NA MARKUS MPANGALA
Ubovu wa Barabara katika kijiji cha Ndumbi. |
RUHUHU
ni miongoni mwa Tarafa zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa. Wilaya hii ni
miongoni mwa zingine kama Songea Vijijini, Songea Mjini, Mbinga, Namtumbo, Tunduru
zilizopo mkoani Ruvuma. Wilaya ya Nyasa ilianzishwa rasmi mnamo Machi 2012 baada
ya kugawanywa wilaya ya Mbinga. Eneo la wilaya ya Nyasa liko kando la Ziwa
Nyasa.
Tarafa
ya Ruhuhu ipo kwenye mwambao huo, ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoachwa nyuma
kimaendeleo na kiuchumi. Tarafa hiyo inazo Kata za; Mbaha, Lituhi, Ngumbo na
Liwundi.
Kwa
mujibu wa sensa ya mwaka wa 2012, Kata ya Mbaha ilikuwa na wakazi wapatao 6,972.
Ni Kata ambayo ndiyo mwenyeji wa Shule ya Sekondari ya Monica Mbega iliyoanzishwa
rasmi mwaka 2006. Jina la shule hiyo lilitokana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Monica Mbega kabla ya kuondoka.
Wananchi
wa Tarafa hii wanakabiliwa na changamoto nyingi mno hali ambayo inadhoofisha
ukuaji wa uchumi. Changamoto hizo zinatokea katika nyakati tofauti na kuziba
mianya ya kujipatia pato kutokana na huduma kadhaa wa kadhaa kuwa dhaifu.
SEKTA ELIMU HOI
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Shule ya Sekondari ya Kata ya Monica Mbega kwa wazazi na
walezi ya Julai 2017 ilisema jumla ya wanafunzi 41 wa kidato cha cha kwanza
walikuwa hawajasoma masomo manne ya Biology, Physics, Book Keeping na Commerce.
Nilipowauliza baadhi ya wanafunzi kuhusiana na suala hilo walidai kuwa kutosoma
kwao masomo hayo ni kutokana na shule hiyo kutokuwa na Walimu wa masomo husika.
Ndiyo
kusema wanafunzi 41 waliongia kidato cha pili mwaka 2018 katika sekondari hiyo
hawafahamu lolote kuhusiana na masomo hayo yaliyotajwa, hali ambayo
inawadhoofisha ukuaji wao wa kitaaluma. Kwamba tunapoteza wataalamu na
kuwafunza watoto wetu elimu duni.
Aidha,
kabla ya serikali kusitisha kuajiri tatizo lilikuwepo. Mwaka 2017 Serikali
kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitangaza ajira za walimu wa
shule za msingi kwa walimu ambao wamemaliza masomo yao mwaka 2014/2015 katika
ngazi ya cheti (III A). Kwamba hapa serikali ilitoa ajira za walimu.
Aidha,
mwaka huo huo Ofisi ya rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilitoa orodha
ya walimu wa Shahada na Stashahada waliopangiwa vituo vya kazi katika shule za
Sekondari mbalimbali nchini. Lakini hakukuwepo na Mwalimu aliyekabidhiwa jukumu
la kufundisha wanafunzi wa Sekondari ya Monica Mbega katika masomo tajwa hapo
juu. Natambua serikali inaweza kujitetea kuwa hiyo ni awamu ya kwanza, lakini
je kuanzia mwaka 2006 hadi hivi leo haikufahamu matatizo ya shule zake za Kata
ikiwemo Monica Mbega? Mazingira ya
aina hii hayatodautiana na hali ya shule za zingine zilizopo Kata ya Ngumbo na
Liwundi ndani ya Tarafa hiyo.
TAABU YA MAWASILIANO, MIUNDOMBINU NA UCHUKUZI
Hili
ni eneo ambalo linaleta simanzi zaidi. Kampuni za Simu nchini hazijafanya
jitihada za kutosha kuwapata wateja wapya katika Tarafa hii pamoja na kutimiza
sheria na matakwa ya serikali kufikisha huduma za mawasiliano vijijini. Nakiri
kuwa kampuni hufuata faida, lakini kwa tofauti iliyopo kati ya miaka 1990 na
sasa ni dhahiri kiwango cha wananchi kutumia simu za mkononi kimeongezeka.
Tatizo linakuja mawasiliano ni hafifu mno.
Upande
wa barabara nimewashuhudia ukarabati ambao ninaweza kusema ni sawa na kumpa mgonjwa
vidonge vya kutuliza maumivu (Panadol) badala ya Mseto (tiba). Ukarabati
unaofanywa ni kwa maeneo korofi lakini hali halisi ya barabara si nzuri.
Ninakumbuka alipokuwa waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, alisema kuwa Serikali
itajenga barabara kwa kiwango cha lami kuunganisha Wilaya ya Mbinga hadi Wilaya
ya Nyasa itakayokuwa na urefu wa Kilometa 67.
Dkt.
Magufuli aliyasema hayo alipokuwa anahutubia mamia ya Wakazi wa Nyasa kwenye
Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa miguu Mbamba bay, mara
baada ya Rais Jakaya Kiwete kufungua Madaraja pacha ya Ruhekei A, B na C
yaliyogharimu kiasi cha Tsh. bil.4.
“Mhe.
Rais napenda kutamka hapa kuwa kama tumeweza kujenga mtandao wa barabara za
lami zaidi ya km. 11,000 nchi nzima hatuwezi kushindwa kujenga km. 67 kwa
kiwango cha lami. Dkt. Magufuli aliongeza kuwa tayari Wizara ya Ujenzi ilitenga
fedha kiasi cha Shilingi Bil. 2.3 katika mwaka wa fedha 2014/15 kwa ajili ya
kuanza ujenzi wa barabara hiyo katika kiwango cha lami,”
Aidha,
Novemba 29, 2017 pia nimepokea taarifa ya Kikao cha Bodi ya Barabara mkoani
Ruvuma ambacho kilitangaza mkandarasi kampuni ya Chicco kupewa zabuni ya ujenzi
wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay. Lakini hakuna maelezo yoyote juu ya barabara
za Mbamba-Lituhi wala Lituhi-Kitai hadi sasa hali ambayo inazidi kuwaweka
gizani wananchi wa tarafa ya Ruhuhu. Halimashauri nayo haina jawabu. Inatuliza
maumivu badala ya kutibu.
Miradi
mingi inaelekezwa kwenye Tarafa ya Ruhekei huku wananchi wa Ruhuhu wakibaki
wakitaabika. Barabara ya Lituhi kwenda Songea ni miongoni mwa barabara kuu tatu
za Jimbo la Nyasa, lakini kinachoendelea huko ni ukarabati, kurundikwa vifusi
na wananchi kubugia vumbi. Barabara ya Lituhi kwenda Mbamba Bay inatakiwa
kufanya mapinduzi makubwa kuliko “kutumia mbinu ya Panadol”. Daraja kubwa na
refu lililopo kijiji cha Liweta likisombwa na maji maana yake mawasiliano
hayatakuwepo hivyo kuleta madhara kwa wananchi.
Kwa
wananchi wa Ruhuhu mawasiliano ni tabu. Barabara ni tabu. Bandari zilizopo ni
tatu; Lundu, Mkili na Ndumbi. Lakini Ndumbi imechaguliwa kujengwa bandari kubwa
kwasababu ya jiografia yake karibu na mji wa Lituhi ambao utaunganisha na
Manispaa ya Songea. Je kwa mazingira ya barabara hiyo mizigo kutokana bandari
itapita wapi? Kwanini wananchi hawa wameachwa ukiwa?
HITIMISHO
Katika
mazungumzo yangu yasiyo rasmi na diwani Kata fulani jimbo la Nyasa ambaye yupo
karibu na Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu Waziri wa Viwanda, Baishara na
Uwekezaji, Stella Manyanya, aliniambia,
“Ni
kweli kuna nakisi Tarafa ya Ruhuhu haipewi kipaumbele kama ilivyo tarafa ya
Ruhekei. Hoja yako ya Tarafa ya Ruhuhu ni sahihi kabisa haina chembe ya uwongo,
kutokana na kutokuwa na mradi mkubwa wa kijamii ukiondoa Bandari ya Ndumbi na
Lile daraja la Ruhuhu, lakini naona Mbunge anawaza kitu upande huu wa Ruhuhu.
Tuendelee kushirikiana.,
No comments:
Post a Comment
Maoni yako