January 18, 2018

HAKUNA CHAMA KINACHOENDESHA MAISHA YA MPIGA KURA.

NA HONORIUS MPANGALA, BAHI
NILIPOKUWA mdogo niliamini maisha ni jambo ambalo liko tofauti na la kuogofya sana katika jamii. Sababu kubwa ni pale nilipokuwa nayasikia maneno kama “Usicheze na maisha”. Fikra zangu zilinipeleka kuwa maisha ni jitu linalotisha sana katika jamii.

Baada ya makuzi nikapata misemo kama “Maisha yenyewe ndiyo haya haya” nikaanza kutambua kumbe mwenendo wa kuanzia asubuhi unaamka hadi usiku unaingia kulala hizi harakati zote ufanyazo ndiyo maisha yenyewe.

Katika vipindi ambavyo wapiga kura na wananchi wa kawaida toka vyama vya siasa wanajiona kama na wao ni wenyechama basi ni katika kampeni za uchaguzi. Kipindi hiki kila mwanachama anajiita ni mwenyechama. Ni kipindi ambacho watu hao hudiriki kunukuu maneno ya wagombea wao na kuiaminisha hadhira aliyonayo kuwa chama chetu kitatekeleza mambo kadha wa kadha.


Licha ya elimu inayotuambia siasa ni sayansi wako sahihi kwa yale wanayoyafanya katika mikakati ya kufanikiwa katika siasa. Niliwahi kuambiwa na Mzee mmoja ambaye  alikuwa Mwenyekiti wa tawi wa chama fulani cha siasa kuwa hata uchawi ni sayansi pia, ila uchawi wa kizungu ni wa faida zaidi kuliko huu wa kiafrika. 

Hivyo hata mimi naweza kuamini siasa ni sayansi kwa wenzetu wa mataifa yaliyoendelea lakini kwa nchi za kiafrika ambako demokrasia tunaiga sioni kama siasa ni sayansi.
Vyama vya siasa vimekuwa na kawaida ya kuwatumia wanachama au wapiga kura kwa ujumla kama Makarai kwa fundi muashi. Karai hukumbukwa wakati wa kuwekewa “UdongoUlaya” na “UdongoAfrika” wakati wa ujenzi na litahifadhika vyema sana hadi ujenzi uishe lakini mara baada ya kukamilika ujenzi utalikuta karai halikusafishwa lilipomaliza kazi yake na limetelekezwa katika maeneo ambayo siyo ya kuthaminika tena.

Wapiga kura na wanachama wa vyama vya siasa wamekuwa na mitazamo tofauti sana wakati wa kampeni. Pia kumekuwa na mizuka inayokuja bila kutarajiwa wakati huo ambao unaweza kuwakuta hata wafuasi wakigombana kwasababu ya kutetea vyama vya huku wenyechama wakiwa katika Viti vya kuzunguka na hawajui kwa namna gani mfuasi umepigwa au kuumizwa na juhudi za kukitetea chama chako.

Vilemba, kofia, Fulana, kanga, vitenge na vidani vya mkononi vimekuwa kama sehemu ya kuelezea mtu ni mfuasi wa chama gani. Licha ya kukisemea sana chama unakuta maisha ya hao waliokuwa wananadi chama chao Kwa kunukuu maneno matamu na yenye matumaini ya maisha wakiwa wamechoka na maisha na kutaabika sana.

Kitu wanachosahau watu ni kwamba hawakujua kuwa maisha yao ni yao hayana uhusiano wowote na kiongozi wa kisiasa ambaye alipata kazi hiyo kuwekewa alama ya vema labda atakuwa msaada wa kuleta chumvi na sukari kama ilivyofanyika usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi.

Kauli za kusema vyuma vimekaza huwa najiuliza kukaza huko anakaza kiongozi kiasi kwamba mtu akashindwa kwenda shambani kulima na hatimaye akaja akauza mazao yake? Tatizo ni maisha ya utegemezi ambayo wote tumeyazoea kuwa kila kitu kinaendana na utegemezi kutoka katika serikali. Sasa inapokuja suala la kukutaka ujiendeshe mwenyewe kimaisha ndipo tunapolitupilia mbali suala la ugumu wake kwa aliyechaguliwa kuwa kiongozi. Tatizo ni kuchukua na kumeza maneno ya wakati wa kampeni na kufikiri kuwa ndiyo uhalisia wa maisha utakuwa hivyo.

Nimesimamia chaguzi mbili yaani wa mwaka 2010 na ule w mwaka 2015 nikiwa Mkoa wa Mbeya. Nazikumbuka kampeni zile lakini niliporejea maeneo yale Julai mwaka 2017, nikakuta mazungumzo tofauti toka kwa watu walioonekana ni wenyechama wakati wa kampeni za uchaguzi wakasahau kama wao ni wanachama tu. 

Kwavile fikra na mitazamo yao na mimi iko tofauti katika suala la kuiona siasa ndiyo kila kitu nilibaki kukaa kimya huku nikitasabamu wakati wenzangu wakiwa wanazungumza kwa kusikitikia hali iliyopo ni ngumu kimaisha. Nilipoulizwa mbona kama unacheka jibu langu lilikuwa nilikataa kuishi kwa kutegemea masuala ya kisiasa kuwa ndiyo muafaka ya utatuzi wa maisha yangu. Palepale nikawaambia nendeni bustanini mkalime nyanya au vitunguu bei iko vizuri sokoni.

Nikawaambia jinsi ufuta unavyotafutwa nyakati hizo. Nikawaeleza juu ya faida kilimo cha biashara. Nilipowaambia mwanamuziki wa Bongo Fleva, Seleman Msindi au maarufu kwa jina la Afande Sele wa Mkoani Morogoro sasa hivi yuko shambani analima Pilipilihoho, Bamia,Matikiti,Karoti,Nyanya, Vitungu na Mbogamboga (Horticulture) na anauza walishangaa. 

Niliwapa mfano wa Afande Sele kwasababu alikuwa ameingia katika siasa na kugombea ubunge kupitia ACT-Wazalendo jimbo la Morogoro Mjini lakini baadaye alipogundua mitazamo yake inakinzana na uhalisia wa siasa iliyopo akaamua kujiweka kando.

Laiti kama tungelijua kama wenyechama wanawaona wanachama kama Makarai wakati wa ujenzi basi sidhani kama wangefikia hatua ya kulalamikia mamlaka mbalimbali katika ugumu wa maisha wanayoyasema.

Mnufaika namba moja katika masuala ya siasa katika uongozi anaweza kuwa mwanafamilia ya kiongozi. Lakini wengine wataishia kukutana na lugha nzuri ambayo itawafanya waamini kukosea ni jambo ambalo lipo. Ujanja wa kitumia maandiko ya kwenye vitabu vitakatifu na uhalisia wa wananchi wanaojifanya kuzijua dini huingia miguu yote miwili na kuamini kuwa hata Mungu alisema samehe saba mara sabini.

Si ajabu kuona wanasiasa wakijifanya kujihusisha na masuala ya Mungu baada ya kuwa viongozi wakati hapo awali wakati wa kutafuta walipishana kwa waganga wa kienyeji kama magari yanayopishana Ubungo mataa huko Dar es salaam.

Utegemezi wa maisha ya kufikiri wanasiasa ndio watakao kuletea sukari, sabuni na chumvi kama wanavyowahadaa siku kadhaa kabla ya uchaguzi ndio kitu kinachowafanya wengi wafikiri kuwa maisha yapo hivyo kupitia uongozi wa mgombea husika.

Aliyekuja na kauli ya ‘pambana na hali yako’ natamani nimjue walao nimwagizie zawadi kwa ubunifu. Maana uhalisia wa alichokisema ndiyo unaotakiwa katika maisha kamwe usitegemee kuweka bango hata katika milango ya maskani yenu itafanya ugumu ulionao wa maisha upungue kwa kutazama picha.

Kuna kijana aliyebandika bango la mgombea fulani katika mlango wake katika kibanda chake cha biashara mkoani Mbeya. Naye alijiona ni mwenyechama kwa wakati ule kwani aliitwa na viongozi wa eneo lile na kupewa posho ya kusambazia vijana wenzake. 

Siku aliponieleza uzuri wa bango lile kukaa pale nikamwambia watumie kwa akili hao jamaa zako kwani maisha baada ya uchaguzi wenzako watakuwa wanaonyesha Pikipiki walizopewa halafu wewe utakuwa umebaki kama ulivyo na bango lako. Na huo ndo uhalisia ulitokea maisha yamekuwa yaleyale. Maeneo ni yaleyale kwa mtu yuleyule. Hii ndio siasa ya kiafrika ya utegemezi wa fikra na mitazamo kwa kutoka kwa wanasiasa.

Kila mmoja aichunguze njia yake ya kutafuta maisha lakini kuna wale wanaoingia kichwa kichwa bila kujua uhalisia wa kile wanachokihitaji kama kitapatikana kwa njia zipi. Bibi zetu na babu zetu kule vijijini wanapokuwa wanapokuwa na masimulizi ya hii nchi ilikotoka utaona wanakuambia shika jembe ukalime ni kama wanatambua msingi wa maisha uko katika mikono na kichwa chako na sio mwanasiasa.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako