisho wa mwaka, Desemba 14, itakuwa chachu
ya kuwaunganisha watu wote, sanjari na kujadili changamoto zinazoikabiri
Handeni na Tanzania kwa ujumla.
Muhingo alisema kuwa tamasha hilo lina umuhimu
mkubwa kutokana na kuandaliwa maalum kwa ajili ya Watanzania kwa ajili ya
kuangalia ngoma na matukio mbalimbali ya kijamii.
“Wakati napongeza kwa dhati kuandaliwa kwa tamasha
hili wilayani hapa, pia nawaomba watu waje kwa wingi kushuhudia namna gani
Handeni imepiga hatua kimaendeleo na kuangalia namna gani wanaweza kusonga
mbele.
“Naamini tutafikia hatua nzuri kwa kushirikiana na
wadau wote, hivyo wale wanaoishi mbali na Handeni pia ni wakati wao kurudi
nyumbani mwishoni mwa mwaka kujifunza mambo ya utamaduni wao, sanjari na
kufanya juhudi za kupiga hatua kimaendeleo,” alisema.
Tamasha hilo linaloandaliwa na Mratibu wake Kambi
Mbwana, hadi sasa limedhamiwa na Phed Trans, Clouds Media Group, Grace
Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles &
Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country
Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group.
Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware,
Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia
kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog,
Jiachie Blog na Taifa Letu.com, huku likipangwa kuanza saa 2 za asubuhi hadi
saa 12 za jioni.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako