July 27, 2011

TANZIA; TANGULIA DANNY MWAKITELEKO

MIMI; “shikamoo, naulizia lile shauri langu.

DANNY; Nafahamu, ila halina shaka linazungumzika. Muone Muhingo (Rweyemamu) atakueleza zaidi, tumejadili. Usihofu.

Nayakumbuka maneno hayo kati yangu na aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Daniel Daimon Mwakiteleko, ambayo yalinipa imani juu ya suala fulani lililotokea wakati nikiwa New Habari Corporation.

Hilo lilitokea februari mwaka 2009, na lina kumbukumbu nyingi sana kwangu, ni funzo na falsafa maridhawa kwani nilikuwa kazini na magwiji wa taaluma ya Habari nchini.

Jaribu kujenga picha kufanya kazi na watu hawa; Muhingo Rweyemamu, Danny Mwakiteleko, Ezekiel Kamwaga, Eddo Kumwembe, Mayage S. Mayage, Attilio Tegalile, Rosemary Mwakitwange, Balinagwe Mwambungu, Manyerere Jackton, Robert Komba, Deus Ngowi na wengineo. Ni kumbukumbu muhimu maishani mwangu.

Lakini  kumbukumbu muhimu zaidi ni uwezo wa hayati Danny Mwakiteleko kubadilisha suala gumu kuwa rahisi. Kubadili uchungu kuwa jambo jepesi zaidi, ni hayo ya kukumbukwa nami daima. Hata kama uchungu ulijongea, lakini huelekeza mtazamo chanya.

Lakini kwa hali iliyojitokeza, kupata ajali mbaya baada ya gari yake kugongana na gari kubwa la mizigo (semi trela) katika eneo la Tabata (ToT) kisha kupoteza uhai wake pale Muhimbili Hospitali, inaleta uchungu na kushindwa kuamini kilichotokea.

Danny Mwakiteleko mzaliwa wa Mwakaleli nje kidogo ya mji wa Tukuyu, jijini Mbeya ana mengi aliyotuachia. Ni mengi aliyotufundisha na sisiti kusema ni mmoja wa walimu wangu katika taaluma ya Uandishi wa Habari.

Pamoja na kwamba sikuwa chini yake tangu 2009, lakini kuna mambo mengi ambayo naweza kujivunia. Jambo la msingi ni namna ya kuishi na watu. Namna ya kufanya kazi katika mazingira magumu.

Namna ya kuweza kukabiliana na changamoto kazini na kadhalika. Kwa muda ambao sikuwa chini yake, lakini safari zangu za mara kwa mara pale New Habari Corporation ni kuendeleza mengi tuliyoshirikiana tangu zamani.

Maana kipaji hunolewa. Hii ni kutokana na kuanza kazi hapo nikiwa mwanafunzi wa Chuo Cha Uandishi wa habari cha Royal, kisha mwanafunzi wa sayansi ya jamii na elimu pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Ni fahari kufanya kazi na gwiji Danny Mwakiteleko.

Gwiji ambaye ajali ya gari imekatisha uhai wake akiwa na afya njema. Tangulia Danny, tangulia nasi tutakuja kuungana nawe. Maisha yako duniani hakika yana mafunzo wengi.

Mafunzo yenye nidhamu ya kazi, kuheshimu misingi ya taaluma. Kuheshimu wafanyakazi wote waliokuwa chini yako. Tangulia Danny.

Tangulia tu sisi tupo njiani tukisafiri na kungojea siku zetu. Tunangojea na kujiuliza kama tutarudi na roho zetu. Maisha yetu yana mengi mazuri, kama ambavyo ulivyoshiriki katika taaluma ya Habari, tangu ukiwa Tanzania Daima, Mwananchi, Majira na Habari Corporation.

Ni ujuzi wako uliotufanya wengi tupende kuwa nawe daima. Ni weledi wako uliojuzwa Mzumbe sekondari na kuhitimu mwaka 1988, kisha ukajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Mwaka 1993 ukahitimu chuo kikuu ambako ulipikwa kuwa mtumishi wa taaluma ya habari.

Tangulia Danny ukijua kuwa miaka 45 uliyoishi duniani haioshi kukamilisha yote. Lakini kwa yale uliyotimiza wajibu wako inatosha kushukuru. Nguvu zako kwa miaka 45 tangu uzaliwe ni inaonekana sasa tunapokukumbuka jinsi ulivyokuwa enzi za uhai wako.

Wahenga walisema, utaona umuhimu wa mtu pale anapokosekana. Na sasa umuhimu wako unaonekana na bado mawazo yako yatadumu. Hata nilipokuwa nje ya New Habari Corporation, niliweza kupata mawaidha yako hivyo ulikuwa muhimu.

Nilitarajia kujifunza mengi katika safu yako ya JICHO KONGWE kwenye gazeti la RAI. Lakini majukumu yalikufanya usiandike mara kwa mara. Hata hivyo hizi siyo lawama, bali usimamizi wako kwenye RAI unaonekana kutokana na kutuletea mtindo mpya wa uchambuzi wa gazeti la wiki.

Ni mtindo huu ambao wengi wamechukua toka kwako na kuweka katika magazeti ya kila siku. Ni utoaji wa habari kiuchambuzi uliozama ndani zaidi badala ya kutegemea chanzo cha habari kilivyosema.

Hakika mtindo huu uliotuletea kupitia RAI unastahili pongezi. Unaonesha namna gani Danny Mwakiteleko ulivyojikita na taaluma ya Habari. Tangulia Danny Mwakiteleko, mwana wa Mwakaleli uliyefundishwa kuyafanya makosa kuwa na mtazamo chanya.

Mwana uliyefahamu kuwa mwenye uchungu anahitaji nini na wakati gani afanywe nini. Mtazamo wako mpana wa mambo unaweza kuelezewa na wanafunzi wenzako tangu ulipokuwa Mzumbe sekondari.

Tangulia Danny, ustarehe kwa amani. Lakini umetuachia chama cha waandishi wa habari za bunge. Chama ambacho kilitokana na wazo ulilojenga kichwani mwako hata leo kikapata kiongozi mweledi Godfrey Dilunga.

Ni maneno machache kwangu yanatosha kwakuwa wewe ulikuwa mwalimu na msimamizi wangu. Ingawa nilianza kazi ya uandishi mwaka 2007, lakini ulipofika mwaka 2008 ndipo nikakufahamu wewe Danny Mwakiteleko.

Ni miaka 6 sasa tangu nilipojikita kwenye taaluma ya uandishi wa habari. Lakini nilipata manufaa kuwa nawe kwa miaka miwili (2008-2009).

Mazuri nitendayo ni kutokana na kusimamiwa na ewe mjuzi mahiri. Na leo nakutumia salamu hizi nikisema, daima utakuwa sehemu ya maisha yangu kupitia taaluma ya habari.

Daima utakuwa kiongozi wangu kwa kila jambo kwenye taaluma hii. Na fikra zako zitadumu. Tangulia tu Danny Daimon Mwakiteleko. Tangulia ewe Jicho Kongwe.

Niwape pole wafanyakazi wote wa New Habari Corporation. Wapokee rambi rambi hizi kutoka kwa wenzao walioko chini yangu hapa Maestro Mp Ltd kwani mmiliki na mwenyekiti wao nimesimulia mengi niliyojifunza kwa Danny Mwakiteleko.

Tangulia Danny nasi tutafuata. Niseme tu, “Danny Mawakiteleko, you were too good to be popular and you were too popular to be good”. Ustarehe kwa amani.

1 comment:

Maoni yako