Michuano hiyo ilifanyika katika uwanja wa Halmashauri pale Mbinga. Moja ya nyimbo zilizotumbuizwa ilileta simanzi kubwa kwa wanafunzi,walimu,wapenzi wa michezo na wananchi wengine. Wimbo huo ulihusu kuzama kwa Mv Bukoba.
Daima nikikumbuka wimbo huo hunipa majonzi makubwa kwakuwa watunzi walitumia fasihi yenye hisia kuwasilisha. Sababu za kuzama kwa Mv Bukoba zilitajwa.
Tume ikaundwa, na maelezo mengi tukapewa juu ya ajali ile. Ni ajali mbali sana kutokea kwani ilichukua maisha ya watu wengi. Na bahati mbaya alitokea mtu mmoja tu ambaye alipendekeza kutoboa Mv Bukoba ili kuwaokoa abiria.
Naam, ni ushauri mbovu kwakuwa hakujua madhara ya kutoboa (sijui kama alikuwa na ufahamu wowote kuhusu uanamaji au la maana tuliokulia kwenye uvuvi tunajua madhara) meli hiyo ni kusababisha maafa.
Waokoaji kutoka Afrika Kusini walibainisha wazi kuwa kubolewa kwa Mv Bukoba lilikuwa kosa ambalo lilisababisha meli hiyo kuzama zaidi na kugharimu maisha ya watu. Watu walipoteza maisha, vilio vilisikika na nchi yetu ilihuzunika.
Lakini tangu ajali hiyo tumejifunza kitu gani tena? je, ni kweli mungu alisababisha ajali ya Mv Bukoba? Mv Bukoba ilikuwa na matatizo ya kiufundi, kisha ikawa na mizigo mingi,watu wengi kwahiyo tani ziliongezeka.
Mtumiaji wa usafiri wa meli anafahamu kuwa ikiwa inaegemea upande mmoja basi ni ujumbe kuwa kuna tani nyingi kuliko uwezo wake. Ni sawa na watumiaji wa mitumbwi (nimetumia hii nafahamu sana), ukikaa ukingoni na ukawa na uzito mkubwa huku ndani yake kuna mizigo basi ni rahisi kupinduka.
Muulize mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe ambaye amewahi kuapata ajali ya kupinduka na mtumbwi miezi michache iliyopita mwaka huu. Mtumbwi ukizidishwa mzigo (maana kule Nyasa mihogo inasafirishwa sana kwa Mitumbwi) lazima utapinduka bila kujali hali ya hewa.
Pia, waulizeni watumiaji wa usafari wa meli katika ziwa nyasa wataeleza namna wanavyonusurika mara kadhaa kwa usafiri huo. Mwaka 1999 nilipokuwa kidato cha pili, baada ya shule kufungwa nilipanda Mv Iringa kurejea nyumbani Lundu.
Lakini baada ya Mv Iringa kuondoka bandari ya Nkili injini ilileta tatizo. Mv Iringa ikawa inaelea tu. Na tatizo hilo si geni kwa wafanyakazi wa meli hiyo(labda liwe limebadilika miaka mitatu iliyopita kwani sijatumia usafiri huo).
Kilichobaki ilikuwa ni kungojea ‘ifufuke’ ndipo tuendelee na safari. Mv Iringa hii hii iliwahi kupigwa na dhoruba kali mwaka 1995 mara baada ya kuondoka katika bandari ya Lundu.
Nahodha aliamua kuendelea na safari huku akitambua ziwa nyasa lina dhoruba kali sana na siku hiyo ilikuwa hivyo hivyo. Matokeo yake Mv Iringa ilikumbana na kasheshe sana.
Lakini kwakuwa yamepita, na hakukutokea madhara basi tunaishi kwa mazoea kwamba yamepita. Hatujali, ila tunajali wakati wa ajali na kusema mapenzi ya Mungu.
Mv Songea kwa ziwa nyasa ndiyo inaonekana kuwa imara zaidi. Angalau hii inaweza kuonekana kuwa ni meli yenye uhakika lakini kuna nyakati tunatakiwa kuambizana ukweli, ipo siku tutashuhudia maafa zaidi.
Mtu yeyote anayelifahamu ziwa nyasa atakubaliana nami kuwa tunahitaji Meli yenye uwezo mkubwa kuhimili dhoruba maana ziwa hilo si mchezo. Pia katikai ya dhoruba hiyo ni lazima tuongozwe na utashi.
Dhoruba ikikolea ziwa nyasa ni vigumu sana kupita salama eneo la Makonde, Lundu, na Liuli. Maeneo haya yanakuwa na dhoruba kali sana.
Mfano mwingine ni boti moja ndogo iliyowahi kutokea Mbamba Bay kwenda Liuli. Boti hiyo ilijaza mizigo mingi na kelele za abiria hazikusaidia kitu, nao wakakubali kwua sehemu ya tatizo.
Mmoja wa abiria waliokuwepo ni mama yangu mzazi, na masimulizi yake mara nyingi ni namna mizigo ilivyojazwa, ndiyo maana ilinusurika kuzama.
Pia, kuna wazungu fulani (watalii) waliokuwa katika kisiwa cha Likoma kwa upande wa Malawi walijikuta hawana mwelekeo na kupoteza mawasiliano hadi walipookolewa na wavuvi wa kijiji cha Lundo, wilaya Mbinga.
Tatizo lao lilikuwa kiburi ambacho wenyewe walikiri kudharau ushauri kutokana na dhoruba iliyokuwepo. Yote hayo ni akili za binadamu wala tusimsingizie Mungu. Tangu lini Mungu anaua watu wasio na hatia?
Je, ndani ya Mv Bukoba kulijaa Mafarisayo na Masadukayo? Kulijaa walanguzi na watoza ushuru? Kulijaa wanafiki na wasiomsujudia mwenyezi Mungu? Kulijaa wapagani? Hapana si Mungu, uzembe mkubwa sana wa kushindwa kuihangaisha akili zetu.
Turudi katika ajali ya Spice Islanders. Wenzetu wameaga dunia, wakatishwa uhai, wapoteza wapenzi wao, kaka, dada, mama, wajomba, shangazi, binadamu na wajukuu. Inauma sana kuona hilo.
Lakini, mbona makosa yale yale ya Mv Bukoba yamerudiwa? Jaza mizigo, jaza abiria, na abiria nao hawajali, haya twende songa mbele. Katika yote hayo mizigo ililipiwa, abiria wamelipa na fedha nono imepatikana. Fedha halali na si halali, haya songa mbele. Tafakari hilo.
Hakuna Mungu aliyepanga ajali hii. Hii maana yake tumeshindwa kufikiri na kutatua tatizo letu. Siyo sahihi kumsingizia Mungu katika jambo hili. Huu ni wakati wa kujiuliza, meli ilikuwa tani ngapi? Mizigo inatakiwa kuwa tani ngapi? Inabeba watu wangapi? Uwiano wake katika kutembea ni kiasi gani?
Si sahihi kusema Mungu, hiki ni kipindi cha kukasirika. Haiwezekani kwa mara nyingine tumerudia kosa lile lile halafu tukakosa kufikiri na kusema ni mungu. Hii ni mantiki iliyopinda kabisa.
Sawa, wanaosema ajali hiyo ni mapenzi ya Mungu wanashangaza jambo moja tu. Wapo tayari kuona tume inaundwa kuchunguza kiini ya ajali ya Spice Islanders. Hawa wanaosema kuwa ajali hiyo ni mapenzi ya Mungu wanataka tume, ajabu hii.
Kwanza wanasema hupangwa na Mungu. Lakini wakati huo wanaunga mkono kuundwa tume ya kuchunguza. Swali linakuwa hivi; Ikiwa wanajua kuwa matukio hayo ni fumbo, kwamba Mungu anatueleza kitu fulani, kwanini tuunde tume? Kwa msukumo upi? Kwasababu wanasema tume ikiundwa itabainisha kiini cha ajali, lakini wamesahau kuwa wanasema Mungu ndiye mpangaji wa hayo maana yake ni kiini.
Hebu tutumie akili hapa tulizopewa na Mwenyezi Mungu, kabla ya kumsingizia. Kwamba mizigo ilipojazwa ilikuwa amri ya Mungu? Mantiki inakataa kabisa, ajali hiyo si mapenzi ya Mungu.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako