February 22, 2018

UTUKUFU.

Na Kizito Mpangala
Utukufu nikupe au nisikupe? Twasema utukufu kwake yeye aliye juu japo sijui yupo juu ya mti, juu ya paa, au juu ya kichwa cha mtu mwingine au juu ya mnazi, au pengine juu ya mbuyu basi kotekote utukufu uende tu kwa sababu ni juu. KumBe nami nikiwa juu nitapata utukufu, sawa! Lakini utukufu gani nitakaopewa unifanye niwe mtukutu badala ya mtukufu? Unaona sasa, kumbe nikiwa mtukufu sipaswi kuwa mtukutu lakini nikiwa mtukutu sipaswi kuwa mtukufu kwa kuwa watoaji wa utukufu wanapungua, nasema tu wanapungua ingawa siwajui wanaotaka kunipa utukufu kama nisipokuwa mtukutu.
Lakini mimi tu, kweli? Mimi nikipewa nitawapa na wengine utukufu huo ili tuone kama ni watukutu au ni watukufu katika utukufu huo uliotolewa na wenye utukufu wanaoonwa ya kwamba ni watukutu katika akili  na utashi lakini wanao utukufu ambao huwapa wengine na wengine hao wakipewa utukufu huo wanakuwa watukutu kwa kuwa wamepewa utukufu basi pengine ni watukufu kweli kadiri ya wagawaji wa utukufu wanaotazamwa kama watukutu. Jamani mimi nausema utukufu uliotolewa na wenye haki ya kukaa nao na wakawapa wa kuutumia ili wawarudishie mambo matukufu.

 
Jamani mpenzi wangu Aminata, wewe hupendi utukufu wangu nikikupa? Chukua utukufu nilokupa mie mwenye utukufu ili unipe mambo matukufu. Mie sisemi sana maana wewe mpenzi wangu mwenyewe wajua kunipa mambo matukufu tena kwa hiyari yako mwenyewe ulisema nikikupa utukufu basi utanipa mambo matukufu wakati mtukufu. Sasa iweje ukaonekane mtukutu wakati mtukufu huo? Hapana mpenzi wangu Aminata. Pole kwa kuubeba utukufu wangu niliokupa ili nipate mambo matukufu kadiri ya kiwango cha utukufu nilichokupa ingawa sijui wewe mpenzi wangu Aminata upo juu ya nini, pengine juu ya meza, au juu ya kiti, au juu ya mlima, au juu ya mbuyu, au juu ya kichwa cha mtu mwingine, au juu ya mnazi, au juu ya tanuri la matofali yanayochomwa na kadhalika.

Lakini uliniambai kuwa wapo rafiki zako nao wanataka utukufu wapewe na wanaotarajia mambo matukufu wakishautoa utukufu kwa ajili ya faida tukufu wakati mtukufu na mambo matukufu yaje kwa utukufu. Safi. Ila waambie kuwa wakishapewa utukufu huo na wanaotarajia mambo matukufu wakati mtukufu wasiende kuwa watukutu kwa sababu wataongeza uchoyo wa utukufu uwe kwa waliowapa utukufu ili warejeshe mambo matukufu kwao katika muda mtutkufu uliopewa utukufu wa matukufu kuja. Sawa Aminata, we  ni vumilie tu ingawa ilitakiwa nikupe maneno matukufu muda huu mtukufu na katika sehemu hii tukufu yenye rutuba tukufu ya kuzaa watukufu lakini yapo matukufu zaidi ya haya ambayo watukufu wanaozaliwa ndio hutoa utukufu maalumu kwa watu maalumu kama hao rafiki zako ili walete matunda matukufu penye utukufu na pasipo na utukufu ili kote itawale furaha na amani tukufu.

Mpenzi wangu Aminata, nakuona umechoka jamani, pole. Ndio utukufu wenyewe huo na sie tunatarajia kupata mtukufu uliyemuweka sehemu tukufu kwa muda maalumu mtukufu ambaye atakuja kuwa mtoa utukufu katika wakati atakaostahili kutoa utukufu kwa watu maalumu wenye kuhitaji utukufu ili naye afaidi matukufu kutokana na fikra zake tukufu wakati sisi kama wazazi tutakapokuwa na umri mtukufu wa busara tukufu. Natumaini umenielewa. Wengine wanaweza kukuita mama kijacho ila mimi nakuita mama kitukufu.
Hicho kitukufu kikija uwaambie wale rafiki zako kule utukufuni mkutanako nyakati zote tukufu kasrini mwetu tukufu, hawa akina kitukufu wako wengi na wengine wana muda mtukufu wa kutoa utukufu kwa rafiki zako hao kasrini mwetu humu, sasa wasiwaudhi kwa matukutu yasiyotarajiwa na watoa utukufu ka malengo matukufu. Pakitokea kitukufu kimoja kina kipawa fulani hasa kipawa cha kitaaluma basi uwaambie wakiangalie na wakilee vema kwa kanuni tukufu za kasri letu tukufu ili kikawe kitukufu na kuweza kukipa utukufu kipawa chake na utukufu huo uwe sifa njema ya kasri letu tukufu. Pole kwa maneno yangu mengi mama kitukufu, Aminata mpenzi. Siyo lazima kipawa cha kitaaluma tu, wengine wanavyo vipawa vya namna mbalimbali, basi msiwasahau kuwajali kitukufu.

Nakuambia haya ili kasri letu ambalo ninyi mmeshikilia funguo tukufu za milango mitukufu ya kasri hili liende vema hasa kuinua elimu tukufu ambayo hata kitukufu chetu kikaionje muda mtukufu ukifika kwake na kikakijaze kichwa chake kitukufu mambo matukufu. Sasa kwenye elimu tukufu itakayofaa kasrini mwetu humu na utukufu wake ambao tunanyimana kila siku, basi ni vema kila mhadharishaji mtukufu awe anahadharisha somo moja tu na kwa madarasa mawili tu kwa siku moja tukufu ambayo itampa morali tukufu kwa siku itakayofuata kuendeleza machachari matukufu katika somo lake ili vitukufu vyetu baadae tuseme vimeiva kwa taaluma tukufu ambayo sasa ipo kama inanyimwa utukufu wake mtukufu kutokana na baadhi ya watukufu wa kasri letu kuwa na utukutu fulani ambao unavunja ndoa tukufu ya amani na mkewe furaha tukufu. Ndoa hii ikivunjwa basi kamati kwa vijimamlaka vitukufu basi hata kamati iliyoandaa sendiofu tukufu ya binti yao mtukufu Furaha akaolewe na kijana mtukufu na rijali Amani itadai michango yake yote. Hapo ndipo tutakumbuka sindano tukufu ya kufumia sweta la uzi ilipo maana tangu sweta lilipofumwa likawa imara na lilisaidia kuwa kielelezo kwa mafundi waliotaka kufuma masweta yao nao, basi sindano ya kufumia ikisahaulika iliko basi hata kiraka kitukufu hakitafaa kitu kwa kuwa mvaa sweta atakuwa amevumilia baridi kali na sasa atafanya utukufu gani kama si utukutu wa kutafuta sweta tena kwa ghadhabu? Oh! Pole mpenzi wangu aminata kwa kunisikiliza japo najua ilibidi nikupe maneno matukufu na kitukufu chetu kisikie, lakini haya ni matukufu pia maana yanakifaa hata nacho kikija muda mtukufu.
Enhe, nimekumbuka kitu kimoja kizuri sana mpenzi wangu Aminata. Naona kama kinahitaji utukufu kwa lazima na tena katika hicho kitu kuna wanaotaka kuwadharilisha hata wale waliopewa utukufu wa kuondoa ujinga mtukufu wa vitukufu vyetu. Lakini hata hao waliopewa utukufu huo wasivibughudhi vitukufu vyetu hasa vitukufu hivi vyenye ngozi nyororo tukufu tena majamali matukufu kwa urembo asilia kisha wakawapa nundu kubwa tukufu mbele ya tumbo lao halafu wakashindwa kwenda mbele utukufuni mwa taaluma kasrini mwetu ingawa ni changamoto tukufu kasrini mwetu humu, lakini tuuvae utukufu kwanza sisi, uwaambie rafiki zako walioshika funguo za chumba cha dipatimenti ya elimu tukufu wasitumie mikwara mitukufu na mikali mno kiasi kwamba watukufu wengine wanovitukufisha vitukufu vyetu wakajinyonga kwa kitanzi kitukufu kutokana na mawazo halafu habari tukufu ikaja kusema kwamba kajitukufisha kitanzini kwa sababu ya penzi tukufu na mkewe! Pole mpenzi wangu kwa kutega sikio lako kubwa hivyo kama kengele za makanisa ya Kijerumani. Nakutania tu nawe, hee umenuna kiasi hicho? Basi yaishe, nipe msamaha mtukufu mahabubu wangu mtukufu.
Haya basi, twende huku kwenye kanuni tukufu za barabarani ambazo mara nyingi wale watukufu walioshika funguo za makaratasi yaliyoandikwa kanuni tukufu za usalama mtukufu barabarani ili madereva na makondakta watukufu wasifikwe na majanga kwamba kanuni hizo tukufu waziweke wazi tena na tena kwa lugha yetu tukufu ambayo tunafurahia kuzungumzwa na wajerumani au wahidni wakiwa uhindini wakati sisi tunaiona kama ni mavi matukufu! Unajua mpenzi wangu Aminata wewe ni msikivu mno, safi kabisa. Tangu wakati ule mtukufu tulipopewa baraka tukufu na wazee wetu watukufu basi wewe umekuwa mtukufu kuliko mimi kwa sababu pamoja na kufanya kazi tukufu huko utukufuni mwa kasri letu na tena nasikia unawapa adhabu tukufu wale wanaokuwa watukutu kadiri ya sehemu zao tukufu walizopangiwa, lakini ukija hapa nyumbani unakuwa msikivu kwa kiongozi wako wa familia mie mtukutu wa maneno. Basi kawaambie rafiki zako kule utukufuni kwamba wakavifundishe vitukufu vyao maadili matukufu na fikra tukufu kuhusu mahusiano matukufu kati mume na mke ila siyo kila siku makelele matukufu tu kwamba mume wangu hiki au wanaume wa siku hizi hawana utukufu au wanawake wa siku hizi si wa kuwaamini wakati baba yake alikuwa na mwanamke ndipo kwa utukufu mtukufu yeye akazaliwa. Utukufu mbaya uliopo katika hayo ni ubinafsi.
Enhe, nimepata wazo jingine, usichoke kunisikiliza. Hivi unajua ndege ilianzaje? Yaani ilikuwa mzaha tu lakini leo kuna midege mikubwa ambayo ina ubongo mtukufu wa kujiendesha yenyewe halafu mingine nasikia haionekani kwenye rada! Yangu macho tu kwenu tulowapa utukufu kwa upuuzi mtukufu wa kuua vipaji kwa mgongo wa mamlaka fulani halafu wale watukufu weupe wakija kuwachukua wenye vipawa vitukufu na kwenda nao kwao na kuwaimarisha baadae tuseme kuwa siyo wazalendo kasrini mwetu. Uzalendo sio kubeba kitambaa kitukufu cha kasri letu na kujifunika huko waliko, uzalendo mtukufu unaanzia nyumbani kwanza. Kuna kijana mmoja ana kipawa cha ufundi na amekuwa fundi magari mtukufu kwa muda mrefu halafu baadae akaunda helikopta tukufu lakini alipewa mkwara mtukufu hadi leo yuko kimya. Sasa hapo kiwanda kipi kitukufu kitakuwepo bila kujali wenye kipawa. Hata anayeunda magobole nadhani ana kipawa kitukufu basi mchukeni na mpeni elimu tukufu ya silaha kisha aifae kasri yetu kwa kutengeneza silaha tukufu ili ulinzi mtukufu wa kasri yetu uwe imara zaidi, yaani mpeni elimu hiyo tukufu ya silaha kisha asimamiwe na kuwekwa katika mazingira yatakayomwondolea mawazo ya uhalifu mtukufu yaani tumjali.
Jamani mpenzi wangu mtukufu Aminata nashukuru kwa kuwa msikivu hadi sasa. Hivi kule wanakotoa utukufu wa kitaaluma ngazi ya shahada tukufu zile, kwa nini wanafunzi hawa watukufu huwa na mbwembwe nyingi tukufu za maisha matukufu? Utukufu huo wamepewa na nani? Au ni sehemu ya mtaala mtukufu wa elimu tukufu ya juu? Yaani wanafunzi hao watukufu wanaweza kuagiza keki ya shilingi tukufu laki tatu kwa ajili ya sherehe ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa na ni masaa kadhaa tu na wengine wanaweza kuvunja urafiki mtukufu endapo rafiki huyo wa mlengwa hakupata wasaa mtukufu wa kuhudhuria. Nani kawapa utukufu huu? Sawa, walio juu wamepewa utukufu juu ya muembe, au juu ya mpapai au juu ya meza au juu ya paa au juu ya kichwa cha mtukufu mwingine na kadhalika. Keki tukufu ya shilingi laki tatu halafu hana kitabu hata kimoja kinachoendana na kozi tukufu anayoisoma. Halafu muda wa majaribio au mitihani mitukufu anahaha kutaka kuongezewa alama au maksi tukufu. Basi nenda ukawaambie wale walioshika funguo za chumba cha makaratasi yaliyoandikwa kanuni tukufu za mwenendo wa kitaaluma kwamba wawe makini ili wasiazalishe wahitimu watukutu.
Safi kabisa bado umetega sikio. Utukufu huo mliopewa na watoa utukufu kwa matarajio ya mambo matukufu wakati mtukufu basi utukufisheni ipasavyo na siyo tu kwa kuwa utukufu wenu ni mkubwa basi ule mdogo muuyumbishe, jueni kuwa upo muda wa kupumzika utufufni na mtayakuta mawimbi makali yanayoyumbisha utukufu mdogo mdogo mliouyumbisha ninyi pengine kwa sababu zisizotukufu.
Kuna mtukufu wa ardhi, nyumba na makaazi, safi kabisa aliyebuni utukufu huu kwa tarajio tukufu la wale watoa utukufu kadili ya ufafanuzi wa Watukrasia kwamba ni utawala mtukufu wa watoa utukufu, kwa ajili tukufu ya watoa utukufu wapate sehemu tukufu ya maisha matukufu. Lakini mtukufu huyu mara nyingi anadili na ardhi tu. Hivi nyumba na makaazi bora ni ardhi pekee? Hata kushauri watu walao wajenge nyumba za matofali imara na wawe wanafanya marekebisho ya nyumba zao pale penye hitilafu ili wasifikwe na majanga matukufu yanayoweza kuleta hatari tukufu katika maisha yao. Ilitakiwa awe pete na kidole na mtukufu wa mazingira kwamba makaazi bora yanaendana na mazingira bora yenye usafi mtukufu ili afya iwe tukufu, lakini kila siku ni mashauri ya ardhi tu. Mpezni wangu Aminata mimi haya ni maoni yangu matukufu na litakayemgusa tukufu lolote basi ndiyo hivyo ila aniwie radhi yule ambaye tukufu lolote litamuweka pembeni ya utukufu na kuwa utukutuni kisha likamkwaza. Basi siishii hapa tu mpenzi wangu Aminata, ngoja niigawe aya nyingine hapa chini.
Utukufu wa sekta tukufu ya habari, sanaa na michezo ni mzuri mno. Lakini mara nyingi sanaa haipewi utukufu murua. Ikipewa basi ni muziki wa Ubongo Fuleva tu na mabishano matukufu kati ya wasanii wenyewe, vijembe vitukufu kati yao, mapenzi kati yao halafu baadae twamtaka mtukufu wa sekta hii amleta Van Viker aje kasrini mwetu tupige naye picha kisha arudi kwake halafu tuseme kiwanda cha filamu zetu kimepata mgeni kumbe ni kupiga naye picha tu. Hee, mpenzi wangu Aminata utaishia kutazama mazingaombwe ya filamu za Wahindi zenye madoido mengi matukufu ambayo ni ya kufikirika kwa kiasi kikubwa. Ingawaje suala la bajeti tukufu katika kiwanda cha filamu lakini basi hata waandaaji wenyewe wawe na morali ya kutafuta mambo matukufu yanayoendana na filamu ili nasi tukawike hapo baadae.
Haya mpenzi wangu Aminata naiomba radhi yako tukufu kwa kukutegesha masikio yako matukufu. Ningelikuambai mengi lakini mpaka hapa najua kuwa umeshapata mwanga mtukufu wa mwenendo wa tukufu mbalimbali zilivyo, basi kwingine ambako sikugusia wewe utawaambia rafiki zako kule mafunguoni ili majadiliano matukufu yakatamalaki na siyo kuleta mabishano matukufu halafu mkaseme mnawapigania wanyonge watukufu wakati si ukweli mtukufu kwa watoa utukufu, na wakichoka na utukutu basi wao watakuwa na utukufu mwingine watakaouona una utukufu ule walioukusudia.
Lakini nimekumbuka kitu kimoja tu. Samahani kwa kuchomekea chombezo tukufu hili. Ni kwamba kuna waandikaji watukufu wa hadithi au niseme kazi za fasihi tukufu andishi, basi hapo ni chombezo la kwenye sanaa kwa sababu fasihi ni sanaa, hivyo kawaambie rafiki zako kuwa kila mmoja wenu akawatukufishe watoa utukufu kwenye eneo lake tukufu kuwa wawe wanapendelea kujiburudisha kwa hadithi hizo tukufu zilizomo vitabuni na siyo zile za runingani tu. Hata wakijitokeza wawili basi nao watawatukufisha wengine ili kwamba lengo tukufu likaimarike.
Haya basi utukufu ukishatukufishwa, basi kule kutukufishwa kwake kutatukufisha na kuteua tukufisho lipi ni tukufu na tukufisho lipi ni TUKUTU. Kawaambie pia ndoa ya kijana AMANI na mkewe FURAHA isivunjwe kitukutu iwe kwa maneno ya udaku au kwa kuwavamia watoa ukufu hao kasrini ambao ndio watoto wa mzee Amani na Bi Furaha. Wakitoweka wazee hao basi watoto na wajukuu zao hawa watoa utukufu watahangaika mno. Mkakae kwenye makiniko tukufu ili utukufu  wa watoa utukufu ukae nanyi huko juu ya mti, juu ya meza, juu ya paa, juu ya mbuyu na kadhalika.
© KIZITO MPANGALA   

No comments:

Post a Comment

Maoni yako