Erik akiwa dimbani
“Soka letu linaumwa. Kwahiyo vijana wadogo kama hawa ni tiba kubwa ya soka letu, tuwekeze kwao.” Haya ni maneno ya Waziri wa Habari na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi wakati akizindua michuano ya Copa Cocacola mwaka huu katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Wakati akizungumzia vijana hao ambao walidhihirisha kwamba nchi yetu imejaliwa vipaji vingi sana vya soka, ndipo upesi nilimkumbuka kijana mdogo kabisa Erik Klaesson, ambaye amejaliwa vipaji vingi maishani mwake, ikiwemo soka.
Ukimtazama umbile lake unaweza kumfananisha na aliyekuwa kiungo mahiri wa Pamba ya Mwanza, Simba ya Dar es salaam na Taifa Stars, Hussein Amani Masha.
Lakini sura yake inakuvuta na kumfananisha na beki mahiri David Luiz wa Chelsea ya England. Erik Kalesson anafanana na beki huyo Mbrazil kutokana na kuwa na nywele nyingi (Afro) ambapo mwandishi wa makala haya anamwita jina la utani, Ras Erik (kwa lugha ya Kiswidi, tamka Irik).
Bila kujali umri wake, anachokuambia kijana huyu utabaini kuwa amejengwa katika misingi imara ya soka. Nilimuuliza juu ya wanasoka mahiri wa Sweden, alisema, “nilipenda kumwangalia Henrik Larsson akicheza hapa Sweden, lakini amezeeka na sasa tunamtazama Zlatan Ibrahimovich, nami nimfikie.”
Anaongeza kwa kusema, “nawapenda Robinho, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Zlatan. Nataka kuwapiku”
Erik Klaesson mapema Jumanne katikati ya wiki alikuwa kwenye mechi za watoto kati ya timu yake ya IFK Skoghall dhidi ya timu ya Norrstrands IF Rod, zote za Sweden.
Uwezo wake kumiliki mpira ni mkubwa kulingana na umri wake. Anaweza kucheza kwa ufasaha beki wa kushoto na kiungo nambari 10. Hii ni kutokana na kasi, chenga na ujuzi wake unaojitokeza tangu akiwa kinda.
Harakati zake za kucheza soka zinamfanya kuwa na ndoto za kuchezea klabu mashuhuri AC Milan ya Italia. Kinda huyu anaeleza wazi hisia zake kwamba hapendi kucheza soka la kulipwa nchini Sweden anakoishi sasa, kwani amepania kucheza nje ya nchi hiyo. Na mawazo yake yanaelekea kucheza ligi kuu ya Italia maarufu kama Serie A, pindi umri wake utakaporuhusu.
“napenda kucheza je ya Sweden hasa Milan. Kama nitaanzia hapa Sweden basi nitachezea timu ya Malmo, naipenda sana,” anasema Erik.
Mwandishi wa makala haya alimuuliza Mama yake, Yasinta Ngonyani juu ya kinda huyo kuchagua timu ya taifa kati ya Sweden au Tanzania.
Naye bila kusita alisema, “Binafsi napenda miaka ijayo achezee Tanzania. Lakini ni ngumu kwa sasa kuzungumzia kwani ana vipaji vingi. Kwa mfano ana kipaji cha kucheza Floorball na Fiddle.”
Hata hivyo aliongeza kwa kusema, “Yeye (Erik) atachagua ni timu gani anataka kuchezea kati ya Tanzania na Sweden, akitaka ushauri wetu atapata, nadhani unajua nipo upande gani hapo.”
Suala hili na wimbi la makinda wengi kukumbwa na tatizo la kuchagua nchi za kuchezea linaendelea kushamiri huku baadhi yao wakiwa na mabadiliko ya uamuzi kulingana na hali halisi inayowatokea wanapochezea nchi fulani.
Kwa mfano mshambuliaji wa klabu ya Sevilla ya Hispania Frederick Kanoute aliichezea timu ya taifa ya vijana ya Ufaransa, lakini aliamua kuacha kisha kuchezea timu ya taifa ya wakubwa Mali, ambako ni asili ya wazazi wake.
Mwingine ni Danny Wellbeck ambaye anachezea timu ya taifa ya vijana ya England na ameshachezea timu ya wakubwa ya nchi hiyo kwenye pambano la kirafiki dhidi ya Denmark. Hata hivyo anaweza kuchagua kuchezea England au Ghana.
Wengine ni Kevin-Prince Boateng ambaye alizaliwa Ujerumani na kuamua kuchezea Ghana ambako wametokea wazazi wake, pia nduguye Jerome Boateng aliamua kuchezea timu ya taifa ya Ujerumani badala ya Ghana.
Lakini kwa upande wa kinda huyu Erik Klaesson moja kwa moja anaweza kuiwakilisha Sweden kutokana na uraia wa kuzaliwa na baba yake, lakini anaweza kufanya uamuzi wa kuchezea Tanzania kutokana na asili ya mama hivyo kuukana uraia wa Sweden.
Uwezekano wa hili la pili ni mkubwa kwakuwa Erik Klaesson amekuwa akiwasili nchini mara kwa mara ndipo ndoto ya kuanzisha timu yake pindi akistaafu soka, ilipoanza kumea. Na vilevile msukumo wa baba yake ambaye ni mpenzi mkubwa wa Tanzania na amekuwa akimweleza kijana huyo umuhimu wa nchi hii.
Akizungumzia, mawazo ya mwanaye miaka ijayo alisema, “huwa anasema anataka kuanzisha timu yake Tanzania pale atakapokuwa mkubwa na ana ndoto nyingi nasi tunazifuata.”
“kuna kipindi alikuwa akienda sana kwenye mazoezi ya Fiddle, lakini akatuambia akili yake inafikiria mpira wa miguu 100% na anahitaji msukumo wetu.”
“nina hamu sana kumwona (Erik) akicheza mpira wa miguu hata kama hatavaa jezi za AC Milan kama anavyoazimia, muhimu ni kucheza mpira wa kulipwa nje ya Sweden, nasi tunakubali hilo.” Anasema Torbjorn Klaesson, baba wa Erik.
Akaongeza kusema, “nikimtazama mtoto huyu (Erk) naamini atakuwa moto wa kuotea mbali, kwanza anabidii, utulivu wake na uwezo wake anapokuwa na mpira. Walimu wake wananiambia subiri matunda kwa kijana wako muda si mrefu.”
“napenda mpira kupita kiasi, na Sweden unajua tunavyompenda Henrik (Larsson) tangu akicheza Glasgow Rangers kule Uskochi (Scotland) na baadaye Barcelona kule Hispania na kidogo Manchester United. Alikuwa na uwezo mkubwa na anajituma, nami sikujua kama nitapaja kijana mwenye kipaji cha soka, lakini naambiwa nivute subira, namuunga mkono,” anasema Torbjorn Klaesson
Alipotokea Erik Klaesson
Kinda huyu kwa sasa ana miaka 11. Alizaliwa tarehe 3/6/2000 nchini Sweden. Ana kipaji kikubwa cha kucheza soka, na michezo mingine kama floorball /innebandy.
Kama tulivyoona hapo mwanzo, baba yake ni Torbjorn Klaesson, raia wa Sweden na mama yake ni Yasinta Ngonyani, ambaye ni Mtanzania na mzaliwa wa Songea mkoani Ruvuma.
Jambo moja kubwa ni kwamba baba wa kijana huyu anapenda mila na desturi za Mtanzania, na hana shaka juu ya mwanaye endapo atachagua kuwakilisha Taifa Stars miaka ijayo.
Kutokana na yeye kuishi na kufanya kazi kwa muda mrefu hapa nchini, suala ambalo anatoa kipaumbele kwa kijana wake ni kumhimiza kutimiza ndoto zake.
Kwa sasa kinda huyu analelewa kwenye kikosi cha timu ya IFK Skoghall ya Sweden ambako anajifunza mambo mengi kuhusu soka. Ni umri huu ndiyo unakuwa tiba kwa wanasoka mahiri ulimwenguni, hivyo kauli ya Waziri wa Habari na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi kuhusu kuwalea vijana inatakiwa kuungwa na mkono.
Kwani tayari tunaye kinda Erik Klaesson mwenye asili ya Tanzania anayekuja juu kisoka aliyeko nchini Sweden. Kazi kwao TFF.
Da Yasinta, hongera kwa malezi mazur yaliyoibua vipaji lukuki vya eric. hakikisha Eric anachezea Tanzania, kwa mama yake akiwa mkubwa. Sijamuona akicheza lakini naamini akiendelea hivyo atakuwa Zidane mpya.
ReplyDeleteMarkus...Erik anasema Ahsante. kazi nzuri Markus. Ahsante sana
ReplyDeleteNjonjo yote ni ya Mwenyezi Mungu. wapi atachezea hata mimi sijui kwa kweli...
Kazi nzuri, na hongera kwa wazazi ambao kwa juhudi zao tunaona matunda yake!
ReplyDelete