January 04, 2018

ITIKADI HAIELEWEKI, SIASA YA UTAIFA HAIPENDWI

NA MARKUS MPANGALA
KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu wananchi wake kuwa wanachama wa chama cha siasa. Ni suala la uhuru wa kuchagua. Utashi wa mwanadamu pia unamfanya awe mwanachama, mfuasi au mtu yeyote mwenye kuamini kuwa ili awe mkamilifu lazima ajiunge na chama cha siasa.
Vyama vya siasa vimevuna wanachama kwa mtindi mwingi, ikiwemo mikutano, wanasiasa, familia,pamoja na ununuzi wa wanasiasa kutoka upande wowote.
Katika eneo hili wanachama na wanasiasa wote hupendelea sana kushabikia itikadi ya chama chao. Labda niseme kwanza maana ya Itikadi katika vyama vya siasa (hoja hii haitajikita kwenye upande mwingine wa itikadi). Wataalamu wa masuala ya sayansi ya siasa wanatuambia kuwa Itikadi ni mkusanyiko wa imani unaoshikiliwa au kuaminiwa na kikundi cha watu fulani. Kwahiyo Itikadi ni imani au mawazo fulani ambayo ni misingi ya nadharia za mfumo wa kisiasa au kiuchumi.


Kuna aina kuu mbili za itikadi:- itikadi za kisiasa, na itikadi za kiepistemolojia (ambazo ni sehemu ya falsafa inayohusu utafiti wa jinsi tunavyojua mambo).
Itikadi ya kisiasa ni upangiliaji unaohusu mawazo ya kimaadili na vipi nchi itaendeshwa. Itikadi za kiepistemolojia ni upangiliaji unaohusu mawazo ya kifalsafa, ulimwengu, na jinsi gani watu wanapaswa kufanya maamuzi. Kuna aina nyingi za itikadi. Moja kati ya hizo ni pamoja na Ukomunisti, Usoshalisti, na ubepari ni itikadi kubwa sana za kiuchumi na kisiasa kwa ujumla.

Wanachama wengi hufuata itikadi ya chama na au wengine kuvutiwa na mwanasiasa au kiongozi wa chama cha siasa bila kujali itikadi inayoongoza chama chenyewe.Ndiyo kusema chama kinaweza kuwa na kundi kubwa la wanachama lakini wasiwe na mafungamano na itikadi yake inayoongoza. Hilo linaweza kutolewa mfano kwa namna wanasiasa wanavyohama kutoka chama kimoja kwenda kingine. 

Au namna wanachama wanavyovutiwa na mwanasiasa wa chama fulani pasipo kutaka kujua itikadi ya chama alichomo mwanasiasa husika. Mwanasiasa huyo akihama chama A kwenda chama B kunakuwa na kundi fulani ya watu wanaoamini walikuwapo katika chama hicho kwasababu yake.

Wakati fulani tumewahi kuhabarishwa kuwa mwanasiasa fulani katika mkoa mmoja amehama chama fulani pamoja na wanachama 80 au chukulia namna Augustine mrema alipojiondoa CCM na kujiunga vyama vya upinzani, utaona kila chama amekuwa akihamia na kundi fulani la wanachama.

Swali la kujiuliza kwanini hao wanachama (hata kama hawakufikia idadi hiyo au kuwa habari ya uongo) wanamfuata mwanasiasa huyo kila aendeko?Kwamba wanachama wanaohamia chama A kutoka chama B kwasababu za kimaslahi au mtu. Ipo dhana nyingine kuhusiana na ukweli katika vyama vya siasa. kwa mfano, wanachama wanaojiunga na chama A kwasababu ya hasira, ghadhabu na uonevu dhidi ya kundi jingine.

Kwa mfano mwanasiasa anaweza kuhamasisha wafuasi wake wajiunge na chama alichomo ili kutimiza mahitaji yake ya kukikomoa chama B au A. Na mwingine anaweza kufanya hivyo ili kukikomoa chama A au B. Katika mazingira hayo kundi la wanachama A wanaamini kuwa ukweli wa mambo yote kuhusiana na siasa unamilikiwa na kundi lao pekee. 

Wanachama wa kundi A wanajenga fikra kuwa mtu yeyote anayetoka kundi lao ndiye msema ukweli na wanaumiliki ukweli huo kwa mtindo huo. Hali kadhalika wanachama wa kundi B nao wanaamini ukweli unatoka kwa miongoni mwa watu wao.

Tuchukue mfano, kundi la wanachama wa Chadema wanaamini ukweli unatoka katika chama chao,mwanasiasa wao au itikadi yao. Vilevile Kundi la Chama cha Mapinduzi (CCM) linaamini hivyo kuwa ukweli unatoka kwao na wanasiasa wao tu. 

Hali hii inazaa ufuasi na imani kuwa mwanasiasa fulani ndani ya chama hicho anapozungumza bila kujali muktadha au hoja yenyewe, msingi wa kwanza unakuwa kumwamini kwasababu anatoka kundi lao liwe A au B. 

Makundi hayo yamejijengea uhalali kuwa wao ndiyo wenye hatimailiki ya namna ya kuendesha siasa pamoja na kuhakikisha nchi inafuata mkondo wao. Iwapo kunakuwa na kundi jingine la tatu (tuliite C) likawa na mtazamo tofauti dhidi ya makundi hayo mawili (A na B) maana yake watatengwa na kuonekana wenye itikadi tofauti. 

Madhali kundi A na B yamejikita katika upande wao inawawia vigumu wananchi waliopo katika kundi C. hasara mojawapo ya kuelemewa kiasia kwa hatua hiyo ni pale nchi inapokuwa inapambana na nchi nyingine kwa msingi wa uzalendo. 

Mfano, watu wa kundi A na B hawawezi kuungana kwa namna yoyote ile. Tuliwahi kushuhudia hilo katika utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuhusiana na mzozo wetu dhidi ya Rwanda kuhusiana na waasi waliokuwa wakiongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda. 

Aidha, tuliona hilo katika mzozo wa Tanzania dhidi ya Malawi kuhusiana na mpaka wa Ziwa Nyasa. Tuliona hilo katika mizozo kadhaa kati ya Tanzania na Kenya ambapo wanachama wa kundi A na B hawakupatana wala kujali kuwa wanapaswa kupigania siasa za utaifa. 

Tuliona hilo kwneye upigaji wa kura za kuunga mkono au kupinga hatua ya serikali ya Israel kuhamisha makao yake makuu kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalemu kisha kuungwa mkono na rais wa Marekani, Donald Trump. Kwamba katika malumbano ya hoja yaliyotamalaki kundi moja tu pekee(Kundi C) lilissimama kidete katikia siasa za utaifa. Kwamba tunanyukana na wapinzani wetu kidiplomasia hivyo tunapaswa kuwa kitu kimoja. Lakini kwa makundi ya A na B katu hawataki kuungana kwenye siasa za utaifa. 

Hata hivyo ukizitazama itikadi za vyama vyenyewe vimebaki vituko. CCM kinajipambanua kama chama kinachofuata siasa za ujamaa na kujitegemea, lakini kinacheza ndombolo ya ubeberu. Chadema vilevile kinacheza siasa za ubeberu ilhali mwongozo wa chama ni tofauti kabisa. Vivyo hivyo kwa vyama vingine vilivyoko havijipambanui katika siasa za utafita bali itikadi zao huku vikisahau madhumuni mengine ya kuilinda nchi kwa hali yoyote ileile. 

Tumefika mahali siasa za utaifa hazipendwi ila vyama vyetu vimekuwa ndiyo mahaba mazito pasi na kikomo. Tunavijali vyama kuliko nchi. Tunawajali wanasiasa wetu kuliko tunavyoijali nchi. Hata kama nchi ni wanasiasa lakini hawawezi kuwa bila siasa za utaifa kupewa kipaumbele. Tunanuka u-vyama vya siasa. Maisha yetu yananuka u-vyama vya siasa, na tunashindwa hata kuishi maisha halisi ya kuendeleza nchi yetu. 

Heri ya mwaka mpya 2018!
Wasalaamu!

No comments:

Post a Comment

Maoni yako