January 29, 2014

Dk. Leader Stirling: Mzungu wa kwanza kuwa waziri wa afya Tanzania




Na Markus Mpangala, Dar es salaam

Miongoni mwa majina ambayo yalijitokeza katika baraza la mawaziri lililokuwa linaoongozwa na hayati Mwalimu Nyerere ni Leader Dominic Stirling mwenye asili ya Uskochi (Scotland) aliyekabidhiwa jukumu hilo kati ya mwaka  1975 hadi 1980.
Mzungu huyu alikuwa mtumishi wa wamisionari ambao kwa miaka mingi alikijikita barani afrika wakisambaza imaniya ukristo na sera za mataifa yao. Leader Dominic Stirling alizaliwa januari 19, 1906 mjini Finchley, Uingereza. 

Alianza maisha katika kitongoji cha Sussex Weald, baadaye alijiunga chuo cha Stortford na chuo kikuu cha London kisha aliteuliwa kuja kufanya kazi barani Afrika, ndipo akaletwa hapa nchini.
Miaka 14 aliishi mji wa Lulindi uliopo wilaya ya Masasi akiwa utumishi wa shirika la Benedictine Mission huku akiendelea na kazi yake ya utabibu chini ya Dk. Frances Taylor.
Dk. Taylor na Leader Stirling walikuwa wasimamizi wa Hospitali ya Kanisa Katoliki wilayani Masasi. Alifanikisha ujenzi wa hospitali za Lulindi na Newala, na kufanikiwa kuwa na vitanda 50 katika kipindi amabcho Tanganyika ilikuwa na ongezeko kubwa la watu.
Aidha alipelekwa katika hospitali ya Luatala. Ambako alifanikisha ujenzi wa wodi nne za wagonjwa. Hata hivyo hospitali hizo zilimudu kupokea wagonjwa 300 hadi 400 na wakati mwingine walifika 500. Baadaye alipelekwa Kibosho, mkoani Kilimanjaro ambako aliishi kwa miaka mitano kuanzia 1964 hadi 1969.

Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mbunge ambako alidumu kwa miaka 22. Katika miaka yake mitano ya mwisho ya ubunge aliteuliwa kuwa waziri wa afya na Mwalimu Nyerere.
Licha ya kujihusisha na masuala la utabibu na siasa kupitia bunge, pia Stirling aliongoza kikosi cha Skauti hadi mwaka 1962 kabla ya muungano wa jamhuri ya Tanzania. 

Kwa mara ya kwanza Leader Stirling aliwasili, Zanzibar kama kituo chake cha kwanza barani Afrika kisha akaletwa upanda wa Tanzania bara (zamani Tanganyika). 

Lakini kuna simulizi nyingine ya kusisimua kuhusu Dk Stirling, kwamba alikuwa muumini wa kanisa la Anglikani kabla ya kuacha na kujiunga na Kanisa Katoliki. 

Kama inavyojulikana kwamba Uingereza ndiyo taifa lililoasisi kanisa la Anglikana, na wananchi wake wengi ni waumini wa kanisa hilo. Mwaka 1948 Dk. Leader Stirling, Fr. Birch na makasisi wengine watano waliamua kuachana na kanisa la Anglikana na jumuiya yake iliyokuwa Afrika (UMCA) na kujiunga kanisa Katoliki na baadaye kuanzia kikosi cha Skauti. 

Mara baada ya kujiunga na Kanisa Katoliki, Dk Leader Stirling alianza kufanya kazi katika hospitali ya Mnero iliyomilikiwa na shirika la Benedictine Mission.  Baadaye alianzisha shule ya chekechea akiwa na mipango ya kuendeleza kazi za Skauti na akaongeza nguvu kujihusisha na masuala ya siasa. 

Dk. Leader Stirling na uwaziri wa afya
Kufuatia siasa za nchi kuwa katika mihemko zaidi aliombwa na ofisi ya rais kwenda Dar es salaam ambapo aliambiwa ni kwa sababu ya utoaji huduma za afya.
Lakini kwa asili Dk Leader Stirling alipenda siasa tangu akiwa na miaka 18, hivyo kuitika wito wa kwenda Dar es salaam kwa maombi ya ofisi ya rais halikuwa jambo la kushangaza kwake. 

Ndipo mwaka 1958 akiwa na miaka 52 alitoa hotuba yake kwa mara ya kwanza Mnero chini ya uenyekiti wa Mwalimu Nyerere. Tabibu huyo alivutiwa na harakati za chama cha TANU, ambacho kilikwua kikiwani uongozi katika uchaguzi wa mwaka 1958.
Ulikuwa mwaka huo ndipo Dk Leader Stirling alipita bila kupingwa kuwa mbunge na alipaswa kugombea tena mwaka 1960 kama moja ya makubaliano ya kupatikana uhuru wa Tanganyika. 

Majimbo mawili yalikuwa yanahitaji mgombea; Mbeya na Chunya kwa tiketi ya TANU. Dk Stirling alichukua jukumu hilo kwa unyenyekevu kutokana na chama cha TANU kuhitaji mgombea mmoja ambaye angewakilisha jamii ya kizungu katika uchaguzi mkuu.
Dk Stirling alifanikwia kutetea kiti chake mwaka 1960 na kufanikiwa kutumikia bunge na kazi ya udaktari. Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 alidumu kuwa mbunge mpaka mwaka 1965 ikiwa na maana ya kipindi cha miaka mitano pekee. 

Katika kipindi chake cha uwaziri alishiriki mipango mbalimbali ya maendeleo ya huduma za afya za taifa ikiwemo mjumbe wa bodi ya chakula. Lakini kuna rekodi moja ya kusisimua, Dk. Leader Stirling alishindwa katika uchaguzi na nafasi yake kurudi bungeni ikaota mbawa mwaka 1979.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako